Menu - Pages
▼
Sunday, 31 May 2015
Mhudumu wa baa taabani kwa kifo cha mteja
Muhudumu mmoja wa baa amepatikana na hatia ya mauaji baada ya kumpa mteja wake jumla ya vipimo 56 vya pombe na kisha akafa.
Raia huyo wa Ufaransa alimpa Renaud Prudhomme, mwenye umri wa miaka 56, ''shoti'' 56 za mvinyo katika baa yake kwa nia ya kuvunja rekodi ya mywaji pombe nambari moja.
Marehemu Prudhomme, aliyekuwa ameandamana na binti yake kujiburudisha, alipelekwa nyumbani akiwa mlevi chakari.
Inaarifiwa kuwa alikimbizwa hospitalini ambapo alipatikana ameaga dunia siku iliyofuatia.
Hata hivyo mahakama ilimpata na hatia mhudumu huyo Gilles Crepin, mwenye umri wa miaka 47, kwa kumchochea marehemu Prudhomme aendelee kubugia mvinyo ilihali alikuwa mlevi kupindukia.
Mahakama ilisema kuwa Crepin aliendelea kuandika nani anayeshikilia rekodi hiyo kwenye ubao uliotundikwa hadharani kwa wateja wake.
Sasa Crepin amehukumiwa kifungo cha nyumbani cha miezi minne na kupigwa marufuku ya kufanya kazi katika baa yeyote kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Wakili wake Renaud Portejoie tayari amesema kuwa atakata rufaa dhidi ya kauli hiyo ya mahakama.
"kauli hii haina hata chembe ya haki bali ni hisia tu zilizotumika hapa ,ninavyoona mimi hizi ni jitihada za amahakama kutoa hukumu ili iwe funzo''
Awali alikuwa ameiambia mahakama kuwa kifo cha Prudhomme hakikutokea kimsingi na kufuatia matukio ya mteja wake kwani marehemu alikuwa na maradhi ya kupumua mbali na kuwa mraibu wa tembo.
''kwa hakika hatuwezi kuwalazimisha wateja wote wa pombe kutoa ithibati kuwa wako katika hali nzuri ya afya''
Wakili wa mwanawe marehemu Antoine Portal, alisema kuwa familia yao imetulizwa na marufuku hiyo ya Crepin ya mwaka mmoja.
''Nilikuwa nataka tu kuwakumbusha wahudumu wa baa kuwa ni kinyume cha sheria kuendelea kumpa pombe mlevi''
Ujerumani ina idadi ndogo zaidi ya watoto duniani
Idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Ujerumani imepungua zaidi ya mataifa yote duniani.
Utafiti umeonesha kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Ujerumani ndiyo ya chini zaidi duniani na sasa kunahofu kuwa kupungua kwa uzazi kutaathiri pakubwa uwezo wa vijana kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo tajiri zaidi barani Ulaya.
Watafiti wanaonya kuwa endapo jitihada mahsusi hazitafanywa ilikuimarisha idadi ya watoto nchini humo basi uchumi wa taifa hilo utaathirika vibaya.
Kulingana na utafiti huo,watoto 8.2 pekee walizaliwa miongoni mwa watu wazima 1000.
Awali idadi ya chini zaidi ilikuwa ya Japan ambayo huandikisha idadi ya watoto 8.4 wanaozaliwa miongoni mwa watu wazima 1000.
Kampuni ya uhasibu ya Ujerumani BDO ikishirikiana na chuo cha utafiti wa kiuchumi cha Hamburg Institute of International Economics (HWWI) ndiyo iliyoendesha utafiti huo kwa lengo la kutathmini uwezo wa uchumi wa taifa hilo kujiendesha mbali na viwango vya uzazi vinavyoripotiwa nchini humo.
Barani Ulaya, Ureno na Italia ziliorodheshwa katika nafasi ya tatu na nne zikiwa na jumla ya watoto 9.0 na 9.3 mtawalia.
Ufaransa na Uingereza zinasajili watoto 12.7 wanaozaliwa miongoni mwa watu wazima 1000.
