Monday, 15 June 2015

Waislamu Uingereza watakiwa kufungua mapema


Kiongozi wa kidini anayehusishwa na wakfu wa kiislamu nchini Uingereza anasema kuwa waislamu nchini humo wanapaswa kupunguza muda wanaofunga kula na kunywa wakati wa ramadhan kwani muda wao unazidi saa 19.

Dakta Usama Hasan ambaye ni msomi katika shirika moja linalowashughulikia waislamu Quilliam anasema japo mafundisho ya dini yanamtaka muumini wa dini hiyo kufunga kula na kunywa kuanzia asubuhi hadi jua linapotua waislamu nchini Uingereza hulazimika kufunga kwa zaidi ya saa 19.

Wito wake hata hivyo unapingwa na baadhi ya waislamu ambao wanasema kuwa ni sharti maadili na mafundisho ya dini yaheshimiwe.

Waislamu wanahitajika kususia kula kuanzia alfajiri hadi jua linapotua
Ratiba ya kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadan inatarajiwa kutolewa wakati wowote tayari kwa waislmu kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya dini hiyo.
Share:

Msafara wa baiskeli Tanzania


Mamia ya waendesha baiskeli walijitokeza kwenye msafara katika barabara za mji wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia zaidi usafiri huo kwa ajili ya afya bora huku wakiitaka serikali kupinga uonevu unaofanywa na waendesha magari ambao husababisha ajali za barabarani.
Huu ni mwaka wa tisa sasa msafara huu umekuwa ukifanyika jijini Dar es salaam
Mbali ya kuwa ni tukio la burudani baina ya marafiki na familia, msafara huu una ujumbe maalumu
"msafara huu ni wito kwa serikali na wadau wa miundombinu kutenga sehemu mahususi ya kupitisha baiskeli"

Dar es Salaam ina watumia barabara zaidi ya laki tatu .
Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya waendesha baiskeli mjini Dar es salaam UWABA Mejah Mbuya ,anasema idadi ya watumia baiskeli wanaofariki kutokana na ajali za barabarani ni asilimia 6 vifo vyote vitokanavyo na ajali barabarani.
''Anasema kuwa siku hii ni kubwa kutokana na kutokuwepo kwa waoneaji wa magari, lakini anatamani hali hii ingekuwa ni ya kila siku''
Hata hivyo, waandaaji wamesema tayari mabadiliko yanaonekana ndani ya miaka mitano iliyopita.

Shughuli hii inalenga kuondoa dhana kwamba ni chombo cha usafiri kwa watu maskini.
Anasema kuwa ''serikali imekuwa pamoja nao katika mipango yao ya miundombinu mijini kwa sababu ya misafara hii, na kuwa punguzo la vifo vya waendesha baiskeli''.
Shughuli hii inalenga kuondoa dhana kwamba ni chombo cha usafiri kwa watu maskini.
Na ukiangalia watu wanaotumia baiskeli siku hizi , unaona mambo yameanza kubadilika.
Utaona watu wenye uwezo wa kati na wale wa juu nao wameanza kuutumia.
Share:

Kasisi basha aishtaki kanisa kumbagua


Kasisi mmoja ambaye alinyimwa leseni ya kufanya kazi kama mhudumu katika zahanati ya afya kwa misingi ya kuwa katika ndoa ya jinsia moja ameishtaki kanisa kwa kumbagua.
Kasisi Jeremy Pemberton alikuwa amewasilisha pendekezo la kutaka kuhudumu kama Kasisi katika kanisa lililoko ndani ya hospitali.
Aidha kasisi Pemberton anadai kuwa maombi yake yalipingwa kwa kinywa kipana na kaimu askofu wa Southwell na Nottingham nchini Uingereza.
Rt Revd Richard Inwood alimkashifu kasisi Pemberton kuwa katika ndoa na mwanaume mwenza ambaye ni kinyume na mafundisho ya kanisa la Church of England.
Tume inayosimamia utoaji kazi nchini Uingereza inatazamia kuanza kuisikiza kesi hiyo leo.
Wadau wa maswala ya ajira wanasema kesi hiyo inatumiwa kama funzo na mtihani kwa tume hiyo ya ajira ya uingereza iwapo itazingatia haki za wafanyikazi ama zile za mwajiri.
Kasisi Pemberton alikuwa mhudumu wa kwanza kanisani kuoa nchini Uingereza.
Pemberton alifunga pingu za maisha mnamo mwezi wa Aprili mwaka wa 2014.
Askofu Inwood, alimnyima kazi kasisi Pemberton, na kisha akaiandikia barua bodi inayosimamia hospitali hiyo ya Sherwood Forest akiwashauri wasimpe kazi kasisi Pemberton.
Share:

