Menu - Pages

Thursday, 16 April 2015

Mapacha 5 wa kwanza kuzaliwa Marekani


Mapacha watano wa kike wamezaliwa Marekani katika hospitali moja ya wanawake mjini Texas Houston.
Wauguzi katika hospitali hiyo wanasema kuwa uzazi huo kutokana na mimba moja ni rekodi mpya ambayo haijawahi kutokea Marekani.
Danielle Busby ambaye ndiye mama wa watoto hao ambao wamepewa majina ya Olivia Marie, Ava Lane, Hazel Grace, Parker Kate na Riley Paige;anasema kupata watoto hao wote wakiwa wazima kwake ni baraka ya hali ya juu.

Inasemekana watoto wengi sawa na hao walihahi kuzaliwa mara moja huko London Uingereza ,mwaka 1969 katika hospitali ya Queen Charlotte.
Zaidi ya Madaktari na wauguzi 12 walilazimika kufanya kazi ya ziada ilikumsaidia bi Busby kujifungua watoto hao ambao hawakuwa wametimiza umri wa miezi tisa tumboni kwa njia ya upasuaji .
Baba wa mtoto huyo, Adam Busby amewamiminia sifa kedede wahudumu wote wa hospitali hiyo waliofanikisha operesheni hiyo.

Bwana Busby amesema kuwa mwanawao wa kwanza Blayke anawasubiri kwa hamu na ghamu.
Bi. Busby alikuwa na tatizo la kupata ujauzito hivyo akatumia mbegu pandikizi ya uzazi kwa mimba zake zote mbili.

Kumi wakamatwa Tanzania kwa ugaidi...


Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja anayesadikiwa kuhusiana na watu hao waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kumjeruhi kwa panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo limetokea jana (Aprili 14) majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.Kamanda Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo ambaye umri wake haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa kuwa wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua kufatilia nyendo zao.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata askari huyo eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye namba E.9245 Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa huyo, ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka.”
Alisema polisi walendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.

Kamanda huyo alitaja vitu vilivyokutwa katika mabegi yaliyokuwa ndani ya msikiti huo ni pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia, bisibisi, vinyago vya kuziba uso (masks), nguo za jeshi, misumeno ya chuma na spana.

Mahakama yazima vinu vya nyuklia Japan.


Mahakama moja nchini Japan imetoa agizo la kuzuia kufunguliwa upya kwa kiwanda kimoja cha nyuklia iliyoko pwani ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Vinu 50 vya nyuklia vya Japan vilifungwa mwaka wa 2011 kufuatia mkasa wa Fukushima.
Lakini serikali ya waziri mkuu Sinzo Abe, inashinikiza vinu hivyo kufunguliwa.
Agizo hilo lililotolewa katika mahakama ya wilaya wa Fukui, ni pigo kubwa kwa juhudi hizo za serikali.

Miezi miwili iliyopita mdhibiti wa nyuklia nchini humo alitoa idhini kwa mradi huo wa Takahama ulioko Kaskazini Magharibi mwa Japan kuanzisha upya uzalishaji wa kawi ya nyuklia katika viwanda vyake viwili.
Alisema kuwa mradi huo ulikuwa umetimiza masharti yote ya kiusalama na utaratibu yaliyowekwa punde baada ya mkasa wa Fukushima miaka minne iliyopita.
Lakini leo majaji katika mahakama ya Fukui wameonekana kutokubaliana na uamuzi wa mdhibiti huyo.
Badala yake wamekubaliana na kundi la wakazi wa eneo hilo waliotaka kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji kawi katika kiwanda hicho.
Walidai kuwa kiwanda hicho hakitaweza kuhimili tetemeko kubwa la ardhi kama lile lililosababisha mkasa wa Fukushima.
Kampuni ambayo inamiliki kiwanda hicho, Kansai Electric, tayari imesema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini huenda utaratibu huo ukachukua miezi kadhaa au hata miaka kabla ya uamuzi kutolewa upya.
Na huenda hatua kama hiyo ikachochea wakazi wanaoishi karibu na viwanda vingine vilivyofungwa wakawasilisha kesi kama hii mahakamani.

Akizungumza nje ya mahakama, wakili wa kundi la watu waliowasilisha kesi mahakamani Yuichi Kaido alisema ana matumaini kuwa uamuzi huu ndio mwanzo wa kusitishwa kwa uzalishaji wa kawi ya nyuklia nchini Japan.
''Tunahitaji kuambiwa ukweli wa mambo kuhusu mkasa wa Fukushima na tunahimiza kwamba viwanda vyote vinavyozalisha kawi ya nyuklia vifungwe sio tu kiwanda cha Takahama pekee yake,"alisema Kaido
Mwanaharakati anayepinga matumizi ya nguvu za nyuklia Tadashi Matsuda aliwashukuru waathirika wa mkasa huu kwa mchango wao katika kesi hiyo.
"Huu ni uamuzi uliofanyika, kutokana na msukumo wenu kama waathirika wa mkasa huu''.

''Kwa wale ambao baada wanateseka huko Fukushima, Natumai habari hii itawafikia na tafadhali sikiliza haya yote yamewezekana tu kwa ajili ya mchango wako"alisema Matsuda.
Uamuzi huu ni pigo kubwa kwa serikali ya Japan ambayo inalenga kufufua sekta yake ya nyuklia.
Hadi sasa viwanda 48 vya kuzalisha nyuklia nchini humo vimefungwa kufuatia mkasa huo wa mwaka 2011.
Hata hivyo waziri mkuu wa Japan Yoshihide Suga, amesema serikali bado inamatumaini ya kufufua tena viwanda hivyo.

