Menu - Pages

Monday, 27 April 2015

Yanga mabingwa wapya 2014/2015 Tanzania


Kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mwaka 2014/2015

Timu ya Yanga wamekuwa mabingwa wapya wa ligi kuu ya Tanzania kwa mwaka 2014/2015 na hivyo kuivua rasmi ubingwa Azam iliyokuwa ikishikilia taji hilo.
Ubingwa wa Yanga unakuja baada ya kuizamisha timu ya Polisi Morogoro kwa jumla ya mabao 4-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jumatatu, jijini Dar es Salaam, ilikuwa inahitaji ushindi wa pointi tatu kutangazwa bingwa mpya ikibakiwa na michezo miwili mbele.
Kabla ya mchezo huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa pointi 52 ambapo sasa imefikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ya ligi hiyo ya Vodacom.


Azam ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 kwa sasa, endapo itashinda michezo yake iliyobaki itafikisha pointi 54 tu.
Vita ya kusaka nafasi ya pili sasa imebaki kwa Azam na Simba iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 41.
Timu za Prisons, Polisi na Ndanda ziko hatarini kushuka daraja.
Timu 14 zinashiriki ligi kuu ya Vodacom nchini
Tanzania.
Kocha wa Yanga Hans Pluijm

Babaake Kim Kardashian sasa ni mwanamke


Bruce Jenner aliyekuwa mwariadha bora duaniani kabla ya kuwa nyota wa kipindi cha televisheni na familia moja maarufu duniani ''The Kardashians''. sasa amefichua siri ambayo amekuwa akiificha kwa miaka mingi.
''Kwa nia na madhumuni yote, mimi ni mwanamke.'' Jenner aliambia Sawyer kutoka ABC katika mahojiano maalum yaliopeperushwa hewani siku ya Ijumaa.
''Watu wananiona tofauti,wananiona kama mwanaume, lakini moyo na roho yangu na kila kitu ninachofanya maishani ni sehemu yangu.'' Jenner ambaye ana umri wa miaka 65 amesema. '' Upande huu wa kike ni sehemu yangu.
hivi ndivyo mimi nilivyo.''

Katika masaa ya mahojiano na Diane Sawyer mjini New York na California, Jenner alielezea kwa kina mapambano yake ya kuwa na jinsia mbili tangu utotoni.
''Akili zangu ni za kike sana kuliko za kiume.'' Ameongezea. '' Ni vigumu sana watu kuelewa, lakini hivyo ndivyo nafsi yangu ilivyo.''
Jenner aliyejawa na hisia na mwenye nywele ndefu shati na suruali ndefu alisema kuwa amesubiri kwa miaka mingi ili kujitangaza kwa kuwa hakutaka kuwavunja moyo watu.
Kwa miongo kadhaa wake wa zamani wa Jenner na madada zake waliweka siri kuhusu jinsia yake na kwamba walikuwa watu waliokuwa wakijua siri hiyo.
Mtandao wa watu wanaojua siri hiyo hatahivyo ulipanuka hivi majuzi wakati Jenner alipomwambia mamaake na wanawe 10 .
Jenner ana watoto sita Burt,Cassandra,Brabdon,Brody,Kendall na Kylie pamoja na watoto wanne wa kambo akiwemo Kourtney,Kim,Khloe na Rob Kardashian.

Raia wa Uganda kupewa mafunzo ya kijeshi


Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameviagiza vikosi vya usalama kuanza kutoa mafunzo ya kijeshi kwa raia kama njia mojawapo ya kupigana vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabaab.
Amesema kuwa baada ya kundi hilo kushindwa na vikosi vya usalama vya umoja wa mataifa nchini Somalia,limeanza kuwashambulia raia wa kawaida na maeneo yasio na ulinzi,kama vile shambulizi la West gate na lile la Garissa nchini Kenya.
Kundi la Alshabaab pia lilitekeleza mashambulizi ya mabomu katika eneo la Kampala mwaka 2010 na kuwaua watu 70 waliokuwa wakiangalia mechi ya kombe la dunia.
Rais Museveni amewataka polisi ,jeshi na maafisa wa ujasusi kuwafunza raia wa Uganda ili kuwawezesha kuwalinda.

