Ndovu mwitu aliingia katika mji mmoja katika jimbo la Bengal Magharibi nchini India na kuhangaisha wakazi kwa saa kadha.
Maafisa walitumia vishale vyenye dawa ya kutuliza wanyama kumtuliza. Lakini tayari alikuwa ameharibu nyumba, magari na pikipiki kabla ya kudhibitiwa.
Hata hivyo, maafisa wa mji huo wa Siliguri wanasema hakuna mtu aliyeumizwa wakati wa kisa hicho. Ndovu huyo baadaye alipelekwa kwenye hifadhi moja ya wanyama ambayo hutumiwa kuwafuga ndovu na wanasema wanapanga kumrejesha porini baadaye. Watu walioshuhudia wanasema ndovu huyo aliingia mjini kutoka msitu ulio karibu na alionekana kuwa na wasiwasi na kukanganyikiwa.
Kisa hicho kimetokea siku chache tu baada ya chui kuingia shuleni na kujeruhi watu sita katika eneo la Bengaluru.
Rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi kuchukua hatua baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alifika huko jana baada ya msafara wake kusimamishwa na wazazi waliomtaka kwenda akajionee jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.
Alifika mwenyewe na kujionea hali ya msongamano mkubwa wa wazazi uliosababishwa na uhaba wa vitanda na nafasi finyu katika wodi hiyo.
"Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso, na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua," alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisimamishwa na kina mama hao alipokuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumuona na kumjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Bin Ally.
Mwezi Novemba, siku chache baada ya kuchukua hatamu, Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika sehemu kuu ya ya hospitali hiyo ya Muhimbili na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan baadhi waliolala chini.
Alifanyia mabadiliko usimamizi wa hospitali hiyo na kumteua Prof Lawrence Mseru kuwa mkurugenzi mkuu.
Kampuni kubwa ya chakula pamoja na vinywaji Nestle imevunja ufadhili wake katika shirika la riadha duniani IAAF ,ikihofia kwamba kashfa ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli inyokumba shirika hilo huenda ikaharibu sifa zake.
Kampuni hiyo kutoka Uswizi imesema kuwa imechukua uamuzi huo mara moja.
Hatahivyo ,rais wa shirikisho hilo Lord Coe amesema kuwa amekasirishwa na uamuzi huo na hataukubali.
Mwezi uliopita,kampuni ya nguo za michezo Adidas ilivunja mkataba wake na shirikisho hilo.
Tumeamua kuvunja uhusiano wetu na mpango wa riadha miongoni mwa jina katika IAAF mara moja. Uamuzi huu unatokana sifa mbaya kutoka kwa umma kutokana na madai ya ufisadi na utumizi wa dawa za kutumia nguvu dhidi ya IAAF.
Tunaamini kwamba hili huenda likaathiri vibaya sifa na sura yetu na hivyobasi tumevunja mkataba wetu na IAAF,ulioanzishwa 2012.
Tumeelezea IAAF kuhusu uamuzi wetu na sasa tunasubiri jibu lao kwamba ushirikiano wetu umekwisha.
Farasi huweza kubaini kati ya mtu aliye na furaha na aliye kasirika kwa kuangalia uso wa mwanadumu,utafiti umesema.
Katika jaribio, kwa kutumia picha za mwanamume wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Sussex walionyesha kwamba farasi wanaofugwa nyumbani huchukizwa na sura zilizokasirika.
Wanasayansi hao wanasema kuwa ufugaji huo huenda umewawezesha farasi kuelewa tabia za binaadamu.
Matokeo hayo yamechapishwa katika jarida la Biology Letters.
Kundi hilo lilifanya vipimo vyake kwa kuwasilisha picha nyingi mbele ya farasi 28.
''Mtu mmoja anashikilia farasi huku mwengine akishikilia picha,''alielezea mtafiti Amy Smith.
Matokeo yake ,alielezea ni kwamba waliangalia picha za watu waliokasirika na jicho lao la kushoto.
Akili za wanyama zimeumbwa kana kwamba hisia zinazotolewa na jicho la kushoto huangaziwa na eneo la kulia la ubongo ambalo hutumiwa kuangazia hisia mbaya.
Watafiti hao pia waliweka vipimo vya moyo katika moyo wa farasi hao ,ambavyo vilibaini kwamba nyuso zilizokasirika hufanya myoyo ya wanyama hao kudunda kwa haraka.