Mwanajeshi wa Korea Kaskazini atorokea Kusini


Jeshi nchini Korea Kusini linasema kuwa mwanajeshi wa Korea Kaskazini ametoroka nchi hiyo na kuingia nchini Korea Kusini akipitia mpaka wa mkoa wa Gangwo

Mpaka wenye ulinzi mkali wa mkoa wa Gangwo
Kuhama kwa wanajeshi kupitia mpaka huo ulio chini ya ulinzi mkali si jambo la kawaida.
Korea Kusini ilichukua hatua za kuboresha ulinzi kwenye mpaka kufuatia tukio la mwaka 2012 wakati mwanajeshi mwingine kutoka Korea Kaskazini alivuka mpaka usiku wa manane na kuingia nchini Korea Kusini.
Share:

Amama Mbabazi atampinga rais Museveni


Waziri mkuu wa zamani wa Uganda Amama Mbabazi atampinga rais Yoweri Museveni kuwania tikiti ya urais wa chama cha NRM.
Bwana Amama Mbabazi anataka kuwania kiti cha urais dhidi ya mwandani wake wa zamani katika uchaguzi utakaokuwa mwakani.
Kupitia kwa taarifa aliyoichapisha kwenye mtandao wa Youtube, bwana Mbabazi aliahidi
''kufufua na kuleta muamko mpya nchini Uganda.''
Rais Museveni ametawala Uganda tangu mwaka wa 1986 na anatarajiwa kuwania urais kwa muhula wake wa nne.

Museveni alimfuta kazi bwana Mbabazi mwaka uliopita katika hatua iliyotafsiriwa na wachanganuzi wa kisiasa nchini humo kuwa mbinu ya kukandamiza mpinzani wake mkuu.
Bwana Mbabazi anakabiliwa na changamoto kubwa ya kushinda uteuzi katika chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).
Rais Museveni tayari ameidhinishwa na kamati kuu ya chama japo anahitaji kupokea ithibati ya wanachama katika mkutano mkuu wa wajumbe.
Iwapo atakonga nyoyo za wajumbe wa NRM sasa Mbabazi sasa atawania urais dhifi ya Museveni
Mwandishi wa BBC Rachael Akidi anasema kuwa hii ndiyo itakayokuwa mtihani mkubwa zaidi kuwahi kumkabili rais Museveni ndani ya chama cha NRM.
Share:

Al Shabaab 1 raia wa UK auawa Kenya


Utafiti wa DNA unatarajiwa kuthibitisha kuwa mmoja wa wapiganaji 11 wa Al shabaab waliouawa na wanajeshi wa Kenya hapo jana alikuwa ni raia wa Uingereza.
Duru za kijasusi za jeshi la Kenya zinasema kuwa mmoja kati ya watu wawili wazungu waliouawa anafahamika kama Thomas Evans, 25, ambaye ni raia wa Uingereza na anayetokea Buckinghamshire.
Bwana Evans, alisilimu na kubadili jina lake na kuitwa Abdul Hakim.
Familia yake imeiambia BBC kuwa inasubiri hakikisho kutoka kwa serikali ya Uingereza kuwa ndiye aliyeuawa.
Shambulizi hilo lilitokea jana alfajiri katika kambi ndogo ya kijeshi iliyoko Baure karibu na Lamu ambapo wanajeshi sasa wamethibitisha kuwa waliwauawa watu 11 na kupata bunduki 13 na mizinga mingine tano.

Maafisa wa utawala nchini uingereza wanashirikiana na utawala nchini Kenya kubaini haswa ni nani aliyeuawa.
Kwa mujibu wa polisi katika bonde la Thames nchini Uingereza , mamake Thomas bi Sally Evans amenukuliwa akisema kuwa ''yeye na mwanaye Michael wanasubiri thibitisho kutoka kwa duru za polisi''
Awali Familia yake ilikuwa imeilaumu idara ya uhamiaji ya Uingereza kwa kumruhusu kuondoka nchini humo.
Evans alisafiri kuelekea Misri mwaka wa 2011 punde baada ya kunyimwa ruhusa ya kuenda Kenya.

