Menu - Pages

Wednesday, 28 January 2015

Gumzo:Michelle hakujitanda kichwa Saudia.


Mkewe Rais wa Marekani Barack Obama, Michelle Obama alipowasili nchini Saudi Arabia na mumewe bila ya kujitanda kichwa chake kwa kitambaa, wengi walitarajia kwamba mitandao ya kijamii nchini humo ingewaka moto kwa mingon'ono.
Lakini mambo yalikuwa tofauti maana kimya kilikuwa kikuu.
Ingawa vyombo kadhaa vya habari Ulaya, viliripoti kuhusu utata mkubwa kutokea kwenye mitandao ya kijamii, alama ya njia ya reli kwenye mtandao wa Twitter kwa lugha ya kiarabu...ikimaanisha ....''Michelle Obama bila mtandio''...ujumbe huo ilisambazwa kwenye mtandao huo zaidi ya mara 2,5000.
Hii sio idadi kubwa ya watu waliousambaza ujumbe huo lakini pia sio ndogo sana katika nchi yenye watumiaji wengi wa Twitter.
Pia inaarifiwa ujumbe huo ulizidiwa nguvu na ujumbe mwingine uliotumbwa kwenye Twitter dhidi ya ziara ya Rais Obama nkatika ufalme huo.
''Mfalme Salman amwacha Obama na kwenda kuomba,'' huu ndio ulikuwa ujumbe mwingine uliosambazwa sana kwenye Twitter kuhusu ziara ya Obama nchini humo.
Ujumbe huo: "Mfalme Salman amwacha Obama na kwenda kuomba,'' uliwavutia zaidi ya watu 170,000.

Wananchi katika ufalma huo walisambaza ujumbe huo kama njia yao ya kuonyesha wlaivyofurahishwa na mfalme mpya, Salman kumwacha Obama na kwenda kusali,kama ilivyoonekana kwenye video iliyowekwa kwenye Youtube.
''Huyu ndiye mwanamume aliyemwacha kiongozi wa nchi muhimu zaidi duniani akimsubiri wakati akienda kusali'', aliandika mtu mmoja kwenye mtandao wa Twitter.
Kitengo cha BBC cha Monitoring, ambacho kilikuwa kinafuatilia gumzo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ziara ya Obama nchini Saudia kilisema wengi walikuwa wanafanya tu utani kuhusu ufalme wa Ufalme wa Saudia ambao una sheria kali kuhusu mambo mengi tu.
Baadhi walikuwa wanatumiana picha ya Michelle akiwa amevalia kitambaa kichwani wakati wa ziara yake nchini Malaysia mwaka 2010 wakati wengine wakitoa wito kwa ufalme huo kuwaoa haki zaidi watu wake.
Ni watu wachache sana walionyesha kukerwa na hatua ya Michelle kutovalia kitambaa kichwani kama heshima tu kwa ufalme huo huku wengi kwenye Twitter wakikosoa ufalme huo kwa kile wanachosema ni kuwanyima uhuru wananchi.

'Ajioa' baada ya kukosa mchumba.