Matokeo kama hayo yameripotiwa miongoni mwa mbwa na kuzua maswali kuhusu ni vipi kuishi na binaadamu kuna badili tabia za wanyama hao.
Wanamgambo wa kiislamu wamefanya mashambulio ya makombora katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Walioshuhudia wanasema wanamgambo hao walirusha makombora hayo usiku kucha na kuwa milipuko kadhaa ilisikika karibu na uwanja mkuu wa ndege.
Hata hivyo hakuna ripoti yoyote kuhusu majeruhi, lakini ripoti zinasema kuwa safari kadhaa za ndege kuelekea Mogadishu zimefutiliwa mbali.
Uwanja wa ndege wa Mogadishu unalindwa vikali na unakaribiana na kambi ya wanajeshi wa kulinda amani wa muungano wa Afrika nchini Somalia.
Kikosi hicho cha wanajeshi elfu ishirini na mbili wa muungano huo wanaunga mkono serikali ya nchi hiyo katika harakati zake za kupambana na wanamgambo wa kiislamu.
Ofisi za umoja wa mataifa pia ziko katika kambi hiyo sawa na ubalozi wa mataifa ya kigeni.
Kufikia sasa hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini wapiganaji wa Al shabaab walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, wamefanya mashambulio kadhaa ya mabomu mjini humo.
Wakati huo huo uchunguzi unaendelea kufuatia mlipuko wa bomu katika ndege moja ya abiria iliyotokea tarehe mbili mwezi huu.
Mlipuko huo ulitokea katika ndege inayomilikiwa na shirika la Daalo muda mfupi tu baada ya kuruka kutoka uwanja huo wa ndege wa Mogadishu na kusababisha kifo cha mlipuaji huyo wa kujitolea, hali iliyoilazimisha ndege hiyo kutua kwa dharura.
Watu kum na watano wamekamatwa kuhusiana na shambulizi hilo la Ndege.
Shule zaidi ya 100 zimefungwa nchini India baada ya chui mwingine kuripotiwa kuonekana viungani mwa mji wa Bangalore.
Wakazi wametakiwa kutotoka nje kwa sababu ya usalama wao. Polisi na maafisa wa misitu wanamsaka mnyama huyo.
Chui dume aliingia katika shule moja Jumapili na kuwajeruhi watu sita waliojaribu kumkamata.
Mwanasayansi na mfanyakazi wa idara ya misitu ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwenye operesheni ya kumdhibiti mnyama huyo iliyodumu saa 10.
Chui wa sasa anadaiwa kuonekana na mfanyakazi wa ujenzi Jumatano eneo la Nallurhalli, karibu na Whitefield, mwandishi wa idhaa ya Kihindi ya BBC Imran Qureshi aliyeko Bangalore anasema.
"Tumeunga makundi ya maafisa wa misitu na polisi ambao wanazunguka eneo hilo wakimtafuta. Lakini kufikia sasa hatujaona dalili za kuwepo kwake,” afisa mkuu wa huduma za wanyamapori jimbo la Karnataka Ravi Ralph amesema. Chui huyo alijeruhi watu sita shule ya Vibgyor Jumapili
Mnamo Alhamisi, serikali ya jimbo hilo iliagiza kufungwa kwa shule 129, zikiwemo 53 za serikali.
“Tutaamua baadaye jioni iwapo shule zitaendelea kufungwa Ijumaa au la. Tunasubiri uamuzi wa maafisa wa misitu na polisi,” afisa wa serikali KS Satyamurthy amesema.
Sensa ya karibuni zaidi ilionesha kuna karibu chui 14,000 nchini India.
Maafisa wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani wamesema wameona ushahidi kuwa serikali ya Rwanda imekua ikichangia matukio ya machafuko katika nchi jirani ya Burundi.
Inaelezwa kuwa Rwanda imekuwa ikiwapa silaha na mafunzo wakimbizi waliokimbia machafuko nchini Burundi.
Burundi imetumbukia mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe tangu Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kugombea uraisi kwa muhula wa tatu.
Maafisa hao wa Marekani wanasema taarifa walizo nazo kutoka kwa maafisa wenzano waliopo kwenye kambi za wakimbizi nchini Rwanda, zinasema Rwanda imekuwa ikihusika na vurugu katika nchi jirani ya Burundi.
Akihojiwa na Bunge la Congress mmoja wa wanadiplomasia amesema kuna taarifa za kuaminika kwamba wakimbizi wa Burundi ikiwa ni pamoja na watoto wamekuwa wakipewa mafunzo katika makambi nchini Rwanda, na kufunzwa kupambana kwa silaha na serikali.