Mnamo mwaka wa 2012 Evans inafahamika alimuarifu mamake kuwa amesafiri hadi Somalia kujiunga na wapiganaji wa kundi la Al Shabaab.
Takriban raia 50 wa Uingereza wanaaminika kuwa wamejiunga na al-Shabaab nchini Somalia.
Kundi hilo ndilo linalolaumiwa kwa kutekeleza mashambulizi kadha nchini Kenya na pia Somalia.
Iwapo mwili huo utathibitishwa kuwa wa Evans basi itakuwa ndio mara ya kwanza kwa raia wa Uingereza kuuawa cnhini kenya akipigania kundi la wanamgambo wa Al Shabaab.
Share:

Bashir amewasili mjini Khartoum Sudan..


Rais Omar al Bashir wa Sudan amewasili mjini Khartoum Sudan kutoka nchini Afrika Kusini.
Rais Bashir amekariri kuwa hana hatia yeyote wala hajui kwanini mahakama ya kimatiafa ya ICC inasisitiza kumchafulia jina.
Shirika la habari ya AFP limemnukuu rais Bashir akifoka ''Allah Akbar'' aliposhuka kutoka kwa ndege iliyombeba.
Aidha aliinua mkongojo wake juu na kushabikiwa na wafuasi wake.
Waziri wa maswala ya kigeni wa Sudan Ibrahim Ghandour aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ya Afrika Kusini ilikuwa imemkariria rais Bashir kuwa kuwepo kwake mjini johannesburg ilikuwa ni tukio la kushabikiwa na lenye heshima kubwa kwa hivyo hakukuwa na uwezekano wowowte wake kukamatwa.

Rais Huyo alikuwa ameratibiwa kuhutubia umma lakini kinasa sauti kikaharibika na akaondoka.
Rais bashir aliingia katika gari lake lililowazi na akaondoka uwanjani huku akishabikiwa na wafuasi wake.
Awali kuondoka kwake nchini Afrika Kusini kulikumbwa na atiati, baada ya mahakama moja kuamuru rais huyo asiondoke nchini humo hadi mahakama hiyo itakaposikiza kesi na kuamua iwapo atakamatwa na apelekwe mjini the Hague Uholanzi au la.
Awali Mwandishi wa BBC aliyeko Afrika Kusini Nomsa Maseko, alisema kuwa ndege ya rais al Bashir ilijazwa mafuta jana usiku na kuwekwa mstari wa mbele tayari kabisa kuondoka katika uwanja wa ndege wa kijeshi.

Rais Bashir aliondoka licha ya kuwepo amri ya mahakama ya kumzuia kuondoka nchini humo hadi kesi dhidi yake itakaposikizwa na kuamuliwa.
Mahakama hiyo ilikuwa inapaswa kuamua ikiwa Bwana al-Bashir atakabidhiwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC yenye makao yake mjini Hague Uholanzi ilikukabiliana na mashtaka ya uhalifu wa kivita na mauaji yahalaiki yanayomkabili .
Majaji watatu waliokuwa wanasikiza kesi hiyo dhidi yake wamemtaka waziri wa usalama wa ndani nchini humo kueleza ni vipi rais Bashir aliruhusiwa kukaidi amri ya mahakama .
Share:

Friday, 12 June 2015

WHO:Ebola yaongezeka Guinea na S Leone..


Shirika la afya duniani WHO limeelezea wasiwasi wake kwamba visa vipya vya maambukizi ya maradhi hatari ya Ebola vimeongezeka huko Guinea na Sierra Leone katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
WHO liliripoti kesi 31 mpya katika mataifa hayo mawili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tamaduni za mazishi ndizo zinachangia kusambaa kwa kasi kwa maradhi hayo licha ya tahadhari na mafunzo kupewa raia wa nchi kwamba waripoti visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya maambukizo ya Ebola na kuachia maafisa wa matibabu shughuli za mazishi ili yafanyike kwa utaratibu uliofuatwa.
Share:

Nigeria na mikakati dhidi ya Boko Haram...


