Menu - Pages
▼
Friday, 3 July 2015
WHO:Cuba haina Kaswende, ukimwi kwa watoto.
Shirika la afya duniani WHO, limethibitisha kuwa Cuba imemaliza kabisa maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama mzazi na Kaswende.
Mkuu wa shirika hilo WHO, Daktari Margaret Chan, ametaja ufanisi huo kuwa ''ni mkubwa zaidi kuwahi kutokea kwa afya ya umma.''
Mafanikio hayo ya kutajika yanafuatia kampeini ya muda mrefu miongoni mwa wanawake waja wazito ambao wamekuwa wakishauriwa kuanza kupokea matibabu mapema na kufanyiwa vipimo mahsusi ilikujua hali ya afya ya mama na mwanaye .
WHO inatumai kuwa mafanikio hayo ya Cuba yataigwa na mataifa mengine.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, Kila mwaka takriban wanawake milioni moja nukta nne (1.4) i walioambukizwa virusi vya ukimwi duniani, hupata uja uzito.
Iwapo hawapokei matibabu mapema asilimia 15-45% ya wanawake hao huwaambukiza watoto wanaojifungua wakati wa kujifungua na pia kupitia kwa maziwa ya mama.
Hatari ya maambukizi hupungua kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia moja pekee 1% baada ya kupokea madawa ya kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi.
Aidha wanawake wengine milioni moja huambukizwa kaswende wakiwa wajawazito kila mwaka.
Iwapo wanawake hao watapokea matibabu mapema wanaweza kuzuia kuwaambukiza watoto wao.
Kote duniani wanawake waja wazito 7 kati ya 10 ambao wameambukizwa ukimwi hupokea,madawa ya kupunguza makali ya ukimwi
Nchini Cuba, chini ya asilimia 2% ya watoto huzaliwa na maambukizi ya maradhi hayo.
Hii ikiwa ni kiwango cha chini mno kinachoweza kufikiwa kufuatia matibabu.
Kote duniani wanawake 7 kati ya 10 ambao wameambukizwa ukimwi hupokea,madawa ya kupunguza makali ya ukimwi ilikuzuia maambukizi kwa watoto watakaojifungua.
Dr Carissa Etienne, ambaye amekuwa akishirikiana na WHO amesema kuwa mafanikio ya Cuba yanapaswa kuigwa kote duniani ilikupunguza au hata kumaliza kabisa maambukizi ya Ukimwi na kaswende kutoka kwa mama mja mzito kwa mwanawe.
Lazima ruhusa ya kushika mimba Uchina
Kampuni moja ya Uchina inapanga kutoa masharti ambapo wafanyikazi wake watatakiwa kupata ruhusa kabla ya kuanza familia.
Sheria hizo zimechapishwa na kuzua malalamiko mengi katika mitandao.
Sheria kuu inaelezea kwamba wanawake wote walio kwenye ndoa lazima wawe wamehudumu kwa mwaka mmoja kwenye kampuni hiyo kabla ya kutuma kibali cha kukubaliwa kushika mimba.
Yeyote atakayeshika mimba kinyume cha sheria hiyo atatozwa faini na kunyimwa madaraka yoyote, hata kama amefuzu.
Shirika la utangazaji nchini China limekosoa vikali kampuni hiyo iliyoko mkoa wa Henan na kusema haina ubinadamu kwa wafanyikazi wake.
Muingilio wa masuala binafsi China ni jambo rasmi, hasa sheria ya mtoto mmoja iliyowekwa na serikali miaka ya sabini. Hii iliwalazimisha wazazi kupata mtoto mmoja pakee.
Roboti yamuua mfanyikazi wa Volkswagen.
Mfanyikazi mmoja katika kiwanda cha kutengeza magari aina ya Volkswagen nchini Ujerumani amefariki baada ya roboti kum'beba na kumuangusha katika chuma
Marehemu mwenye umri wa miaka 22 alifariki hospitalini kufuatia ajali hiyo iliofanyika katika kiwanda kimoja kilichopo Baunatal yapata kilomita 100 kazkazini mwa Mji wa Frankfurt.
Alikuwa akifanya kazi miongoni mwa wafanyikazi wa kandarasi wa kuiweka roboti hiyo wakati ilipomkamata kulingana na na kampuni hiyo ya Kutengeza gari ya ujerumani.
Hatahivyo Heiko Helwig amelaumu makosa ya binadaamu kama sababu ya tukio hilo badala ya roboti hiyo.
Roboti hiyo hutumiwa kubeba vipuri katika kampuni hiyo.
Puff Daddy aepuka jela.
Msanii wa muziki aina ya rap Sean P Diddy Combs amesema kuwa hatakabiliwa na mashtaka ya shambulio kufuatia kisa kimoja mwezi uliopita kilichohusisha uzani wa 'kettlebell'.
P Diddy aliye na umri wa miaka 45 alikamatwa mnamo Juni 22 kwa tuhuma za kushambulia kwa kutumia silaha hatari katika chuo kikuu cha California.
Alizuiliwa katika jela kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya dola 160,000.
Hakimu wa wilaya hiyo ameipeleka kesi hiyo katika mji wa Los Angeles kuamua iwapo Combs atakabiliwa na mashtaka hafifu.
