Menu - Pages
▼
Friday, 6 March 2015
Chanjo ya Ebola kujaribiwa Guinea..
Shirika la afya duniani WHO pamoja na wadau wake, mwishoni mwa wiki hii wanatarajia kuanza majaribio ya ufanisi wa chanjo dhidi ya Ebola nchini Guinea.
Chanjo hiyo aina ya VSV-EBOV imetengenezwa na wakala wa afya ya umma nchini Canada ambapo imeelezwa chanjo nyingine ya pili itaanzishiwa majaribio kadri shehena ya kutosha itakapo patikana.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt.Margaret Chan amesema majaribio yatafanyika kwenye maeneo ya Basse Guinée ambayo ndio yameathirika zaidi na Ebola kwa sasa nchini Guinea na utoaji wake utaanzia kwa wagonjwa wapya na wale wote ambao wamekuwa karibu nao.
Lengo la jaribio la sasa ni kutathmini iwapo chanjo hiyo itawapatia kinga dhidi ya Ebola watu waliokuwa na makaribiano na mgonjwa na pili iwapo utoaji wa chanjo utajenga kinga kwa wale waliopatiwa na hivyo kuzuia maambukizi zaidi.
WHO imesema imejitahidi kwa dhati kuhamasisha nchi zilizoathirika na ugonjwa huo pamoja na wadau ili kuendeleza mbinu za kinga na iwapo chanjo hiyo itafaa itakuwa ni hatua ya kwanza ya kinga dhidi ya Ebola.
Wadau wanaoshirikiana na WHO kwenye majaribio hayo ya chanjo ni pamoja na wizara ya afya ya Guinea, madaktari wasio na mipaka, MSF na taasisi ya afya ya umma, Norway.
Mkanyagano watokea katika kivuko Kenya..
Ripoti zinasema kuwa mkanyagano umetokea katika kivukio cha Ferry katika eneo la Likoni huko Mombasa Kenya na kuwajeruhi watu kadhaa
Tukio hilo limejiri baada ya ferry tatu zinazoendesha oparesheni zake katika kivuko hicho kukabiliwa na matatizo ya kiufundi.
Kulingana na ripoti hizo Ferry zilizosalia zimeshindwa kuhudumia idadi kubwa ya watu wanaotumia kivuko hicho pamoja na ile ya magari.
Hatua hiyo imesababisha msongamano mkubwa wa watu katika kivuko hicho.
Dereva Mpalestina awagonga Waisraeli....
Polisi nchini Israeli wanasema kuwa dereva ambaye anaaminiwa kuwa Mpalestina amevurumisha gari katikati ya kundi la watu kwenye mtaa mmoja mjini Jerusalem.
Wanasema kuwa mwamamume huyo aliwajeruhi takriban wapita njia wanne na kisha akajaribu kumchoma kisu mtu mwingine kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na maafisa wa usalama.
Msemaji wa polisi amekitaja kitendo hicho kuwa shambulizi la kigaidi.
Kulishuhudiwa visa vingine kama hivyo mwaka uliopita vilivyoendeshwa na madereva wa Kipalestina ambapo watu watatu waliuwa.
Oxfam:Wanajeshi wa DRC ni wanyanyasaji...
Shirika la kutoa misaada la Uingereza Oxfam limesema kuwa dhuluma zinazoendeshwa na wanajeshi mashariki mwa jamhuri ya demokrasi ya Congo ni mbaya sawa na zile zinazoendeshwa na waasi.
Wanavijiji wamelalamikia kukamatwa bila sababu, kuporwa na kulazimishha kufanya kazi pamoja na kutozwa ushuru kwa lazima.
Wengine wanasema kuwa wamelazimishwa kulipa ili kuweza kupitia kwenye vizuizi haramu na kupigwa ikiwa watakataa.
Makubaliano na kundi la M23 ya mwaka 2003 yalinuia kuleta amani katika eneo hilo na makundi ya waasi likiwemo lile la FDLR yanaendelea na harakati zao.