Ghasia zilizuka nchini Burundi mwaka jana baada ya rais wa nchi hiyo kusema atagombea kwa muhula wa tatu.
Serikali za nchi hizi mbili zina makabila ambayo ni mahasimu, na kuna ongezeko la wasiwasi wa kimataifa kuwa mgogoro mwingine wa kikabila inaweza kuota mizizi katika eneo hilo.
Tayari Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda amekanusha tuhuma hizo ambapo amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kutafuta mikakati ya kutatua mgogoro ya kisiasa badala ya kutafuta nani wa kumtupia lawama.
Mwanamume aliyeishi muda mrefu duniani na moyo wa kupandikizwa amefariki, baada ya kuishi miaka 33 na moyo huo.
John McCafferty aliambiwa alikuwa amesalia na miaka mitano pekee ya kuishi alipofanyiwa upasuaji katika hospitali ya Harefield, Middlesex Uingereza mnamo tarehe 20 Oktoba 1982.
Mjane wake Ann amesema: "Miaka 30 iliyopita ilikuwa ya furaha sana. Tulitembea na kujionea ulimwengu.”
Bw McCafferty, kutoka Newport Pagnell eneo la Buckinghamshire, alifariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 73 akitibiwa hospitali ya Milton Keynes.
Alitambuliwa na Guiness World Records mwaka 2013 kuwa mtu aliyeishi muda mrefu zaidi na moyo wa kupandikizwa.
Wakati huo alisema: “Ninataka rekodi hii ya dunia iwapo moyo wote wanaosubiri kufanyia upasuaji wa kupandikiza moyo na kwa wale, ambao kama mimi, wamebahatika kupandikizwa moyo mwingine kama mimi.”
Bw McCafferty alipatikana na maradhi ya moyo akiwa na umri wa miaka 39.
Alifanyiwa upasuaji na Sir Magdi Yacoub.
Upasuaji wa kwanza wa kupandikiza moyo uliofanikiwa ulifanyiwa nchini Afrika Kusini mwaka 1967 na Prof Christiaan Neethling Barnard na kundi la matabibu 30 katika hospitali ya Groote Schuur, Cape Town.
Mgonjwa wao, Louis Washkansky, alifariki siku 18 baada ya kupokea moyo mpya.
Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika eneo la Bondeni Mpeketoni katika jimbo la Lamu.
Waliotekeleza shambulizi hilo wanadaiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al Shabab ambao walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi.
Walioshuhudia shambulizi hilo wanasema kuwa wapiganaji wao waliwaruhusu waislamu kuondoka huku wale waliokuwa wakristo wakishambuliwa kwa visu na wengine kwa risasi .
Wenyeji wanasema kuwa shambulizi hilo lilitokea mwendo wa saa kumi alfajiri.
Watu wengi waliachwa wakiuguza majeraha.
Nyumba kadha za wenyeji ambao sio waislamu zilichomwa moto.
Operesheni ya uokozi inayoendeshwa na maafisa wa usalama inaendelea katika eneo lililoko karibu na msitu wa Boni ambako inadaiwa wavamizi hao walitorokea. Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni
Hii si mara ya kwanza kwa eneo hilo la Mpeketoni kushambuliwa na wanamgambo wa Al Shabab.
Mwaka 2014 wanamgambo wa Al shabab walishambulia mji wa Mpeketoni na kuua zaidi ta watu 60.
Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni walifikishwa mahakamani majuzi na kusomewa mashtaka dhidi yao.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amemsamehe mwanamke aliyekuwa amefungwa jela miaka 10 kwa makosa ya kumuua mumewe.
Mume wa Jacqueline Sauvage alikuwa mlevi aliyezoea kumpiga na alikuwa amembaka yeye na mabinti zake kwa miaka mingi.
Jacqueline alisema mumewe huyo pia alimnyanyasa mwana wao wa kiume, ambaye baadaye alijiua.
Watu zaidi ya 400,000 walikuwa wametia saini ombi la kumtaka Bw Hollande amwachilie huru.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 ataondoka gerezaji katikati mwa mwezi Aprili, mawakili wake wamesema.
Siku ya tarehe 10 Septemba 2010, siku ambayo mwanawe alijiua, Sauvage alimpiga risasi mumewe mara tatu akitumia bunduki.
