Menu - Pages
▼
Monday, 15 June 2015
Waislamu Uingereza watakiwa kufungua mapema
Kiongozi wa kidini anayehusishwa na wakfu wa kiislamu nchini Uingereza anasema kuwa waislamu nchini humo wanapaswa kupunguza muda wanaofunga kula na kunywa wakati wa ramadhan kwani muda wao unazidi saa 19.
Dakta Usama Hasan ambaye ni msomi katika shirika moja linalowashughulikia waislamu Quilliam anasema japo mafundisho ya dini yanamtaka muumini wa dini hiyo kufunga kula na kunywa kuanzia asubuhi hadi jua linapotua waislamu nchini Uingereza hulazimika kufunga kwa zaidi ya saa 19.
Wito wake hata hivyo unapingwa na baadhi ya waislamu ambao wanasema kuwa ni sharti maadili na mafundisho ya dini yaheshimiwe.
Waislamu wanahitajika kususia kula kuanzia alfajiri hadi jua linapotua
Ratiba ya kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadan inatarajiwa kutolewa wakati wowote tayari kwa waislmu kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya dini hiyo.
Msafara wa baiskeli Tanzania
Mamia ya waendesha baiskeli walijitokeza kwenye msafara katika barabara za mji wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia zaidi usafiri huo kwa ajili ya afya bora huku wakiitaka serikali kupinga uonevu unaofanywa na waendesha magari ambao husababisha ajali za barabarani.
Huu ni mwaka wa tisa sasa msafara huu umekuwa ukifanyika jijini Dar es salaam
Mbali ya kuwa ni tukio la burudani baina ya marafiki na familia, msafara huu una ujumbe maalumu
"msafara huu ni wito kwa serikali na wadau wa miundombinu kutenga sehemu mahususi ya kupitisha baiskeli"
Dar es Salaam ina watumia barabara zaidi ya laki tatu .
Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya waendesha baiskeli mjini Dar es salaam UWABA Mejah Mbuya ,anasema idadi ya watumia baiskeli wanaofariki kutokana na ajali za barabarani ni asilimia 6 vifo vyote vitokanavyo na ajali barabarani.
''Anasema kuwa siku hii ni kubwa kutokana na kutokuwepo kwa waoneaji wa magari, lakini anatamani hali hii ingekuwa ni ya kila siku''
Hata hivyo, waandaaji wamesema tayari mabadiliko yanaonekana ndani ya miaka mitano iliyopita.
Shughuli hii inalenga kuondoa dhana kwamba ni chombo cha usafiri kwa watu maskini.
Anasema kuwa ''serikali imekuwa pamoja nao katika mipango yao ya miundombinu mijini kwa sababu ya misafara hii, na kuwa punguzo la vifo vya waendesha baiskeli''.
Shughuli hii inalenga kuondoa dhana kwamba ni chombo cha usafiri kwa watu maskini.
Na ukiangalia watu wanaotumia baiskeli siku hizi , unaona mambo yameanza kubadilika.
Utaona watu wenye uwezo wa kati na wale wa juu nao wameanza kuutumia.
Kasisi basha aishtaki kanisa kumbagua
Kasisi mmoja ambaye alinyimwa leseni ya kufanya kazi kama mhudumu katika zahanati ya afya kwa misingi ya kuwa katika ndoa ya jinsia moja ameishtaki kanisa kwa kumbagua.
Kasisi Jeremy Pemberton alikuwa amewasilisha pendekezo la kutaka kuhudumu kama Kasisi katika kanisa lililoko ndani ya hospitali.
Aidha kasisi Pemberton anadai kuwa maombi yake yalipingwa kwa kinywa kipana na kaimu askofu wa Southwell na Nottingham nchini Uingereza.
Rt Revd Richard Inwood alimkashifu kasisi Pemberton kuwa katika ndoa na mwanaume mwenza ambaye ni kinyume na mafundisho ya kanisa la Church of England.
Tume inayosimamia utoaji kazi nchini Uingereza inatazamia kuanza kuisikiza kesi hiyo leo.