Serikali ya Nigeria na nchi nyengine nne majirani zimekubaliana kuunda vikosi vya jeshi la pamoja ili kupambana na wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram.
Kikosi hicho kitapiga kambi katika mji mkuu wa Chad, Ndjamena, lakini kitakuwa chini ya usimamizi wa Nigeria.Nchi ya Chad, Cameroon, Niger na Benin pia zitatoa wanajeshi wake.
Baada ya mkutano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, katibu mkuu wa wizara ya ulinzi ya Nigeria, Aliyu Ismail, amesema kikosi hicho kitakuwa tayari kuanza kazi ifikapo mwezi July mwaka huu:"viongozi wa nchi na serikali za nchi za ukanda wa ziwa Chad na Benin zimechukua uamuzi ufuatao.
kupitisha dhana ya ufanyaji kazi, mikakati ya ufanyaji kazi na nyaraka zinazohusiana na kuundwa kwa vikosi vya pamoja katika kupambana na kundi la kigaidi la wapiganaji wa Boko Haram, kupitisha kupelekwa kwa vikosi hivyo katika makao makuu ya Ndjamena, Chad, kwa utekelezaji wa rasilimali watu na mahitaji ya kifedha.
Share:

Gari linalohisi mashimo barabarani..


Watafiti wa gari aina ya Landrover Jaguar wametengeza gari ambalo linaweza kuhisi mashimo yalio barabarani wakati linapoendeshwa.Sensa zilizopo katika gari hilo hubaini mashimo hayo na hutuma ujumbe wa data hiyo kwa haraka kwa madereva na mamlaka ya eneo hilo.
Share:

Mtoto azaliwa kutokana na mayai yaliohifadhiwa..


Mwanamke mmoja nchini Ubelgiji amekuwa wa kwanza duniani kujifungua mtoto kwa kutumia upandikizaji wa mayai ya mwanamke yaliowekwa katika jokovu alipokuwa mtoto.
Msichana huyo wa miaka 27 alikuwa na mayai yaliotolewa akiwa na umri wa miaka 13 kabla ya kuanza kupewa matibabu ya anemia ya seli.
Mayai yake yaliosalia yalifeli kutokana na matibabu hayo hatua ambayo ingeathiri uwezo wake wa kushika mimba bila upandikizaji huo.
Wataalam wanatumai kwamba mpango huo huenda ukawasaidia wagonjwa wengine wadogo.
Mwanamke huyo alijifungua mvulana mwenye afya nzuri mwezi Novemba mwaka 2014 na maelezo kuhusu swala hilo yalichapishwa siku ya jumatano katika jarida la kizazi cha binaadamu.
Mwanamke huyo ambaye hakutaka kujulikana alipatikana na ugonjwa wa anemia ya seli alipokuwa na umri wa miaka mitano.

Alihamia kutoka jamhuri ya Congo na kuelekea Ubelgiji ambapo madaktari waliamua ugonjwa wake ulikuwa hatari kwa yeye kufanyiwa upandikizaji wa uboho kwa kutumia tishu za kakaake zinazofanana na zake.
Lakini kabla ya kuanza upandikizaji huo walitakiwa kutumia kemikali ili kutibu mgonjwa huyo kwa lengo la kudhoofisha kinga yake ili kuzuia kutokataa tishu hiyo.
Matibabu ya kutumia kemikali yanaweza kuharibu kazi ya mayai hayo,kwa hivyo walitoa mayai yake ya upande wa kulia na kuyaweka katika jokovu.
Wakati huo,alikuwa akionyesha ishara za kubalekhe ,lakini alikuwa hajaanza kupata hedhi.Mayai yake yaliosali yalifeli akiwa na umri wa miaka 15.
Miaka kumi baadaye ,aliamua kwamba angetaka kupata mtoto,hivyobasi madaktari wakapandikiza mayai yake katika mayai yaliokuwa yamesalia na mayai mengine 11 katika sehemu zake nyingine mwilini.