Alipatikana na hatia na kufungwa jela miaka 10 gerezani Oktoba 2014, na kifungo chake kikadumishwa Desemba 2015 baada ya rufaa yake ya kujitetea akisema kwamba alikuwa anajikinga kukataliwa.
Kesi hiyo iliangaziwa sana Ufaransa, wengi wakitaka haki ya kutumia sababu ya kujikinga kujitetea ipanuliwe.
Walitaka watu walionyanyaswa na kudhulumiwa nyumbani waruhusiwe kutumia haki hiyo kujitetea.
Bw Hollande amefanya uamuzi wake siku mbili baada ya kukutana na mabinti watatu wa Sauvage.
Wagombea wa kiti cha urais wanafanya kampeni zao za mwisho katika jimbo la lowa ambapo upigaji kura wa kwanza katika uteuzi wa vyama utafanyika siku ya Jumatatu.
Kura ya maoni inaonyesha kuwa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump anaongoza kwa asilimia ndogo dhidi ya mwanzake Ted Cruz lakini wote hao wako mbele ya wengine.
Lakini kinyanganyiro katika chama cha Democratic kina ushindani mkali huku aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani Hillary Clinton akiwa mbele ya Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders. Kila mgombea ambaye atateuliwa kutoka kwa kila chama atagombea urais mwezi Novemba.
Mishoni mwa wiki wagombea walifika katika jimbo lisilo na watu wengi la lowa katika dakika za mwisho za kuwarai wapiga kura ambao bado hawakuwa wamefanya uamuzi.
Mshindi wa mwisho wa chama cha Republican katika jimbo la lowa ambaye alishinda uteuzi wa chama hicho ni George Bush miaka 16 iliyopita.
Suala moja ambalo huenda likaathiri shughuli za leo ni hali ya hewa. Watabiri wa hali ya hewa wanasema kuwa huenda theluji ikashuhudiwa leo usiku.
Maafisa 27 nchini China wameadhibiwa kwa kumnyonga kimakosa kijana mmoja kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo Xinhua.
Huugjilt alikuwa ana umri wa miaka 18 wakati alihukumiwa kutokana na mashtaka ya kubaka na kumuua mwanamke mmoja ndani ya choo za kiwanda mwaka 1996.
Mbakaji mmoja alikiri kufanya makosa hayo mwaka 2005 na Huugjilt kuondolewa mashtaka mwaka 2014. Zhao Zhihong aliyekiti kutenda ubakaji huo
Kuondolewa mashtaka si jambo la kawaida nchini China na sio rahisi hukumu kubatilishwa. Maafisa 26 waliadhibiwa kwa kushuswa madaraka.
Wachunguzi katika eneo la Mongolia walikiri kushinikizwa kupata hukumu ya kesi hiyo wakati matumizi ya nguvu kusababisha mtu kukiri kuripotiwa kuongezeka nchini humo.
Wazazi wake Huugjilt walipewa dola 4800 kama msamaha kutoka kwa mahakama wakati hukumu hiyo ilipobatilishwa.
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema amesikitishwa sana kitendo cha kuuawa kwa rubani Mwingereza aliyekuwa akisaidiana na maafisa wa Tanzania kupambana na ujangili.
Rubani wa helkopta Kapteni Roger Gower, alifariki baada ya majangili kuifyatulia risasi na kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na askari wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
Askari mmoja wa Tanzania alijeruhiwa wakati wa kisa hicho.
Tembo watatu pia walipatikana wakiwa wameuawa.
Dkt Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua rubani huyo wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kurugenzi ya mawasiliano ya ikulu.
Polisi tayari wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na mauaji hayo.
Kiongozi huyo amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote.
Amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hilo na wasaidie kuwafichua watu wote wanaojihusisha na ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.
Hivi karibuni, utawala nchini Tanzania umekuwa ukikosolewa kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na uwindaji haramu wa pembe za ndovu.
Uwindaji haramu umeenea sana katika pori ya Maswa na sio tukio la kwanza ambapo wanaharakati wanaolinda wanyama wa porini wanashambuliwa na wawindaji haramu.
Meli ya kubwa iliyoegemea upande mmoja inakaribia kufika katika pwani ya Ufaransa, maafisa wa bahari wanasema, ingawa kuna matumaini ya kuiokoa kabla ya kuzama.
Meli hiyo kwa jina Modern Express ambayo, imesajiliwa Panama, ilianza kulala upande mmoja Jumanne baada ya kutokea kwa hitilafu za kimitambo.
