Menu - Pages
▼
Tuesday, 21 April 2015
Japan yavunja rekodi treni mwendo kasi
Treni ya kampuni ya Central Japan Railway (JR) ikirejea katika stesheni baada ya kuandika rekodi mpya ya dunia ya mwendo kasi
Treni ya Japan iendayo kasi imevunja rekodi yake duniani kwa kufikia mwendo wa kilomita 603 kwa saa, sawa na maili 374 kwa saa katika majaribio yake karibu na Mlima Fuji.
Treni hiyo imevunja rekodi yake ya mwendo wa kilomita 590 kwa saa iliyoweka wiki iliyopita katika jaribio lingine.
Treni ya maglev ambayo haitegemei kugusana na chuma bali inaendeshwa kwa nguvu ya umeme, inatumia sumaku zilizochajiwa kwa umeme kunyanyua na kuvuta mabehewa juu ya njia ya reli.
Treni ya Kati ya Japan, JR Central, ambayo inamiliki matreni hayo, inataka kuanzisha huduma yake kati ya Tokyo na mji wa Nagoya uliopo katikati ya Japan, ifikapo mwaka 2027.
Safari hiyo ya kilomita 280 itachukua dakika itachukua muda wa dakika 40 tu, pungufu ya nusu ya muda unaotumiwa sasa.
Hata hivyo abiria hawatashuhudia treni hiyo kukimbia mwendo wake uliovunja rekodi kwa sababu kampuni inasema treni zake zitakimbia kasi ya kilomita 505 kwa saa. Kwa kulinganisha treni za mwendo kasi kabisa za Japan aina ya shinkansen, au "bullet train" inakimbia mwendo kasi wa kilomita 320 kwa saa.
Treni ya Maglev ikiwa katika majaribio
Majaribio ya treni hiyo yalifanyika katika reli ya majaribio katika mkoa wa Yamanashi ulioko katikati mwa Japan.
Ujenzi wake unakadiriwa kugharimu karibu dola za kimartekani bilioni 100 au pauni za Uingereza bilioni 67 kwa ujenzi tu wa kwenda Nagoya, ambapo asilimia 80% ya gharama itakwenda katika ujenzi wa mahandaki ya kupitia treni hiyo.
Ifikapo mwaka 2045, treni hizo za mwendo kasi za maglev zinatarajiwa kusafiri kati ya miji ya Tokyo na Osaka kwa muda wa saa moja tu na kupunguza urefu wa safari kwa nusu ya muda uliokuwa ukitumika yaani saa mbili.
Watu wapatao 200 walijipanga kando ya reli kushuhudia majaribio ya treni hiyo yaliyofanyika Jumanne.
"Jinsi treni inavyokwenda kwa mwendo kazi zaidi, ndivyo inavyozidi kutulia- nafikiri ubora wa treni umeimarika," amesema mkuu wa utafiti wa treni ya JR Central, Yasukazu Endo.
Treni hiyo inatumia sumaku iliyochajiwa kwa umeme kunyanyua na kuvuta mabehewa juu ya njia ya reli.
Ethiopia yaanza siku 3 za maombolezi.
Islamic State wakienda kuwaua raia wa Ethiopia
Ethiopia imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kwa heshima za raia wake waliouawa na wanamgambo wa kundi la Islamic State nchini Libya.
Bendera zitapepea nusu mlingoti wakati nalo bunge la nchi hiyo likikutana kujadili hatua ambazo litachukua kufuatia mauaji hayo ya raia wake zaidi ya ishirini.
Msemaji wa serikali Redwan Hussein, alisema kuwa waathiriwa hao wanaaminika kuwa wahamiaji waliojaribu kusafiri kwenda barani ulaya.
Mungano wa Afrika ambao una makao yake makuu nchini Ethiopia ulilaani mauaji hayo na kusema kuwa utafanya mikakati ya kuhakikisha kuwepo usalama nchini Libya.