Mgonjwa huo alianza kupata hedhi baada ya miezi mitano na kushika mimba akiwa na umri wa miaka 27.
Mkunga aliyeongoza tiba hiyo ya kumwezesha mgonjwa huyo kuweza kushika mimba Daktari Isabelle Demeestere alisema kuwa kuna matumaini kwamba mpango huo unaweza kuwasaidia vijana wengine ambao wanakabiliwa na hatari ya kufeli kwa mayai yao ya uzazi,hasa kutokana na ongezeko la idadi ya waathiriwa wa muda mrefu wa magonjwa ya damu wakiwa watoto.
Share:

Akosa taji la urembo kwa picha za uchi


Kwa mara ya pili mfululizo waandalizi wa shindano la malkia wa urembo nchini Zimbabwe wametupilia mbali ushindi wa taji hilo uliomwendea malkia wa urembo kufuatia sakata ya picha za uchi.
Emily Kachote alikuwa ameshinda taji la malkia wa urembo nchini Zimbabwe mnamo mwezi Aprili na alitarajiwa kuwakilisha taifa hilo katika mashindano ya dunia ya malkia wa urembo nchini Uchina mnamo mwezi disemba.
Lakini waandalizi wa taji hilo wanasema kuwa bi kachote alikiuka sheria ya shindano hilo ambalo linapinga wanaoshindana kupiga picha za uchi .
Share:

Nyota wa filamu ya Dracula afariki..


Mwigizaji wa siku nyingi na nyota wa filamu zilizopendwa na wengi Sir Christopher Lee amefariki akiwa na umri wa miaka 93.
Msanii huyo ambaye ni mzaliwa wa Uingereza aliyejenga jina lake kwa kuigiza katika filamu ya Dracula na Frankenstein katika filamu ya kutisha aligiza katika zaidi ya filamu 250.
Alijulikana sana kwa kuigiza kama Scaramanga katika filamu ya James Bond na Evil Wizard Suriman katika filamu ya Lord of the Rings.
Msanii huyo pia ameigiza katika filamu za The Wicker Man na Stars wars.
Inaripotiwa kuwa mwigizaji huyo alifariki siku ya jumapili katika hospitali ya Chelsea Westminster mjini London baada ya kulazwa na ugonjwa wa tatizo la mapafu na moyo.
Share:

Bajeti za Afrika mashariki zasomwa..


Serikali za Afrika mashariki zimetumia kodi kuvitahadharisha viwanda vyake kwa upande mmoja na kuwapa motisha wananuzi wa bidhaa kutoka nje wanaosaidia sekta muhimu kama vile miundo mbinu,kawi mbali na utekelezwaji wa itifaki ya soko la pamoja.
Katika mapendekezo ya bajeti yaliosomwa siku ya alhamisi Kenya, Uganda Rwanda na Tanzania zimepunguza kodi za bidhaa zinaozoagizwa kutoka nje kwa sekta muhimu kama vile kawi,mawasiliano na miundo mbinu.
Kulingana na gazeti la the east African nchini Kenya, shinikizo la kuimarisha miundo mbinu, kupunguza gharama ya kufanya biashara na kuongeza mtiririko wa mapato kutoka kwa mafuta na gesi iliogunduliwa katika eneo la Afrika mashariki umeyafanya mataifa manne ya eneo hili kushusha masharti ya sera za kodi ili kurahisisha biashara na majirani zao pamoja na mataifa ya kigeni.
Rwanda imepunguza kodi katika magari yanayoagizwa kutoka nje hususan matinga tinga,malori pamoja na mabasi ya uchukuzi.
Tanzania kwa upande wake imechukua mkondo kama huo na kupunguza kodi ya kuagiza bidhaa kutoka nje kutoka asilimia 25 hadi 10 miongoni mwa mabasi yanayobeba abiria 25 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uwiano wa kikanda unalenga kurahisisha biashara na kuzuia hasara inayokumba kampuni zinazofanya biashara katika eneo hili.
Hatahivyo,wafanyibiashara katika mataifa kama vile Rwanda na Uganda wanalazimika kulipia hasara inayotokana na masharti ya kibiashara yaliowekwa na wasanifu.
Ili kuondoa matatizo hayo Kenya imetangaza kuwa inapunguza masharti kadhaa ya kibiashara kupitia kuondoa forodha ya usalama katika uagizaji wa sukari ya viwanda na unga na ngano.
Uganda nayo imechukua mkondo huo kwa kuondoa forodha yake ya usalama kwa bidhaa na kuanzisha mtindo wa kulipa unaojulikana ambao unalenga kuleta uwiano.
Share:

Monday, 8 June 2015

Jack Warner azidi kuchunguzwa.


Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Kandanda duniani FIFA Jack Warner amekumbwa na kashfa ingine na uchunguzi dhidi yake kuhusiana na kupotea kwa fedha ambazo zililengwa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililoikumba Haiti mwaka 2010.
Warner aliitembelea nchi hiyo miezi kadhaa baada ya tetemeko hilo a kuchangisha kiasi cha dola dola mia saba na elfu 50 kutoka FIFA na shirika la mpira wa miguu la Korea kusini kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo.
Lakini hata hivyo, Wachunguzi wa kashfa hiyo rushwa inayoikabili FIFA wanasema fedha hizo zilihamishwa katika Akaunti inayodhibitiwa na Bwana Warner kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Miaka minne baadaye fedha hizo bado hazijatolewa maelezo.Warner mwenyewe amekana tuhuma zote zilizotolewa dhidi yake.
Share:

Lewis Hamilton afurahia ushindi


Dereva wa mbio za magari ya Langalanga Lewis Hamilton, amekiri kuwa alihitaji ushindi kwenye mashindano ya Canadian Grand Prix baada ya kuibuka kidedea mara nne katika mashindano saba ya msimu huu.
Lewis hakufanikiwa kushinda katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Monaco kutokana na matatizo ya kiufundi yaliyoikumba gari lake. ''Sikuhitaji ushindi? Nafikiri nilihitaji" alisema Hamilton.
''Hakika tulipata tatizo ambalo lilimwezesha Nico kushinda mbio zile, lakini kwa ujumla nilikuwa na kasi nzuri kwa mashindano mawili ya mwisho kwahiyo hairidhishi, ni vizuri kuendelea na nguvu nzuri na inapendeza kuona timu ikiendelea kuwa na nguvu huku ikisonga mbele.

Hilo ndilo jambo la kuvutia zaidi" aliongeza mchezaji huyo.
Meneja mkuu wa Mercedes Toto Wolff, amesema timu yao imepitia katika wiki mbili ngumu kutokana na ukosoaji mkubwa walioupokea kutokana na makosa ya Monaco ambayo yamepelekea kufanya tathmini kuhusiana na maamuzi ya kiufundi ya mbio.
Share:

Google yamuorodhesha Modi kama muhalifu


Kampuni ya mtandao wa Google imeomba radhi baada ya picha za waziri mkuu wa India Narendra Modi kuonekana katika picha za watu kumi wahalifu.
''Tunaomba radhi kwa kuchanganyikiwa na kutoelewana ambako kumesababishwa na picha hizo'',taarifa iliotoka kwa kampuni hiyo ilisema.
Picha za Modi zinaonekana unapowatafuta watu 10 wahalifu pamoja na magaidi,wauaji na madikteta.

Viongozi wengine duniani waliomo katika orodha hiyo ni aliyekuwa rais wa Marekani George Bush na Libya Muammar Gaddafi.
Viongozi wengine wakuu wanaopatikana ni waziri mkuu wa Delhi Arvind Kejriwal,wakili Ram Jethmalani na mtoro Dawood Ibrahim pamoja na mwigizaji wa Bollywood Sanjay Dutt ambaye kwa sasa anahudumia kifungo kutokana na mlipuko mkubwa uliotokea mjini Mumbai mwaka 1993.
''Haya matokeo yanatushangaza na hayawakilishi maoni ya Google'',kampuni hiyo ilisema katika taarifa yake iliotolewa jumatano usiku.

Kampuni hiyo imesema kuwa matokeo hayo yanatokana na gazeti moja la Uingereza ambalo lilichapisha picha ya Modi kimakosa.
Msamaha huo unajiri baada ya wanasiasa wengi wa India kuonyesha wasiwasi wao katika mitandao ya kijamii.
Share:

Polisi asimamishwa kazi Marekani..


Polisi mmoja mzungu katika jimbo la Texas nchini Marekani amesimishwa kazi baada ya video moja kuwekwa kwenye mitandao ikionyesha akihangaisha kundi moja la vijana wengi wao wakiwa ni weusi.
Afisa hiyo anaonekana akiwalenga vijana wawili wa kiume kwa bunduki yake huku pia akimuangusha chini na kumkamata msichana wa umri wa miaka 14.
Polisi hao walikuwa wameitwa na wenyeji waliokuwa wakilalamikia kuwepo usumbufu kwenye kidimbwi kimoja cha kuogelea.