Mabaharia wote 22 wameondolewa kutoka kwenye meli hiyo. Juhudi za kuisimamisha zimefeli, lakini maafisa wanasema jaribio jingine litafanywa leo Jumatatu.
Juhudi za leo zikishindikana, basi meli hiyo itagonga pwani ya Ufaransa kati ya Jumatatu usiku na Jumanne asubuhi.
Hali mbaya ya hewa ilitatiza juhudi za uokoaji Jumapili.
Meli hiyo imebeba tani 3,600 za mbao na mashine kadha za uchimbaji, na imeinama kwa pembe ya kati ya nyuzi 40 na 50.
Ina tani 33 za mafuta. Mwaka 2002, meli ya kusafirisha mafuta kwa jina Prestige ilizama karibu na pwani ya Uhispania na kumwaga mafuta tani 50,000 na kuchafua eneo kubwa la bahari.
Shirika la Afya Duniani (WHO) leo linafanya mkutano wa dharura kujadili kuenea kwa virusi vya Zika.
Mkutano huo mjini Geneva utajadili iwapo mlipuko wa virusi hivyo unafaa kutangazwa kuwa “dharura ya kimataifa”.
Maafisa wa WHO wamesema mlipuko huo wa Zika unabadilika utoka “hatari ndogo hadi kuwa wa hatari kubwa”.
Katika visa vingi, watu walioambukizwa virusi hivyo vya Zika huwa hawaonyeshi dalili zozote, lakini virusi hivyo vinadaiwa kusababisha maelfu ya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo Amerika Kusini. Kutangazwa kwa mlipuko wa sasa wa Zika kuwa “dharura ya kimataifa ya afya ya umma” kutavifanya virusi hivyo kutambuliwa kama hatari kubwa duniani na kupelekea pesa, rasilimali na wataalamu wa kisayansi kutengwa kuangazia tatizo hilo Amerika Kusini na katika maabara kote duniani.
WHO inaangazia sana hasa baada ya kukosolewa kutokana na ilivyoshughulikia mlipuko wa maradhi ya Ebola Afrika Magharibi. ◾ Kundi laomba wenye Zika waruhusiwe kutoa mimba ◾ “Msishike mimba sasa”, mataifa yashauri wanawake
Wengi walisema ilichelewa sana katika kuchukua hatua, na huenda hilo lilichangia vifo vingi. Katika mkutano huo wa leo, wataalamu wa kudhibiti magonjwa, wataalamu kuhusu virusi na wale wanaoangazia kutengenezwa kwa chanjo, watamfahamisha mkugugenzi mkuu wa WHO Dkt Margaret Chan habari muhimu kuhusu mlipuko wa Zika.
Wiki iliyopita, alisema: “ Kiwango cha wasiwasi ni cha hali ya juu, na pia hali ya suitafahamu.
“Kuna maswali mengi, na tunahitaji majibu upesi.”
Nigeria inaomba mkopo wa dharura wa jumla ya dola bilioni tatu unusu kutoka kwa Benki ya Dunia kujaribu kuziba pengo kwenye bajeti yake.
Uchumi wa Nigeria umeathiriwa sana na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Waziri wa fedha nchini humo Kemi Adeosun amesema amekuwa akifanya mazungumzo na maafisa wa Benki ya Dunia.
Hatua ya Nigeria kuomba mkopo wa dharura inashangaza ikizingatiwa kwamba siku chache zilizopita Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilisema haihitaji usaidizi wa kifedha. ◾ Nakala za bajeti zatoweka Nigeria ◾ Nigeria kurudisha fedha zilizoibiwa
Serikali mpya ya Rais Muhammadu Buhari ilikuwa imeacha pengo katika ufadhili wa bajeti yake katika juhudi za kujaribu kusisimua uchumi wa taifa.
Lakini tofauti kati ya mapato na matumizi imeendelea kuongezeka na kuilazimu Nigeria kuomba usaidizi kutoka nje.
Nigeria silo taifa la pekee kuathiriwa na kushuka kwa bei ya mafuta duniani. Azerbaijan, nchi nyingine inayozalisha mafuta kwa wingi, pia imeanza mazungumzo na Benki ya Dunia.
Uchumi wa Venezuela nao umekuwa katika hali ya tahadhari.
Kushuka kwa bei ya mafuta kulichangia sana katika kushuka kwa jumla ya mapato ya taifa Urusi mwaka jana.
Mwenyekiti wa ZEC amesema uchaguzi huo unafaa kurudiwa
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha ametangaza kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi visiwani humo akisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.