Wadau wa maswala ya ajira wanasema kesi hiyo inatumiwa kama funzo na mtihani kwa tume hiyo ya ajira ya uingereza iwapo itazingatia haki za wafanyikazi ama zile za mwajiri.
Kasisi Pemberton alikuwa mhudumu wa kwanza kanisani kuoa nchini Uingereza.
Pemberton alifunga pingu za maisha mnamo mwezi wa Aprili mwaka wa 2014.
Askofu Inwood, alimnyima kazi kasisi Pemberton, na kisha akaiandikia barua bodi inayosimamia hospitali hiyo ya Sherwood Forest akiwashauri wasimpe kazi kasisi Pemberton.
Mwanajeshi wa Korea Kaskazini atorokea Kusini
Jeshi nchini Korea Kusini linasema kuwa mwanajeshi wa Korea Kaskazini ametoroka nchi hiyo na kuingia nchini Korea Kusini akipitia mpaka wa mkoa wa Gangwo
Mpaka wenye ulinzi mkali wa mkoa wa Gangwo
Kuhama kwa wanajeshi kupitia mpaka huo ulio chini ya ulinzi mkali si jambo la kawaida.
Korea Kusini ilichukua hatua za kuboresha ulinzi kwenye mpaka kufuatia tukio la mwaka 2012 wakati mwanajeshi mwingine kutoka Korea Kaskazini alivuka mpaka usiku wa manane na kuingia nchini Korea Kusini.
Amama Mbabazi atampinga rais Museveni
Waziri mkuu wa zamani wa Uganda Amama Mbabazi atampinga rais Yoweri Museveni kuwania tikiti ya urais wa chama cha NRM.
Bwana Amama Mbabazi anataka kuwania kiti cha urais dhidi ya mwandani wake wa zamani katika uchaguzi utakaokuwa mwakani.
Kupitia kwa taarifa aliyoichapisha kwenye mtandao wa Youtube, bwana Mbabazi aliahidi
''kufufua na kuleta muamko mpya nchini Uganda.''
Rais Museveni ametawala Uganda tangu mwaka wa 1986 na anatarajiwa kuwania urais kwa muhula wake wa nne.
Museveni alimfuta kazi bwana Mbabazi mwaka uliopita katika hatua iliyotafsiriwa na wachanganuzi wa kisiasa nchini humo kuwa mbinu ya kukandamiza mpinzani wake mkuu.
Bwana Mbabazi anakabiliwa na changamoto kubwa ya kushinda uteuzi katika chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).
Rais Museveni tayari ameidhinishwa na kamati kuu ya chama japo anahitaji kupokea ithibati ya wanachama katika mkutano mkuu wa wajumbe.
Iwapo atakonga nyoyo za wajumbe wa NRM sasa Mbabazi sasa atawania urais dhifi ya Museveni
Mwandishi wa BBC Rachael Akidi anasema kuwa hii ndiyo itakayokuwa mtihani mkubwa zaidi kuwahi kumkabili rais Museveni ndani ya chama cha NRM.
Al Shabaab 1 raia wa UK auawa Kenya
Utafiti wa DNA unatarajiwa kuthibitisha kuwa mmoja wa wapiganaji 11 wa Al shabaab waliouawa na wanajeshi wa Kenya hapo jana alikuwa ni raia wa Uingereza.
Duru za kijasusi za jeshi la Kenya zinasema kuwa mmoja kati ya watu wawili wazungu waliouawa anafahamika kama Thomas Evans, 25, ambaye ni raia wa Uingereza na anayetokea Buckinghamshire.
Bwana Evans, alisilimu na kubadili jina lake na kuitwa Abdul Hakim.
Familia yake imeiambia BBC kuwa inasubiri hakikisho kutoka kwa serikali ya Uingereza kuwa ndiye aliyeuawa.
Shambulizi hilo lilitokea jana alfajiri katika kambi ndogo ya kijeshi iliyoko Baure karibu na Lamu ambapo wanajeshi sasa wamethibitisha kuwa waliwauawa watu 11 na kupata bunduki 13 na mizinga mingine tano.