Kulingana na msemaji wa jeshi la Uganda Luteni Paddy Nkunda lengo lao sio Al Shabaab pekee.
Amesema kuwa sera hiyo inalenga kuwatuliza raia wenye ufahamu wa maswala ya usalama lakini hakuna atakayepewa silaha.
Maafisa wa serikali bado wanafanya mipango kuhusu ni lini mafunzo hayo yataanza pamoja na maelezo yao.
Kumekuwa na tamaduni ya wanafunzi wa shule za upili kupewa mazoezi wanapomaliza shule lakini mpango huo ulisitishwa katika miaka ya hivi karibuni.

Warundi 152,572 wawa raia wa Tanzania


Waliokuwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania zaidi ya 152,572 walioingia nchini humo tangu mwaka 1972, wamekabidhiwa vyeti vya uraia wa Tanzania na kuwa huru kuishi kama Watanzania wengine.
Wakimbizi hao walikuwa wameomba uraia wa Tanzania mwaka 2008 na kupewa na waziri wa mambo ya ndani mwaka 2010, sasa ni halali kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo za udiwani na ubunge.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa vyeti hivyo, mkuu wa makazi ya Mishamo, Frederick Nisajile alisema ugawaji wa vyeti hivyo ulianza Novemba 24 mwaka 2014 katika makazi ya Katumba mkoani Katavi magharibi mwa Tanzania ambako watu 56,554 walipewa vyeti vya uraia na baadaye kuhamia katika makazi ya Ulyankulu mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania ambako wakimbizi 43,453 tayari wamepewa vyeti hivyo.
Kwa upande wake msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Isaack Nantanga amesema hatua ya Tanzania kuwapa uraia wakimbizi hao ni kutokana na hiyari yao na kwamba serikali ya Tanzania ilishauriana na Burundi na hatimaye kukubaliana wapatiwe uraia wanaotaka wa kuwa Watanzania.
Hata hivyo si mara ya kwanza kwaTanzaniakutoa uraia kwa wakimbizi wanaoishi Tanzania kwa muda mrefu. Tanzania imefanya hivyo kwa wakimbizi wa Burundi na Somalia ambao wameishi Tanzania kwa miaka mingi.

Maandamano:Jeshi lasambazwa Burundi


Jeshi la Burundi limetawanywa nchini humo kujaribu kukabiliana na wale wanaopinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania muhula wa tatu.
Polisi walivunja maandamano ya Wanaharakati na wapinzani nchini humo waliongia mitaani kwa siku ya pili kufanya maandamano.
Waandamanaji kadha walipigwa risasi jana Jumapili na watu wanne wanaripotiwa kufariki

Tetemeko laua zaidi ya watu 3,600 Nepal


Watu wapatao 3,617 wamefahamika kufa katika tetemeko kubwa la ardhi lililoipiga Nepal Jumamosi.
Kituo cha Taifa cha Dharura cha Majanga kimesema watu zaidi ya 6,500 wamejeruhiwa.
Watu kadhaa pia wameripotiwa kufa katika nchi jirani za China na India
Zaidi ya wapanda milima 200 wameokolewa kuzunguka Mlima Everest, ambao umekumbwa na athari za tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8.
Wakaazi wengi wa mji mkuu Kathmandu wamekuwa wakilala katika mahema kwa wale wasio na makazi au wanaohofia kurudi majumbani kutokana na athari zaidi za tetemeko la ardhi zinazoendelea. Maelfu wamelala nje kwa siku ya pili Jumapili, baada ya tetemeko hilo kuipiga Nepal Jumamosi.
Maafisa wamesema idadi ya vifo au majeruhi ikaongezeka wakati huu ambapo vikosi vya waokoaji vimefanikiwa kufika katika ameneo ya milimani magharibi mwa Nepal.
Taarifa za awali zinasema jamii nyingi za watu, hususan wanaoishi karibu na kingo za mlima, wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na tetemeko hilo.
Mtu mmoja ambaye aliokolewa na helikopta kwenda katika mji wa Pokhara, kilomita 200 kutoka Kathmandu, amesema karibu kila nyumba katika kijiji chake chenye nyumba zaidi ya 1,000 kimeharibiwa, Bwana Darvas ameiambia BBC.