Hariri:Mwandishi kizimbani ICC


Mwaandishi habari mmoja raia wa Lebanon leo atakuwa mshtakiwa wa kwanza kufikishwa kizimbani katika mahakama ya jinai ya ICC iliyoko The Hague nchini Uholanzi katika uchunguzi wa kuuawa kwa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri.
Bi Karma Khayat na runinga anayoifanyia kazi ya Al-Jadeed, yanashutumiwa kwa kupuuza ushauri wa kundi maalum la uchunguzi wa kesi hiyo nchini Lebanon, kwa kutoa taarifa kuwahusu mashahidi.
Amekanusha kutenda kosa lolote.

Bi Khayat amesema kuwa ripoti yake ilikuwa kwa manufaa ya uma.
Mahakama hiyo maalum ilibuniwa na umoja wa mataifa, ili kubaini watu waliohusika na mauaji ya bwana Hariri.
Watu watano wanaotuhumiwa kuhusika katika mauwaji hayo ya Hariri wangali mafichoni.

Ghasia za ubaguzi zapingwa Afrika Kusini


Maelfu ya raia katika mji wa mashariki wa Durban nchini Afrika Kusini wanaandamana kupinga ghasia za hivi majuzi dhidi ya wageni.
Takriban watu watano wameuawa tangu wiki iliopita katika ghasia dhidi ya wahamiaji ambao wameshtumiwa kwa kuchukua kazi za raia wa taifa hilo.
Hofu ya kusambaa kwa ghasia inaendelea kutanda.

Mjini Johannesburg ,wamiliki wa maduka kutoka mataifa ya Ethiopia,Somalia na mataifa mengine ya Afrika wamefunga biashara zao wakihofia kuporwa.
Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini ameshtumu ghasia hizo na anatarajiwa kulihutubia bunge baadaye.
Mnamo mwaka 2008 watu 62 waliuawa kufuatia ghasia za kibaguzi zilizokumba taifa hilo.

Al Shabaab inaendelea kuwasajili Wakenya


Huku ujenzi wa ua utakaotenganisha Kenya na Somalia ukianza kwa madhumuni ya kuwakomesha wanamgambo wa Al Shabaab kutoishambulia Kenya,
shirika la BBC limepata ushahidi kuwa kundi hilo lenye makao yake nchini Somalia linaendelea kuwasajili wanachama wapya katika miji mikuu ya Kenya.
Katika mji wa Isiolo ulioko Kaskazini Mashariki mwa Kenya, takriban vijana barubaru 26 wametoweka makwao.
BBC imebaini kuwa vijana hao wamewapigia wazazi wao simu wakiwaarifu kuwa tayari wamejiunga na wanamgambo wa Al Shabab.
Nusu ya wazazi wao wameripoti kutoweka kwao kwa vyombo vya usalama .

Asilimia kubwa ya wale waliokaa kimya wanahofia kudhalilishwa na maafisa wanaopambana na ugaidi nchini Kenya .
Ilikuwashawishi wakenya kujiunga na serikali kutambua wafuasi wa kundi hilo waliotangamana na jamii, serikali ya Kenya imetangaza
msamaha kwa wakenya waliojiunga na Al Shabaab maadamu watajisalimisha kwa vyombo vya dola katika kipindi cha siku 10 zilizotolewa.
Matukio haya yanawadia takriban majuma mawili tangu wapiganaji wa kundi hilo kuivamia chuo kikuu cha Garissa na kuwaua takriban wanafunzi wakristu 150.
Serikali ya Kenya baadaye ilitangaza kuwa kiongozi wa wapiganaji hao alikuwa ni Wakili mkenya.

Usajili huu unaoendelea unatizamwa na wachanganuzi wa maswala ya kiusalama kama mbinu mpya na ya kuhofiwa.
Ukweli ambao umewaogofya wabunge na maafisa wa usalama nchini humo.
Hata hivyo mmoja wa viongozi wa kiislamu wanaoheshimiwa nchini Kenya Sheikh Abdullahi Salat, ameonya kuwa hofu ya jamii dhidi ya polisi na shauku huenda ikahujumu jitihada hizo.

Mafuriko yasomba basi la abiria Mandera..


Maafisa wa shirika la msalaba mwekundu kaunti ya Mandera kazkazini mwa Kenya wanasema kuwa takriban watu 16 wametoweka baada ya basi kusombwa na mafuriko kilomita chache kutoka mji huo.
Mvua kubwa iliripotiwa kunyesha katika eneo la mji huo na viunga vyake mapema Alhamisi.
Katibu mkuu wa shirika la msalaba mwekundu Abbas Gulet anasema kuwa wamewaokoa watu 42 kufikia sasa.
Basi hilo liliondoka mjini Mandera likielekea jijini Nairobi mapema siku ya jumatatu kabla ya kukwama katika matope.
Baadaye mvua kubwa ilinyesha na mafuriko kulisomba basi hilo.
Maafisa wa msalaba mwekundu wanasema kuwa wameanza kuwasaka watu waliotoweka katika mto mmoja uliopo ambapo mafuriko hayo yanaelekea.