Wanamgambo wa Islamic State walitoa kanda ya video ambayo inakisiwa kuonyesha mauaji hayo yanayoonyesha watu hao wakipigwa risasi na kukatwa vichwa.
Mkenya ashinda tuzo la Goldman
Phyllis Omido mshindi wa tuzo la Goldman
Phyllis Omido, kutoka Kenya, alikuwa miongoni mwa washindi sita waliokabidhiwa tuzo hilo huko San Francisco, Marekani, Jumatatu usiku. Omindo alipata tuzo hilo kwa kutetea wakaazi wa mtaa wa mabanda wa Owino Ohuru ulioko Mikindani kaunti ya Changamwe mjini Mombasa.
Wakaazi hao wameathirika na sumu aina ya ''lead'' kutokana na kiwanda cha kukarabati betri kuu kuu kilichojengwa karibu na mtaa huo wa mabanda. Ukarabati wa betri kuu ulisababisha umwagikaji wa madini ya sumu aina ya "lead" na kuwadhuru kiafya wakaazi hao kiasi kwamba baadhi ya wanaume sasa wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya nyumbani.
Kiwanda hicho kilianza kazi mwaka wa 2009 lakini Omido alitetea wakaazi hao wa Uwino Uhuru kwa kufanya maandamano ya mara kwa mara hadi kikafungwa miaka mitatu baadae.
Omido apongezwa kwa ushindi wake
Anastacia Nambu anatueleza jinsi mumeo ameumia:''Sasa sisi tunaishi tu kama dada na ndugu kwa sababu mzee sasa hawezi kazi na si kupenda kwake ni kwa sababu ya hicho kibanda. Sisi tuliakua tunaishi karibi sana na hicho kibanda ndio kwa maana huo moshi ukaumiza mzee wangu. Ni jambo ka kusikitisha sana maanake tulitaka tupate watoto wengine lakini sasa hatuwezi. Tuna watoto wanne.''
Mzee wa kijiji Alfred Ogolla anatueleza juhudi zao za kuhimiza serikali ya Kenya iwape matibabu zimegonga mwamba. Ogolla anatueleza zaidi:''Sote hapa wazee, kina mama na watoto tunaumia sana. Mimi ninakohoa kila mara, wasichana hawawezi kuzaa kwa sababu huo moshi uliharibu nyumba zao za uzazi na watoto nao wengine miguu imejipinda na wengine nao ni vibofu hawawezi kuona. Pesa ya matibabu ni nyingi sana hatuwezi kupata dawa kila siku.''
Tuzo hilo la Omido limeandamana na kitita cha dola 175,000.
Omido afurahia tuzo lake
Je, Omido atatumiaje fedha hizo ambazo ni kama shillingi milioni 17 za Kenya?:''Kiasi kikubwa cha pesa hizi nitatumia kwa wakili maanake kesi ya wakaazi wa Owino Uhuru ingali kotini. Tunataka serikali iwape fidia na kuwalipia matibabu. Fedha zingine nitazitumia kuendeleza shirika langu lisilo la kiserikali (Centre for Justice, Governance and Environmental Action) maanake kuna mengi nataka kufanya licha ya vitisho kwa maisha yangu kwa sababu ya kupigania wakaazi wa Owino Uhuru.
''Kwa kweli nimefurahia sana kupata tuzo hili ambalo linanipa morali zaidi kwa kuwa kazi yangu imetambuliwa kote duniani. Nataka kufuata nyayo za mwanaharakati mwingine wa mazingira, merehemu Wangari Maathai. Nitazidi kutetea wanyonge kwa sababu ni wengi sana wanaumia.''
Uharamia wapungua duniani
Maharamia
Halmashauri ya kimataiafa ya safari za baharini IBM imetoa ripoti yake ya hivi punde kuhusu uharamia.
Halmashauri hiyo inasema kuwa uharamia sasa unaripotiwa kusini mashariki mwa bara Asia, huku meli ndogo za kusafirisha mafuta zikishambuliwa baada ya kila wiki mbili.
