Menu - Pages
▼
Monday, 20 April 2015
Mama aliyeua Watoto Marekani ahukumiwa
Mwanamke mmoja katika Jimbo la Utah nchini Marekani ambaye alikiri kuua watoto wake wachanga sita wa kuzaa mwenyewe huenda akahukumiwa Kifungo cha maisha gerezani.
Megan Huntsman, 40, alikamatwa mwaka mmoja uliopita baada ya miili ya Watoto kukutwa kwenye maboksi katika gereji ya Nyumba yake ya zamani.
Mwezi Februari alikutwa na hatia kwa makosa sita ya mauaji.
Jaji wa mjini Provo alitoa hukumu dhidi ya mwanamke huyo ya takriban miaka 30 mpaka kifungo cha maisha.
Polisi wamesema Watoto hao walizaliwa kati ya mwaka 1996 na 2006 na kueleza hali ya Watoto hao kuwa mauti iliwakuta kwa kukosa hewa au kwa kukabwa na Huntsman mara tu baada ya kuzaliwa.
Polisi wamesema miili aliiweka kwenye mifuko ya plastiki na kuiweka kwenye maboksi.
Mwanamke huyo aliacha maboksi hayo katika Nyumba aliyoishi alipokuwa akihama, miili iligunduliwa na mumewe,Darren West, mwezi Aprili mwaka jana.Mtoto wa saba pia anaaminika alipoteza maisha wakati mwanamke huyo alipokuwa akijifungua.
Polisi wanasema Huntsman alikuwa akitumia dawa zenye nguvu ziitwazo methamphetamine, dawa zinazosisimua neva mwilini ili kuwezesha akili na mwili kufanya kazi kwa uchangamfu, pia mwanamama huyo hakuwataka Watoto hao.
Maafisa wanasema West ni Baba wa Watoto lakini yeye si mshukiwa wa tukio hilo.Yeye na Huntsman wana Watoto watatu.
Mwezi Aprili mwaka 2014 West aliachiwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka minane gerezani kwa makosa ya kujihusisha na uhalifu wa madawa, hivyo alikwenda kwenye nyumba kwa ajili ya kukusanya vitu vyake ndipo alipogundua miili ya Watoto.
Uamuzi wa mwisho kuhusu muda ataotumikia Huntsman gerezani uko mikononi mwa jopo la wanasheria.Waendesha mashtaka wamesema huenda akatumikia kifungo cha maisha.
Ulaya kumaliza vifo vya Wahamiaji?
Mkuu wa sera za kigeni ndani ya Umoja wa Ulaya amesema kuwa uharaka unahitajika katika kushughulikia majanga yanayojitokeza katika bahari ya Mediterania.
Federica Mogherini ameainisha mambo tisa ya mpango wa kumaliza tatizo la vifo vya wahamiaji.
Operesheni ya uokoaji itaimarishwa na kutakuwa na Kampeni maalumu ya kuteketeza boti zilizotumiwa kusafirisha watu.
Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, amesema Roma ina mpango wa kupambana na wale waliowaita Wafanyabiashara wa utumwa.
Imeelezwa kuwa hatua zitachukuliwa kupunguza idadi ya wahamiaji na kuwarejesha wale wanaoingia barani Ulaya.
Mpango huu utajadiliwa na Viongozi wa Ulaya siku ya Alhamisi.
Wakati hayo yakijiri,Polisi nchini Italia inawashikilia watu wawili miongoni mwa walionusurika kwenye ajali ya boti.
Mtu mmoja mwenye asili ya Tunisia ambaye anaaminika kuwa nahodha wa chombo hicho na mwenzake Raia wa Syria walikamatwa wakishukiwa kuhusika na vitendo vya kusafirisha watu kinyume cha sheria.
Watu hao walikamatwa baada ya meli moja yenye manusura wa ajali kuwasili katika bandari ya Catania katika kisiwa cha Sicily.
Zwelithini alaani mashambulio AK.
Mfalme wa kabila la Zulu, Goodwill Zwelithini, ameelezea kama jambo la aibu mashambulio dhidi ya raia wa mataifa mengine yanayofanyika nchini Afrika Kusini, ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu saba.
Mwaandishi habari wa BBC mjini Durban mahala ambapo mfalme huyo alitoa matamshi hayo anasema kuwa hata ingawa anakanusha kuwa amenukuliwa visivyo, matamshi yake dhidi ya raia wa kigeni imesababisha athari mbaya.
Amesema kuwa umma uliwapigia kelele mabalozi wanaoziwakilisha mataifa yaliyoathirika zikiwezo Msumbiji na Zimbabwe.
Polisi nchini humo wameakamata washukiwa kadhaa miongoni mwao wanaume watatu ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya rais mmoja wa Mozambique katika eneo la Alexandra viungani mwa mji mkuu wa Johannesburg.
Picha kadhaa zimeonyesha Emmanuel Sithole akindungwa kisu huku umati mkubwa ukitizama.
Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, amesema mashambulio hayo yanakwenda kinyume na maadili yote wanayoamini.
Makundi kadhaa yaliyojihami yameshambulia na kupora maduka kadhaa yanayomilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa mengine ya Afrika.
Huku idadi ya watu wasio na kazi nchini humo, ikikadiriwa kuwa zaidi ya asilimia Ishirini na nne, raia wengi wa taifa hilo wamewashutumu raia wa kigeni kwa kuchukua nafasi zao za kazi.
Maelfu ya raia hao wa kigeni, wamekimbia makwao na sasa wanaishi katika kambi za muda, ili hali mataifa jirani wameanza shughuli ya kuwahamisha raia wao.
Siku ya Jumapili, serikali ya Zimbabwe imetuma mabasi kadhaa mjini Durban kwenda kuwachukua raia wake wapatao mia nne.
Takwimu rasmi za serikali zinakadiria kuwa kuna raia milioni mbili wa kigeni wanaoishi nchini Afrika Kusini, lakini wengi wanahoji kuwa idadi hiyo huenda ni kubwa zaidi.
Huenda 800 waliangamia baharini
Umoja wa Mataifa unasema unahofia kuwa huenda watu 800 walifariki siku ya Jumapili, pale mashua waliyokuwa wakilitumia kuvuka bahari ya Mediterenean ilipozama karibu na Libya.
Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR, limekuwa likizungumza na manusura baada ya kuwasili katika kisiwa cha Sicily mapema leo Jumanne.
Mkuu wa sera kwenye Muungano wa Ulaya Federica Mogherini anasema kuwa pana haja ya kuwepo hatua za haraka ili kushughulikia suala kuhusu wahamiaji katika bahari ya Mediterranean, huku akizindua mikakati kumi ya mpango wa kutanzua vifo vya wahamiaji.
Mogherini, anasema kuwa mipango hiyo ni hatua kubwa ya kuzuia kupotea kwa maisha ya watu. Majukumu ya muungano huo ni kuzidisha operesheni ya uokozi, pamoja na mipango mipya ya kuharibu mashua zinazotumiwa na walanguzi wa binadamu wanaowavusha watu baharini.