Maafisa wa utawala nchini uingereza wanashirikiana na utawala nchini Kenya kubaini haswa ni nani aliyeuawa.
Kwa mujibu wa polisi katika bonde la Thames nchini Uingereza , mamake Thomas bi Sally Evans amenukuliwa akisema kuwa ''yeye na mwanaye Michael wanasubiri thibitisho kutoka kwa duru za polisi''
Awali Familia yake ilikuwa imeilaumu idara ya uhamiaji ya Uingereza kwa kumruhusu kuondoka nchini humo.
Evans alisafiri kuelekea Misri mwaka wa 2011 punde baada ya kunyimwa ruhusa ya kuenda Kenya.
Mnamo mwaka wa 2012 Evans inafahamika alimuarifu mamake kuwa amesafiri hadi Somalia kujiunga na wapiganaji wa kundi la Al Shabaab.
Takriban raia 50 wa Uingereza wanaaminika kuwa wamejiunga na al-Shabaab nchini Somalia.
Kundi hilo ndilo linalolaumiwa kwa kutekeleza mashambulizi kadha nchini Kenya na pia Somalia.
Iwapo mwili huo utathibitishwa kuwa wa Evans basi itakuwa ndio mara ya kwanza kwa raia wa Uingereza kuuawa cnhini kenya akipigania kundi la wanamgambo wa Al Shabaab.
Bashir amewasili mjini Khartoum Sudan..
Rais Omar al Bashir wa Sudan amewasili mjini Khartoum Sudan kutoka nchini Afrika Kusini.
Rais Bashir amekariri kuwa hana hatia yeyote wala hajui kwanini mahakama ya kimatiafa ya ICC inasisitiza kumchafulia jina.
Shirika la habari ya AFP limemnukuu rais Bashir akifoka ''Allah Akbar'' aliposhuka kutoka kwa ndege iliyombeba.
Aidha aliinua mkongojo wake juu na kushabikiwa na wafuasi wake.
Waziri wa maswala ya kigeni wa Sudan Ibrahim Ghandour aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ya Afrika Kusini ilikuwa imemkariria rais Bashir kuwa kuwepo kwake mjini johannesburg ilikuwa ni tukio la kushabikiwa na lenye heshima kubwa kwa hivyo hakukuwa na uwezekano wowowte wake kukamatwa.
Rais Huyo alikuwa ameratibiwa kuhutubia umma lakini kinasa sauti kikaharibika na akaondoka.
Rais bashir aliingia katika gari lake lililowazi na akaondoka uwanjani huku akishabikiwa na wafuasi wake.
Awali kuondoka kwake nchini Afrika Kusini kulikumbwa na atiati, baada ya mahakama moja kuamuru rais huyo asiondoke nchini humo hadi mahakama hiyo itakaposikiza kesi na kuamua iwapo atakamatwa na apelekwe mjini the Hague Uholanzi au la.
Awali Mwandishi wa BBC aliyeko Afrika Kusini Nomsa Maseko, alisema kuwa ndege ya rais al Bashir ilijazwa mafuta jana usiku na kuwekwa mstari wa mbele tayari kabisa kuondoka katika uwanja wa ndege wa kijeshi.
Rais Bashir aliondoka licha ya kuwepo amri ya mahakama ya kumzuia kuondoka nchini humo hadi kesi dhidi yake itakaposikizwa na kuamuliwa.
Mahakama hiyo ilikuwa inapaswa kuamua ikiwa Bwana al-Bashir atakabidhiwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC yenye makao yake mjini Hague Uholanzi ilikukabiliana na mashtaka ya uhalifu wa kivita na mauaji yahalaiki yanayomkabili .
Majaji watatu waliokuwa wanasikiza kesi hiyo dhidi yake wamemtaka waziri wa usalama wa ndani nchini humo kueleza ni vipi rais Bashir aliruhusiwa kukaidi amri ya mahakama .