Niger iliyoko Afrika ndiyo inayoandikisha idadi kubwa zaidi ya watoto wanaozaliwa duniani.
Nchini humo watoto 50 huzaliwa miongoni mwa watu wazima 1000.
Kulingana na utafiti huo wa BDO iwapo hali itaruhusiwa kuendelea hivyo basi idadi ya watu wenye umri wa kati ya miaka 20 na 65 wenye uwezo wa kufanya kazi na uwezo wa kuendesha uchumi wa taifa hilo itapungua kwa asilimia 61% hadi 54% ifikapo mwaka wa 2030.
Aidha afisa wa BDO Arno Probst, aliwatahadharisha wajerumani kuwa kiwango cha malipo na mishahara ya wafanyikazi kitaongezeka maradufu kadri ya upungufu wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi .
Probst alisema Ujerumani italazimika kuwaruhusu wahamiaji kuingia nchini humo na kufanya kazi ilikuepuka kuzorota kwa uchumi wake.
China yatetea miradi yake baharini
Mmoja wa makamanda wa ngazi za juu katika jeshi la China ametetea sera za China za kujenga miradi katika maeneo yanayozozaniwa baharini katika bahari ya kusini mwa china siku moja baada ya marekani kutaka miradi hiyo kusitishwa mara moja.
Su Jianguo ambaye ni naibu wa mkuu wa majeshi aliuambia mkutano mkuu nchini singapore kuwa miradi hiyo ina lengo la kuboresha uwezo wa China wa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na kusaidia eneo hilo.
Alisema kuwa kati ya majukumu hayo ni pamoja na jitihada za uokoaji, utunzi wa mazingira na uhuru wa safari za baharini. China inasema kuwa karibu eneo lote la kusini mwa bahari ya china ni lake.
Majeshi yazima shambulizi la Boko Haram.
Jeshi la Nigeria limezima mashambulizi ya wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram katika mji wa Maiduguri ulioko Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo.
Wapiganaji hao wa Kiislamu walikuwa wanafyatua makombora mazito mazito kuelekea mji huo usiku wa kuamkia leo lakini wanajeshi wakahimili mashambulizi na kuwakabili.
Watu 13 wameripotiwa kupoteza maisha yao katika mashambulizi hayo ya Boko Haram.
Shambulizi limetokea saa chache baada ya kuapishwa kwa rais mpya wa Nigeria Jenerali mstaafu Muhammadu Buhari ambaaye ameahidi kukabiliana na tishio la mashambulizi ya kigaidi ya Boko Haram bila huruma.
Mwandishi wa BBC aliyeko Nigeria anasema kuwa huenda hii ni njia ya kundi hilo la wapiganaji kumuonesha Rais mpya kuwa wangali wapo licha ya mashambulizi makali dhidi yao na majeshi ya muungano wa mataifa ya Magharibi mwa Afrika.
Rais Buhari akihutubia taifa punde baada ya kuapishwa alisema kuwa jeshi la taifa hilo litakita kambi yake katika mji huo wa Maiduguri ilikuitokomeza kabisa kundi hilo la waislamu la Boko Haram.
Awali Katika mahojiano maalumu na BBC, kiongozi huyo mstaafu wa jeshi amesema anatarajia kulishinda kundi hilo baada ya dhamira mpya kutoka jeshini na msaada wa nchi jirani.
"Kwa ushirikiano na majirani zetu Cameroon, Chad, Niger na jumuia ya kimataifa na dhamira ambayo tutapata kutoka katika jeshi, Nafikiri itachukua muda mfupi zaidi kukabiliana nao."
Jenerali Buhari amesema tayari ameainisha msingi wa tatizo linalokabili nchi ya Nigeria, lakini amewataka raia wa nchi hiyo kuwa wavumilivu.
"Tumebaini matatizo makubwa matatu.
Ambayo ni kukosekana kwa usalama nchini, tatizo ambalo kila mmoja analifahamu na lingine ni ukosefu wa ajira, hii ina maana uharibifu wa uchumi ikiwa ni kutokana na vitendo vya rushwa na rushwa yenyewe.