Yasmin Eleby hakupata mchumba wa kumuoa mtu ambaye alitaka awe mume wake atakapofikisha miaka 40--kwa hivyo akafanya kitendo ambacho kimewashangaza wengi, aliamua kujioa mwenyewe.
Kwa mujibu wa mtandao wa MySanAntonio.com,Eleby aliahidi kwamba ikiwa hatapata mchumba wakati atakapokuwa ametimiza miaka 40, basi atafanya harusi ya mtu mmoja yaani atajioa ili kusherehekea miaka yake 40.
Duru zinasema kuwa mwanamke Eleby alifanya harusi yake mwenyewe katika makavazi ya Houston akiambatana na jamaa na familia yake na wageni wengine waalikwa.
Kwa sherehe hii, dadake Eleby ndiye aliendesha sherehe hio, kwani ni kinyume na sheria kwa mtu kujioa mwenyewe. Harusi ya kawaida ni kati ya watu wawili.
Katika picha za kanisani sherehe ilionekana kuwa ya kawaida bila ya mchumba.
Kulingana na John Guess Jr afisaa mkuu wa makavazi hayo, sherehe hiyo ilionekana kuwa bila tashwishi na kuonekana kama jambo la kawaida kwani makavazi hayo huwakumbatia watu wa jinsia mbali mbali kuendesha harusi zao hapo.
Aliposikia kwamba Eleby, ambaye anaishi na kufanya kazi ugenini alikuwa anapanga kujioa mwenyewe, aliharakisha kwenda katika eneo hilo kujionea mwenyewe.
"Eleby alipofikisha umri wa miaka 40 bila ya kupata mpenzi na mtu mwenye nia ya kumuoa, aliamua angejioa mwenyewe,''alisema Guess Jr ambaye anasema harusi hiyo imewashangaza wengi na kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii.
Anasema anakubaliana na Eleby na mtazamo wake wa mapenzi kwamba mtu anaweza kujipenda na kujioa kwa kukosa wa kumuoa kwani cha muhimu ni mtu kujipenda kwanza kabla ya kupendwa.
"watu wengu huolewa bila ya kutafakari mara mbili kuhusu yule anayemuoa, '' Guess Jr alisema.
Anadhani kwamba pindi watu watakapomuona Eleby anavyojishughulikia mwenyewe, huenda akapata ushindani.
"ni mrembo, anafanya kazi kwa bidii na anasifika duniani na pia anaona uamuzi wake umewapa gumzo watu wengi. ''

Msikiti mkubwa Afrika wajengwa Algeria.


Msikiti utakaoshindana na maeneo mengine ya Kiislam ya kuabudia makubwa kuliko yote duniani unajengwa katika pwani ya kaskazini mwa Algeria.
Nini malengo ya kujenga msikiti mkubwa kama huu?
Nusu ya eneo katika ghuba ya Algiers, jengo kubwa taratibu limeanza kuibuka kutoka ardhini.
Katika sehemu moja kitakuwa chumba cha kuabudia cha Msikiti Mkuu wa Algiers. Katika sehemu nyingine kutakuwa na mnara mrefu kuliko yote duniani, ukiwa na urefu wa mita 265 kwenda juu.
Kutakuwa na shule ya korani, maktaba na jumba la makumbusho, na maeneo na bustani zenye miti ya matunda mbalimbali.

Wageni watawasili katika magari, matreni na hata maboti. Jengo hilo, litakalokuwa na uwezo wa kuchukua watu 120,000 people, litaunganishwa na bandari katika bahari ya Mediterani katika njia mbili za mandhari ya kutembea.
Msikiti huu utakuwa wa tatu kwa ukubwa wa eneo duniani, kwa mujibu wa wataalam wa majengo na kuwa msikiti mkubwa kuliko yote barani Afrika.
"Ni moja ya miradi ya karne," amesema Ouarda Youcef Khodja, afisa mwandamizi katika wizara ya nyumba na mipango miji, wakati alipotembelea eneo hilo la ujenzi.
Bi Ouarda amesema Rais Abdelaziz Bouteflika alitaka msikiti huo kuwa"Mnara wa Uislam na kwa mashujaa wa mapinduzi ya Algeria" - vita vya kupigania uhuru kutoka Ufaransa.
Lakini pia unaamanisha kuwa ishara kwa siku za baadaye. "Mnara huu utakuwa kitu cha kurejelea katika mapinduzi ya sasa-mapinduzi ya maendeleo ya Algeria."
Kama ilivyo kwa miradi mingine mikubwa, inayofadhiliwa kutokana fedha inayotokana na mafuta, ujenzi wa msikiti huu unategemea wataalam na wafanyakazi kutoka nje. Umebuniwa michoro na wataalam wa majengo wa Ujerumani na unajengwa na kampuni ya ujenzi ya China iitwayo China State Construction Engineering Corporation, ambayo ina mamia ya wafanyakazi wanaoishi katika eneo la ujenzi.

