Menu - Pages
▼
Sunday, 5 April 2015
Ndege za dharura kusambaza dawa Yemen..
Shirika la Kimataifa la Msalaba mwekundu limesema linamatumaini ya kupeleka ndege mbili za dharura katika mji mkuu wa Yemen Sanaa.
Shirika hilo la Msalaba mwekundu limesema limepewa ruhusa na Muungano wa jeshi linaloongozwa na Saud Arabia, kutua na ndege zilizobeba wafanyakazi na dawa zitakazosambwazwa nchini humo.
Jeshi hilo la Saudia linaongoza kampeni ya kupambana na waasi wa Houthi.
Kusini mwa Yemen waasi hao wa Houthis wameweza kuongeza nguvu katika mji wa Aden dhidi ya majeshi yaliyotiifu kwa rais wa nchi hiyo Abdrabbuh Mansour Hadi, licha ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na majeshi hayo ya muungano.
Tishio la ugaidi lakatiza ibada Mombasa..
Ibada katika kanisa moja la Kianglikana nchini Kenya ilikatizwa ghafla baada ya tishio la ugaidi siku ya Jumapili.
Waumini walihamishwa kutoka kanisani hilo baada ya gari moja kuingia ndani ya uwanja wa kanisa kimabavu.
Kenya iko katika hali ya tahadhari baada ya mauaji ya watu wasiopungua 150 kaskazini mwa taifa taifa hilo.
Ibada hiyo ya Pasaka iligeuka na kuwa mbio za mguu niponye baada ya waumini kuarifiwa kuhusu gari hilo lisilo na nia njema.
Askofu wa kanisa hilo, Julius Kalu, amesema aliarifiwa kuhusu gari ambalo liliingizwa ndani ya uwanja wa kanisa bila hilo idhini kabla ya kusimamishwa kwenye lango kuu la kanisa lenyewe.
Askofu Kalu amesema waliokuwa ndani ya gari hilo walitoroka
Polisi waliitwa, na baada ya kulikagua gari hilo walilivuta hadi makao makuu ya polisi.
Mkuu wa polisi eneo la Mombasa Robert Kitur amesema hawakupata kitu, lakini wamelizuia gari hilo kwa uchunguzi zaidi.
Papa Francis awapa pole wa Kenya.
Katika maadhimisho ya ibada ya sikukuu ya Pasaka, baada ya mateso,kifo na ufufuko wa Yesu Kristo,Baba Mtakatifu Francis amewaombea wanafunzi waliouawa nchini Kenya mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika utaratibu wake wa kawaida wa kutoa ujumbe katika sikukuu ya pasaka,akizungumza na umati wa waumini waliofurika katika viwanja vya Basilica ya Mtakatifu Peter mjini Vatican, Papa ametoa mwito wa kusitisha kile alichokiita matukio mengi ya mateso ya wakristo ulimwenguni.
Kiongozi huyo wa kiroho anayeongoza waumini wa madhehebu ya kikatoliki wapatao bilioni moja nukta mbili ,amelaani mgogoro unaondelea Mashariki ya kati na kwingineko, lakini ameweka imani yake katika mazungumzo yanayoendelea juu ya mkataba wa vinu vya nyukilia vya Irani ,wenye mwanga wa matumaini wa kufikiwa makubaliano na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.
Kabla ya kuanza hotuba yake,Papa alikwenda katika viwanja hivyo vya Basilica la Mtakatifu Petro kuwasalimia waumini waliokuwa wakimsubiri pamoja na kwamba kulikuwa na hali mbaya ya hewa.
Serikali ya Kenya yamtambua muuaji..
Serikali ya Kenya imemtambua mmoja ya wapiganaji waliohusika katika mauaji ya chuo kikuu cha Garissa kwamba ni mtoto wa afisa wa serikali.
Msemaji wa wizara ya ndani amesema kuwa Abdirahim Abdullahi ni miongoni mwa watu wanne walioshambulia chuo kikuu cha Garissa siku ya alhamisi na kuwaua watu 148.
Mtu huyo sasa ametambulika kama mwana wa kiume wa Chifu wa eneo la Kazkazini mashariki mwa kenya.
Alidaiwa kutoweka na ilihofiwa kwamba amesafiri nchini Somalia.
Wizara ya ndani inasema kuwa wapiganaji wote waliuawa siku ya alhamisi.
Washukiwa wengine watano wamakamatwa kufikia sasa kwa kuhusishwa na mauaji hayo ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kutekelezwa na kundi la wapiganaji wa Alshabaab.
Garissa:Redio 2 zafungwa Somalia.
Mamlaka nchini Somalia imevifunga vituo viwili vya redio nchini humo baada ya kutangaza habari za wapiganaji wa Al-shabaab kuhusu shambulio la chuo kikuu nchini Kenya.
Kituo cha redio cha Sky FM na kile cha Shebelle vilifungwa huku mtangazaji na mkurugenzi wakikamatwa.
Vikosi vya usalama nchini Somali vimekuwa vikiwakamata wanahabari ambao hufanya mahojiano na wapiganaji wa Al-shabaab ama kutangaza habari zao.