Kulingana na mwanahabari wa BBC aliyeko hilo Sammy Awami, mwenyekiti huyo ametangaza hatua hiyo kupitia runinga ya serikali visiwani ZBC.
Bw Jecha amesema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi, kwa mujibu wa taarifa ambayo baadaye imetumwa kwa vyombo vya habari.
Amesema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao".
"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika."
Amesema hilo ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapiga kura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura".
Kadhalika, amesema kura hazikupata ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba ambako amesema kuwa baadhi ya mawakala wa baadhi ya vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.
Ameongezea kuwa vijana katika eneo hilo walivamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kutaka kuzua ghasia, na pia vyama vya siasa vilionekana "kuingilia majukumu ya tume ikiwemo kujitangazia ushindi na kupelekea mashindikizo kwa tume." Hii ni sehemu ya taarifa ya Bw Jecha
"Nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukiwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi," amesema Bw Jecha.
"Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu."
Tangazo la mwenyekiti huyo limetolewa huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda visiwani humo.
Siku moja baada ya uchaguzi kufanywa, mgombea wa chama cha upinzani cha Civic United From (CUF) Seif Sharif Hamad alijitangaza kuwa mshindi, hatua iliyokemewa na chama cha CCM ambacho mgombea wake Dkt Ali Mohamed Shein amekuwa rais wa visiwa hivyo muhula unaomalizika.
Tume ya uchaguzi visiwani humo pia ilishutumu hatua ya mgombea huyo. Kabla ya kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi, tume hiyo ya uchaguzi ilikuwa imetangaza matokeo ya majimbo 31 kati ya majimbo 54 visiwani humo.
Hayo yakijiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania inaendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa urais. Kufikia sasa imetoa matokeo ya majimbo 155 kati ya majimbo 264.
Hizi ndizo sababu nane zilizotolewa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa kisiwani Zanzibar Bw Jecha Salim Jecha kuhusu kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi wa eneo hilo.
1. Makamishna wa uchaguzi katika tume hiyo walipigana kutokana na tofauti zao
2. Makamishna walikuwa na upendeleo fulani.
3. Katika vituo vyengine, hususan kisiwani Pemba,ambacho ni miliki ya Zanzibar, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa.
4. Masanduku ya kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na maajenti pamoja na maafisa wa uchaguzi.
5. Maajenti wa vyama walifukuzwa katika vituo kadhaa.
6. Vijana walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia.
7. Vyama vya kisiasa vimekuwa vikiingilia tume hiyo.
8.Kura ziliharibiwa hususan zile kutoka Pemba
Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CHADEMA Edward Lowassa amesema kuwa hatokubali matokeo ya uchaguzi wa urais yanayoendelea kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC).
Kiongozi huyo amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha kwamba kuna udanganyifu uliofanyika.
Amesema kuwa kura za chama hicho zimepunguzwa katika vituo vingi vya kupigia kura.
Akihutubia wanahabari pamoja na viongozi wengine wa upinzani, amesema kwamba kura zilizohesabiwa katika maeneo tofauti haziambatani na matokeo yaliyotolewa.
Lowassa ameongezea kwamba maeneo yote ambayo walipata ushindi yamecheleweshwa. Aidha, amelalamikia kukamatwa kwa maajenti wa chama hicho akidai kuwa ni ishara za kutaka kuiba kura.
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa limefanikiwa kuwakomboa watu 338 kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram.
Wapiganaji 30 waliuawa kwenye operesheni hiyo kwenye ngome moja ya kundi hilo katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo mnamo Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi Kanali Sanni Kukasheka Usman, wanajeshi walishambulia kambi za wapiganaji hao kwenye msimu wa Sambisa na kukomboa watoto karibu 200, wanawake mia moja na wanaume wanane.
Mwandishi wa BBC aliye Abuja Chris Ewokor anasema kufikia sasa hakujatolewa maelezo zaidi kuhusu watu waliokombolewa.
Operesheni hiyo ni moja ya operesheni kubwa zaidi kufanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya wanamgambo hao.
Jeshi linaonekana kujikakamua kutimiza makataa ya miezi mitatu ambayo walipewa na Rais Muhammadu Buhari kuwashinda Boko Haram, ingawa muda unayoyoma.
Wanamgambo hao wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya kujitoa mhanga na kuua watu wengi kaskazini mashariki mwa taifa hilo, wengi wao waumini wa dini ya Kiislamu misikitini.