Maeneo yaliyoathirika na uharamia
Kwenye ripoti yake ya kila baada ya miezi mitatu, IMB inasema kuwa licha ya kupungua kwa mashambulizi kote duniani miaka ya hivi majuzi, visa vya uharamia viliongezeka katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2015.
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mara ya kwanza hakuna visa vyovyote vya uharamia vilivyorekodiwa pwani ya Somalia na Ghuba ya Aden.
Inasema kuwa uharamia ulianza kushuhudiwa mwaka 2007 eneo hilo lakini ukapungua kuanzia mwaka 2011 wakati doria za meli za kijeshi zilipo ongezeka.
Ripoti hiyo pia imetaja visa kadha vya uharamia pwani ya magharibi mwa Afrika. Inasema kuwa mwaname moja aliuawa wakati wa kutekwa kwa mashua ya uvuvi pwani ya Ghana.
Mawaziri 16 waapishwa Afghanistan
Baada ya miezi kadha ya mizozo ya kisiasa, rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amewaapisha mawaziri 16 wapya kwenye sherehe zilizofanyika mjini Kabul.
Hii inamaanisha kuwa baraza la mawaziri sasa limekamilika. Nafasi ya waziri wa ulinzi imesalia wazi kufuatia kutoelewana kwa serikali ya umoja.
Wale wote walioteuliwa hawajashikilia nyadhifa kama hizo na wengi ni vijana na waliosoma. Wanne kati ya mawaziri hao ni wanawake.
Kinyume na ilivyo kuwa awali, rais Ghani ameahidi kuwateua watu walio na ujuzi badala ya mibabe wa kivita na wapiganaji kuongoza serikali.
Morsi ahukumiwa miaka 20 gerezani
Makahama nchini Misri imemhukumu aliyekuwa rais wa zamani Mohammed Morsi kifungo cha miaka 20 jela kutokana na kuuawa kwa waamdamanaji wakati akiwa madarakani.
Hii nidyo hukumu ya kwanza kutolewa kwa Morsi tangu aondolewe madarakani, na moja ya hukumu zinazomuandama.
Morsi aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2013 kufuatia maandamano makubwa mitaani ya kupinga uongozi wake.
Wafuasi wa Morsi
Yeye pamoja na viongozi wengine wa Muslim Brotherhood walilaumiwa kwa kuwachochea wafuasi wao kumuua mwandishi wa habari na waandamanaji wa upinzani wakati wa makabiliano nje ya ikulu ya rais mwishoni mwa mwaka 2012.
Wakati umati ulipokusanyika nje ya ikulu bwana Morsi aliwaamrisha polisi kuwatawanya lakini wakakataa kufanya hivyo.
Baadaye Muslim Brotherhood waliwaleta wafuasi wao ambapo watu 11 waliuawa kwenye makabiliano, wengi kutoka kwa Muslim Brotherhood.
Kabla ya kutolewa hukumu ya leo, Muslim Brotherhood walimlaumu rais wa sasa Abdul Fatta al-Sisi kwa kutumia mahakama kama silaha.
Jeshi kutuliza ghasia Afrika kusini
Waziri wa ulinzi nchini Afrika kusini ametangaza kuwa jeshi litatumwa wakati ghasia dhidi ya wageni zikiwa zimesababisha vifo vya watu Saba.
Nasiviwe Mapisa-Ngqakula anasema kuwa ombi la kutumwa kwa wanajeshi liliamuliwa baada ya polisi kuomba msaada.
Lakini hakusema ni wanajeshi wangapi watatumwa mitaani. Jeshi litatumwa kwenda maeneo yanayoshuhudia ghasia nyingi ikiwemo mikoa ya Kwa Zulu Natal na Guateng.
Wakati wa ghasia kama hizo mwaka 2008 jumla ya watu 63 waliuawa. Serilali ya Afrika Kusini pia imetangaza kuwa zaidi ya watu 900 wamerudi kwa hiari kwenda nchi zao.