Na kama ilivyo kwa miradi mingine, mradi huu umechelewa kutekelezwa. Wizara ya nyumba na mipango miji hivi karibuni ilichukua jukumu la kusimamia ujenzi wa msikiti huo kutoka wizara ya masuala ya dini. "Mungu akipenda", anasema Bi Youcef Khodja, kwa sasa utakamilika mwishoni mwa mwaka 2016, japo hata hiyo tarehe, ujenzi utakuwa umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja kutoka muda uliokuwa umepangwa.
Vipimo vya msikiti huo, na eneo lake na gharama yake inakadiriwa kuwa dola za Kimarekani bilioni 1-1.5, ikionyesha kuwa ni kipaumbele cha serikali.
Sababu moja ya kutekelezwa kwa mradi huu ni uungwaji mkono na Bwana Bouteflika ambao utakuwa ukumbusho wa urais wake nchini Algeria.
Sababu nyingine inaweza kuonekana kwa ushindani wa mara kwa mara na majirani zake, Morocco. Msikiti wa Algiers utaupita kidogo msikiti wa Hassan wa Pili ulioko Casablanca kwa ukubwa wa eneo na kwa urefu wa mnara.
Lakini msukumo mkubwa huenda ukawa jaribio la serikali kujenga utambulisho wa taifa kidini na kutangaza Uislam kwa kuweka udhibiti juu ya misikiti na maimam wanaosalisha humo.
Jitihada hiyo iliyoanza pamoja na harakati za uhuru mwaka 1962 na kupata dharura na mgogoro wa kiraia na wapinzani wa Kiislam katika miaka ya 1990, wakati huo serikali ilipoteza udhibiti wa baadhi ya misikiti kwa wahubiri waliochochea upinzani dhidi ya utawala wa serikali.

Ni kwa mantiki hiyo Algeria inajenga msikiti mkubwa wa kisasa, kitu ambacho kilikuwa kinakosekana mpaka sasa - anasema Kamel Chachoua, mtaalam wa Algeria wa masuala ya dini katika Taasisi ya Utafiti na Elimu katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislam mjini Marseille.
Uamuzi wa kujenga msikiti huu ulikuwa "ukimaanisha kuwadhibiti wapiganaji wa Kiislam. Ni wazo la kuunda Uislam wa kitaifa baada ya kitisho cha miaka ya 1990 na kuundolea Uislam taswira mbaya na kuufanya kuwa karibu zaidi na serikali na kupambana na misimamo mikali ya kidini."
Msikiti huu una maana ya kuwa ishara muhimu katika sehemu ya Algiers ambayo imeshuhudia vitendo vingi vya misimamo mikali ya kidini katika miaka ya 1990, amesema.
"ni njia ya kuficha misikiti midogo na kuidunisha. Ni namna ya kusema: 'Tunapenda Uislam, lakini Uislama wa kisasa'. "Unaweza kujenga miskiti midogo 1,000 lakini haionekani - haionyeshi kuwa serikali iko katika mchakato wa kuonyesha udhibiti wake juu ya Uislam na kwamba inajivunia Uislam."
Wazo la kuhamasisha utaifa wa dini ya Kiislam ambayo inaondokana na itikadi zenye misimamo mikali kutoka nchi za Ghuba au kwingineko linaonekana katika jitihada za serikali za kutangaza na kushirikisha Sufi zawaya, au sheria za kidini. Pia inajidhihirisha katika utaalam wa ujenzi wa msikiti mpya wa Afrika Kaskazini, wenye mnara mmoja wa muundo wa pembe nne.

