Menu - Pages
▼
Friday, 12 June 2015
WHO:Ebola yaongezeka Guinea na S Leone..
Shirika la afya duniani WHO limeelezea wasiwasi wake kwamba visa vipya vya maambukizi ya maradhi hatari ya Ebola vimeongezeka huko Guinea na Sierra Leone katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
WHO liliripoti kesi 31 mpya katika mataifa hayo mawili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tamaduni za mazishi ndizo zinachangia kusambaa kwa kasi kwa maradhi hayo licha ya tahadhari na mafunzo kupewa raia wa nchi kwamba waripoti visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya maambukizo ya Ebola na kuachia maafisa wa matibabu shughuli za mazishi ili yafanyike kwa utaratibu uliofuatwa.
Nigeria na mikakati dhidi ya Boko Haram...
Serikali ya Nigeria na nchi nyengine nne majirani zimekubaliana kuunda vikosi vya jeshi la pamoja ili kupambana na wapiganaji wa kiislamu wa Boko Haram.
Kikosi hicho kitapiga kambi katika mji mkuu wa Chad, Ndjamena, lakini kitakuwa chini ya usimamizi wa Nigeria.Nchi ya Chad, Cameroon, Niger na Benin pia zitatoa wanajeshi wake.
Baada ya mkutano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, katibu mkuu wa wizara ya ulinzi ya Nigeria, Aliyu Ismail, amesema kikosi hicho kitakuwa tayari kuanza kazi ifikapo mwezi July mwaka huu:"viongozi wa nchi na serikali za nchi za ukanda wa ziwa Chad na Benin zimechukua uamuzi ufuatao.
kupitisha dhana ya ufanyaji kazi, mikakati ya ufanyaji kazi na nyaraka zinazohusiana na kuundwa kwa vikosi vya pamoja katika kupambana na kundi la kigaidi la wapiganaji wa Boko Haram, kupitisha kupelekwa kwa vikosi hivyo katika makao makuu ya Ndjamena, Chad, kwa utekelezaji wa rasilimali watu na mahitaji ya kifedha.
Gari linalohisi mashimo barabarani..
Watafiti wa gari aina ya Landrover Jaguar wametengeza gari ambalo linaweza kuhisi mashimo yalio barabarani wakati linapoendeshwa.Sensa zilizopo katika gari hilo hubaini mashimo hayo na hutuma ujumbe wa data hiyo kwa haraka kwa madereva na mamlaka ya eneo hilo.
Mtoto azaliwa kutokana na mayai yaliohifadhiwa..
Mwanamke mmoja nchini Ubelgiji amekuwa wa kwanza duniani kujifungua mtoto kwa kutumia upandikizaji wa mayai ya mwanamke yaliowekwa katika jokovu alipokuwa mtoto.
Msichana huyo wa miaka 27 alikuwa na mayai yaliotolewa akiwa na umri wa miaka 13 kabla ya kuanza kupewa matibabu ya anemia ya seli.
Mayai yake yaliosalia yalifeli kutokana na matibabu hayo hatua ambayo ingeathiri uwezo wake wa kushika mimba bila upandikizaji huo.
Wataalam wanatumai kwamba mpango huo huenda ukawasaidia wagonjwa wengine wadogo.
Mwanamke huyo alijifungua mvulana mwenye afya nzuri mwezi Novemba mwaka 2014 na maelezo kuhusu swala hilo yalichapishwa siku ya jumatano katika jarida la kizazi cha binaadamu.
Mwanamke huyo ambaye hakutaka kujulikana alipatikana na ugonjwa wa anemia ya seli alipokuwa na umri wa miaka mitano.
Alihamia kutoka jamhuri ya Congo na kuelekea Ubelgiji ambapo madaktari waliamua ugonjwa wake ulikuwa hatari kwa yeye kufanyiwa upandikizaji wa uboho kwa kutumia tishu za kakaake zinazofanana na zake.
Lakini kabla ya kuanza upandikizaji huo walitakiwa kutumia kemikali ili kutibu mgonjwa huyo kwa lengo la kudhoofisha kinga yake ili kuzuia kutokataa tishu hiyo.
Matibabu ya kutumia kemikali yanaweza kuharibu kazi ya mayai hayo,kwa hivyo walitoa mayai yake ya upande wa kulia na kuyaweka katika jokovu.
Wakati huo,alikuwa akionyesha ishara za kubalekhe ,lakini alikuwa hajaanza kupata hedhi.Mayai yake yaliosali yalifeli akiwa na umri wa miaka 15.
Miaka kumi baadaye ,aliamua kwamba angetaka kupata mtoto,hivyobasi madaktari wakapandikiza mayai yake katika mayai yaliokuwa yamesalia na mayai mengine 11 katika sehemu zake nyingine mwilini.