Mkuu wa polisi McKinney anasema kuwa, anachunguza tukio hilo ambalo linafanyika wakati kuna misukosuko baina ya jamii za watu weusi nchini Marekani wanaodai kunyanyaswa na polisi.
Share:

Nyuki avuruga safari ya ndege Uingereza


Abiria wa ndege moja ya shirika la ndege la Flybe linalohudumu nchini Uingereza walicheleweshwa kwa zaidi ya saa mbili baada ya wahandisi wa ndege hiyo kubaini kuwa nyuki alikuwa amepenyeza na kuingia ndani ya mitambo ya ndege hiyo na hivyo safari haingewezekana.
Ndege hiyo ya Flybe yenye namba ya usajili BE384 ilikuwa ikitoka Southampton kuelekea Dublin.
Wahandisi walilazimika kutafuta mbinu ya kumwdoa mdudu huyo.
Abiria mmoja aliyekuwa ndani ya ndege hiyo Noel Rooney, anasema hakuamini tukio hilo hasa kwani ndge hiyo imeitwa jina la nyuki!
Taarifa kutoka kwa shirika hilo lilisema kuwa nyuki huyo alikuwa ndani ya mitambo muhimu ambayo ingehatarisha maisha ya abiria wake.
''rubani wetu alitahadharishwa na kuwepo kwa nyuki na akalazimika kurejea maramoja katika uwanja wa ndege wa Southampton'.'

Nyuki huyo alikuwa ndani ya mitambo muhimu ambayo ingehatarisha maisha ya abiria wake.

Shirika hilo limewaomba radhi abiria wote waliokerwa na hatua ya kurejea kwa ndege hiyo.
Watu wengi waliitania ndege hiyo kufuatia ripoti hiyo kuenea kwenye mitandao ya kijamii.
Rooney aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kuwa ''nimebeba jaa ilikuhakikisha kuwa safari yangu ikamilike''
Share:

Burundi;Watoto Wakimbizi wanadhulumiwa


Shirika la kutoa misaada la Save the Children limesema kuwa zaidi ya watoto elfu mbili mia tatu 2,300 ambao hawana wazazi, wamekimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi.
Shirika hilo limesema kuwa baadhi ya watoto hao walitembea kwa miguu kwa muda wa wiki moja hadi mataifa jirani ya Rwanda, Tanzania na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msemaji wa shirika hilo la Save the Children, Edwin Kuria,amesema idadi kubwa ya watoto hao walifika katika kambi za wakimbizi wakiwa hawana hata viatu na mali waliyokuwa nao ni mavazi tu waliokuwa nayo mwilini.

Tangu aprili mwaka huu watoto wengi kutoka Burundi wamekuwa wakitembea hadi kambi hizo za muda nchini Rwanda,Tanzania Uganda na DRC.
Shirika hilo limeonya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka huku wengi wakitoroka Burundi wakihofia kuzuka kwa mapigano.
Taifa hilo linajianda kwa uchaguzi mkuu ambao awali ulipangiwa kuandaliwa mwezi huu.
Aidha shirika hilo limesema watoto hao wanakabiliwa na matatizo mengi njiani na wanapofika katika kambi hizo ambazo kwa sasa zimefurika usalama wao bado sio shwari.
Baadhi ya watoto hao wameripotiwa kunyanyaswa na kudhulumiwa na wakaazi wa maeneo hayo.

Watoto hao hawaendi shuleni na sasa jukumu lao kuu ni kukusanya kuni au kuchimba vyoo majukumu ambayo sio salama kwa watoto amesema bwana Kuria.
Katika kambi ya Mahama nchini Rwanda watoto hao wanakabiliwa na matatizo ya kupata maakazi ya kuishi na pia maji safi ya kutumia.
Nchini Tanzania katika kambi ya Nyarugusa, idadi ya watoto wanaogonjeka imeongezeka hasa kufuatia kufungwa kwa vituo viwili ya muda kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Share:

Blog Owner

Blog Owner
FESTO MDEMU

Blog Archive

Flag


Total Pageviews

Translate

Powered by Blogger.