Mnara utakwenda juu ya eneo la Mohammedia, na juu ya mabaki ya ukoloni uliopita nchini Algeria. Moja kwa moja nyuma ya eneo la ujenzi ni jengo kubwa lililotumika kukaliwa na wachungaji wa kimisionari kutoka Ufaransa waliojulikana kama "peres blancs, au white fathers". Chini kidogo ya barabara ni eneo la kiwanda cha zamani cha mvinyo.
Msikiti huo umebuniwa kuwa ishara ya utambulisho wa Algeria mpya, lakini utambulisho huo bado unapiganiwa.
Baadhi ya wakosoaji wanauona msikiti huo kuwa zaidi kuwa ishara ya maelewano baada ya mgogoro na wanasiasa waislam kuliko kuwa njia ya kupambana na wasilam wenye misimamo mikali.
"Kipaumbele ni kusema: 'Angalia tulivyo nchi ya Kiislam," anasema Amira Bouraoui, mfuasi wa vuguvugu la upinzani la Barakat. "Ni njia nyingine ya kuwanyamazisha wapinzani wa Kiislam na kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa."
Bi Bouraoui hivi karibuni alitishiwa katika mtadao wa kijamii wa Facebook baada ya kuuliza kama sauti ya vipaza sauti ingeweza kupunguzwa. Wananch iwa Algeria wasiofungamana na dini wanaona hili kama mfululizo wa mifano ya kufuatilia uislam na kukosekana kwa uvumilivu wa kidini.
Hata hivyo kwa kawaida, iwapo Wa-Algeria wanaonekana kuwa watazamaji zaidi, hiyo ni hali ya juu juu, anasema Nacer Djabi, mwana sociolojia katika chuo kikuu cha Algiers. "katika kiwango cha kijamii si fikirii kama wanadini hasa, anasema Djabi.
"Ni watu wasiotaka mabadiliko sana, mabadiliko wanayoonyesha ni ya juu juu. Unaweza kuona hilo katika mitaa ya Algiers - kuna wasichana wengi wenye hijab, lakini hizo haziwazuii kuwa na wapenzi wa kiume, kunywa bia.
"Wa- Algeria wengi, wafanyabiashara, wanakwenda Mecca, wanaswali mara tano kwa siku", anasema."Lakini hali halibadili tabia yao kama wananachi kama Waislam."
Kwa upande wao wakazi wa Mohammedia wanaonekana kutofurahishwa na ujenzi wa msikiti mkubwa katika maeneo yao, wakisema fedha hiyo ingetumika katika mambo mengine.
"Unatakiwa kuanza na elimu na afya, na baadaye unaweza kufikiria kuenzi dini," anasema Racim, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22.
"Katika mtazamo wa Kiislam, mahali pa kuswalia si muhimu sana - ni kile kilichoko moyoni."

Hezbollah lashambulia jeshi la Israel.


Kundi la wapiganaji wa Washia wa Lebanon walio chini ya vugu vugu la Hezbollah, linasema kuwa limetekeleza shambulio dhidi ya msafara wa wanajeshi wa Israeli katika mpaka wa mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake, Jeshi la Israeli linasema wanajeshi wake wanne wamejeruhiwa pale kombora lililorushwa kwa kifaru kupiga gari lake la kijeshi karibu na mpaka wa Lebanon.
Taarifa nyingine kutoka kwa Hezbollah zinasema kuwa zaidi ya waisraeli 15 yamkini wameuwawa au kujeruhiwa.
Kundi la Hezbollah linasema kuwa lilikuwa likijibu mashambulio ya angani yaliyofanywa na Israeli yaliyomuua jenerali mmoja wa Iran na wapiganaji kadhaa wa Hezbollah Nchini Syria siku kumi zilizopita.
Israel ilijibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora Kusini mwa Lebanon
Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alionya kwamba jeshi la Israel liko tayari kutumia nguvu dhidi ya mashambulizi yoyote kutoka kwa washambuliaji.

Amnesty yakosoa jeshi la Nigeria.


Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International, limelishutumu jeshi la Nigeria kwa kushindwa kuwalinda raia katika mji wa Baga uliopo kaskazini mashariki mwa Nigeria, licha ya kuwepo onyo kwamba wanamgambo wa Boko Haram wangelitekeleza shambulio.
Linanukuu duru ambayo haikutajwa jina aliyesema kwamba wanamgambo hao waliwaambia wakaazi miezi miwili awali kwamba walikuwa wanapanga shambulio.
Amnesty International linasema waanjeshi walitazama tu jinsi vikosi vya Boko Haram vilivyokuwa vikiongezeka. Inakadiriwa kwamba kati ya watu 150 hadi 2000 waliuawa katika shambulio hilo lililotokea mapema mwezi huu.
Shirika hilo linadai kwamba limeelezea wasiwasi wake mara kadhaa awali kwamba vikosi vya usalama haviwajibiki vya kutosha kuwalinda raia dhidi ya unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binaadamu unaotekelezwa na Boko Haram.
Tangu mwaka 2009, Boko Haram limekuwa likiwalenga raia na kufanya uvamizi, kuwateka raia na mashambulio ya mabomu, huku mashambulio yao yakiongezeka kwa idadi na ukubwa. Malefu ya watu wameuawa katika mashambulio hayo, mamia kutekwa na maelfu wengine wameachwa bila makaazi baada ya kulazimika kutoweka mapigano.

Profesa Lipumba afikishwa mahakamani.


Kikao cha Bunge la Tanzania leo kimevurugika kutokana na vurugu za baadhi ya wabunge waliokuwa wakibishana kuhusu suala la kiongozi wa chama cha upinzani cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kushambuliwa na polisi Jumanne kwa madai kuwa alihusika katika maandamano kinyume cha sheria.
Hoja iliamshwa na mbunge ambaye pia ni kiongozi wa upinzani aliyetaka suala hilo lijadiliwe kwa dharura. Hayo yametokea huku Profesa Lipumba akifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka ya jinai.
Chanzo ni pale aliposimama James Mbatia mbunge wa kuteuliwa kutaka suala la polisi kumshambulia na kumdhalilisha Profesa Ibrahim Lipumba, kiongozi wa chama cha CUF lijadiliwe kwa dharura bungeni humo.
Licha ya jitahada za Spika Makinda kueleza kuwa suala hilo litajadiliwa kesho, kwa kuwa serikali inahitaji muda wa kuwasilisha majibu, mambo yakavurugika.
Huku wabunge wakiwa wamesimama wima wakishinikiza hoja hiyo ijadiliwe, Spika Makinda aliendelea na msimamo wake wa kutaka hoja ijadiliwe Alhamisi baada ya serikali kuwasilisha majibu, hapo ndipo mkorogano ulipozidi na kuleta kutoelewana kati ya wabunge wa upinzani na Spika.
Spika Makinda alilazimika kuahirisha kikao hicho mpaka jioni baada ya hali kuwa ngumu, na hata jioni likaahirishwa tena mpaka kesho, Alhamisi.
Kiongozi huyo wa upinzani inadaiwa alifika eneo ambako maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne yalikuwa yamepigwa marufuku, ingawa uongozi wa chama cha CUF unadai Profesa Lipumba alikusudia kuwashawishi wafuasi wake watawanyike kutii amri ya polisi ndipo akashambuliwa.
Wakati huo huo Profesa Lipumba amefikishwa mahakamani mjini Dar Es Salaam ambako amesomewa mashtaka ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Hata hivyo kwa muda Profesa Lipumba alikimbizwa hospitalini baada ya afya yake kudhoofika, ikidaiwa ni sababu ya kupigwa na polisi, madai ambayo BBC haijaweza kuyathibitisha.
Hata hivyo alirejeshwa mahakamani baada ya kupata nafuu, na kesi yake imeahirishwa na itatajwa tena mahakamani tarehe 26 Februari 2015.
Ameachiwa kwa dhamana ya watu wawili kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mmoja.