Mgonjwa huo alianza kupata hedhi baada ya miezi mitano na kushika mimba akiwa na umri wa miaka 27.
Mkunga aliyeongoza tiba hiyo ya kumwezesha mgonjwa huyo kuweza kushika mimba Daktari Isabelle Demeestere alisema kuwa kuna matumaini kwamba mpango huo unaweza kuwasaidia vijana wengine ambao wanakabiliwa na hatari ya kufeli kwa mayai yao ya uzazi,hasa kutokana na ongezeko la idadi ya waathiriwa wa muda mrefu wa magonjwa ya damu wakiwa watoto.
Akosa taji la urembo kwa picha za uchi
Kwa mara ya pili mfululizo waandalizi wa shindano la malkia wa urembo nchini Zimbabwe wametupilia mbali ushindi wa taji hilo uliomwendea malkia wa urembo kufuatia sakata ya picha za uchi.
Emily Kachote alikuwa ameshinda taji la malkia wa urembo nchini Zimbabwe mnamo mwezi Aprili na alitarajiwa kuwakilisha taifa hilo katika mashindano ya dunia ya malkia wa urembo nchini Uchina mnamo mwezi disemba.
Lakini waandalizi wa taji hilo wanasema kuwa bi kachote alikiuka sheria ya shindano hilo ambalo linapinga wanaoshindana kupiga picha za uchi .
Nyota wa filamu ya Dracula afariki..
Mwigizaji wa siku nyingi na nyota wa filamu zilizopendwa na wengi Sir Christopher Lee amefariki akiwa na umri wa miaka 93.
Msanii huyo ambaye ni mzaliwa wa Uingereza aliyejenga jina lake kwa kuigiza katika filamu ya Dracula na Frankenstein katika filamu ya kutisha aligiza katika zaidi ya filamu 250.
Alijulikana sana kwa kuigiza kama Scaramanga katika filamu ya James Bond na Evil Wizard Suriman katika filamu ya Lord of the Rings.
Msanii huyo pia ameigiza katika filamu za The Wicker Man na Stars wars.
Inaripotiwa kuwa mwigizaji huyo alifariki siku ya jumapili katika hospitali ya Chelsea Westminster mjini London baada ya kulazwa na ugonjwa wa tatizo la mapafu na moyo.
Bajeti za Afrika mashariki zasomwa..
Serikali za Afrika mashariki zimetumia kodi kuvitahadharisha viwanda vyake kwa upande mmoja na kuwapa motisha wananuzi wa bidhaa kutoka nje wanaosaidia sekta muhimu kama vile miundo mbinu,kawi mbali na utekelezwaji wa itifaki ya soko la pamoja.
Katika mapendekezo ya bajeti yaliosomwa siku ya alhamisi Kenya, Uganda Rwanda na Tanzania zimepunguza kodi za bidhaa zinaozoagizwa kutoka nje kwa sekta muhimu kama vile kawi,mawasiliano na miundo mbinu.
Kulingana na gazeti la the east African nchini Kenya, shinikizo la kuimarisha miundo mbinu, kupunguza gharama ya kufanya biashara na kuongeza mtiririko wa mapato kutoka kwa mafuta na gesi iliogunduliwa katika eneo la Afrika mashariki umeyafanya mataifa manne ya eneo hili kushusha masharti ya sera za kodi ili kurahisisha biashara na majirani zao pamoja na mataifa ya kigeni.
Rwanda imepunguza kodi katika magari yanayoagizwa kutoka nje hususan matinga tinga,malori pamoja na mabasi ya uchukuzi.
Tanzania kwa upande wake imechukua mkondo kama huo na kupunguza kodi ya kuagiza bidhaa kutoka nje kutoka asilimia 25 hadi 10 miongoni mwa mabasi yanayobeba abiria 25 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uwiano wa kikanda unalenga kurahisisha biashara na kuzuia hasara inayokumba kampuni zinazofanya biashara katika eneo hili.
Hatahivyo,wafanyibiashara katika mataifa kama vile Rwanda na Uganda wanalazimika kulipia hasara inayotokana na masharti ya kibiashara yaliowekwa na wasanifu.
Ili kuondoa matatizo hayo Kenya imetangaza kuwa inapunguza masharti kadhaa ya kibiashara kupitia kuondoa forodha ya usalama katika uagizaji wa sukari ya viwanda na unga na ngano.
Uganda nayo imechukua mkondo huo kwa kuondoa forodha yake ya usalama kwa bidhaa na kuanzisha mtindo wa kulipa unaojulikana ambao unalenga kuleta uwiano.