Matatizo haya matatu makuu, Wanigeria wote wanafahamu na tunaomba ushirikiano wa wananchi wa Nigeria,
wasitarajie miujiza kutokea katika kuyapatia ufumbuzi matatizo haya katika kipindi cha miezi michache baada ya kutwaa madaraka kwa sababu uharibifu umechukua miaka mingi,
miaka kumi na sita ya utawala wa chama tawala cha nchi hii." Anasema rais huyo mpya wa Nigeria.
Maandamano yafanyika Venezuela
Maelfu ya watu wamefanya maandamano ya amani nchini Venezuela wakipitia barabara za mji mkuu Caracas wakitaka kuachiliwa kwa viongozi wa upinzani ambao wamekuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Wanasiasa hao ni pamoja na mameya wawili wa zamani Leopoldo Lopez na Daniel Ceballos ambao wanazuiliwa kwa mashtaka ya kuchochea maandamano ya kuipinga serikali.
Rais wa Venezuela Nicholas Maduro amewalaumu kwa vifo 43 vilivyotokea wakati huo. Wiki hii wawili hao walitangaza kuanza mgomo wa kutokula wakiwa gerezani.
Nkurunziza:Sitahudhuria mkutano Tanzania
Msemaji wa rais wa Burundi amesema kuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza hatahudhuria mkutano wa viongozi wa kikanda ambao utaangazia mzozo ulio nchini mwake.
Msemaji huyo aliliambia shirika moja la habari la Ufaransa kuwa rais Pierre Nkurunziza atakuwa akifanya kampeni ya uchaguzi wa urais na kwamba waziri wa mashauri ya kigeni ndiye atahudhuria mkutano ambao utawajumuisha marais wa Rwanda, Uganda , Tanzania na Kenya mjini Dar es Salaam.
Wakati Nkurunziza alihudhuria mkutano kama huo mpema mwezi huu baadhi ya maafisa wa kijeshi walijaribu kumpindua.
Burundi imekumbwa na ghasia tangu Nkurunziza atangaze kuwa atawania urais kwa muhula wa tatu.
Hapo jana Nia ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu ilipata pigo baada Afisa mmoja tume hiyo ya uchaguzi kuiambia redio moja ya Ufaransa kuwa Spes Caritas Ndironkeye aliabiri ndege ijumaa na haijulikani kama alijiuzulu au la.
Tume hiyo ya uchaguzi ina maafisa wakuu watano na inaweza kuendelea kuhudumu hata baada ya kuondoka kwa mmoja wao.
Hata hivyo duru zinaelezea kuwa huenda afisa wa pili wa tume hiyo akajiondoa na hivyo kulemaza shughuli za tume hiyo.
Juma lililopita kanisa katoliki nchini Burundi lilijiondoa kutoka kwa harakati zozote za uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata siku moja tu kabla ya umoja wa Ulaya kuondoa maafisa wake katika shughuli hizo za uchaguzi.
Umoja wa ulaya ulikuwa umetuma maafisa wa kucimamia na kuhakikisha kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki.
Taarifa hiyo imetokea wakati ikisalia wiki moja tu uchaguzi wa wabunge na madiwani ufanyike nchini humo.
Kanisa katoliki ni kiungo muhimu katika suala la amani na demokrasia nchini Burundi tokea kuanzishwa mazungumzo ya amani ya Arusha mnamo miaka ya tisini.
Haya yamearifiwa wakati maandamano dhidi muhula wa tatu wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza yanaendelea kufanyika katika mitaa kadhaa ya mji mkuu Bujumbura kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Makundi ya kutetea haki za binadamu, yanasema kuwa zaidi ya watu 20 wamefariki wakati wa ghasia za maandamano,
Tangu rais Pierre Nkurunziza alipotangaza mwezi uliopita kuwa anapania kuwania tena kiti cha urais kwa muhula wa tatu, kinyume na katiba ya Burundi.
Uchaguzi wa urais umepangiwa kufanyika Juni tarehe tano, huku ule wa urais ukiwa mwishoni mwa mwezi huo wa Juni.