''Tunafurahia kwamba hakimu alikataa mashtaka ya kutumia nguvu kupitia kiasi dhidi ya Combs'',alisema wakili wake.
P Diddy na mwanawe Justin Combs
Vyombo vya habari vilisema kuwa P Diddy alihusika katika mgogoro kati yake na kocha wa timu ya soka ya Marekani chuoni humo.
Hatahivyo Combs amesema kuwa alikuwa akimtetea mwanawe Justin Combs ambaye ni mchezaji wa timu ya chuo hicho na kwamba alikuwa akifanya mazoezi wakati wa tukio hilo.
Bidhaa zauzwa bila nembo ya ubora TZ.
Soko la Tanzania limekuwa likipokea bidhaa kutoka ndani na nje ya nchi lakini baadhi ya bidhaa zinaarifiwa kuuzwa madukani huku zikikosa nembo za ubora.
Baadhi ya bidhaa hizo pia zimeonekana kuuzwa katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Katika maonyesho kama hayo ya biashara ya saba saba nchini Tanzania huwa ni fursa ya wafanyibiashara na wajasiriamali kuonyesha bidhaa zao mbali mbali lakini kwa wengine huwa wanatumia fursa hiyo kusambaza na kuuza bidhaa duni kwa bei ya kutupa.
katika maonyesho hayo bidhaa hizo na nyingine zinaendelea kuuzwa huku kukiwa na sheria na utaratibu kamili .
Bi Roida Andusamile ni msemaji wa shirika la viwango Tanzania na anasema hali halisi ni kwamba kuna baadhi ya wajasiriamali ambao wanaonyesha biashara zao wakati bidhaa zao hazijathibitishwa na shirika la viwango kuwa zina ubora.
Hata hivyo viongozi wa maonyesho hayo wanasisitiza kuwa wameweka uthibiti wa kutosha ili kukinzana na tatizo hili la bidhaa feki katika maonyesho hayo ya biashara.
Ingawa baadhi ya wafanya bishara wanakiri kukosa kiambishi cha kuonyesha ubora wa bidhaa zao zinawanyima soko , sio nyumbani tu lakini hata kimataifa kwa kuwa uwezo wao bado ni mdogo ingawa bidhaa zao zina ubora.
Wakati maonyesho hayo yakiendelea, maafisa wa serikali wanachukua fursa ya kuwepo kwenye maonyesho na kutoa mafunzo kuhusu ubora wa bidhaa .
Mamlaka ya chakula na dawa inasema iko makini katika hilo kwani maafisa wao bado hutembelea mabanda ili kubaini bidhaa feki zilizoingia.
Afisa wa uelimishaji jamii;James Ndege anasema sio vyema kuwalaumu wafanyabiashara pekee yao kutokana na tatizo hili kwani tatizo la bidhaa feki linamgusa kila mmoja.
Hata hivyo bidhaa hizi zisizo na viwango zimekuwa ni changamoto kwa kuwa na athari nyingi kiafya na usimamizi wake kuwa mgumu.
Buhari alaani mauaji ya Boko Haram.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amelaani misururu ya mauaji yaliyotekelezwa na wapiganaji wa Boko Haram.
Buhari ameyataja mauaji ya watu 150 Kaskazini Mashariki mwa nchi kama ya kikatili na ukiukaji mkubwa wa kibinadamu.
Rais huyo aidha ametaka ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na wapiganaji hao.
Wakati huo huo Rais wa Ufaransa, Francois Hollande anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenzake wa Cameroon Paul Biya ambaye amechangia kikiso maalum cha kukabiliana na Boko Haram.
AMISOM:Hatutaondoka Somalia.
Wanajeshi wa umoja wa Afrika nchini Somalia Amisom hawataondoka katika miji yoyote ya kusini mwa Somalia kinyume na ripoti za vyombo vya habari,kwa mujibu wa Amisom
Kumekuwa na ripoti kwamba wanajeshi hao wamekuwa wakiondoka katika miji mitano ya Somalia,lakini mwakilishi wa Umoja huo nchini Somalia balozi Maman Sidikou amesema kuwa huo ni uvumi unaolenga kuzua hofu.
Ameongezea kuwa vikosi vya AU vinapangwa kuendeleza vita dhidi ya kundi la La Alshabaab.
Ugiriki yaombwa kusema, 'La'
Waziri MKuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amewaomba wapiga kura kupinga vitisho na kusema 'La' wakati wa kura ya maamuzi ya hapo Jumapili.
Katika hotupa fupi kwenye runinga ya taifa, Bw Tsipras amesisitiza kwamba hakuna tisho lolote la Ugiriki kufukuzwa kutoka Muungano wa Ulaya.
Amewaambia wafuasi wake kupuuza kelele za wale aliowataja kama wanaotoa vitisho.
Hapo Jumapili wapiga kura wa Ugiriki wataamua kuunga au kukataa masharti ya kupokea mkopo kutoka kwa mashirika ya kimataifa.
Ugiriki ilishindwa kuafikiana na wakopeshaji wake wakati wa mazungumzo ya miezi kadhaa.Viongozi wa Ulaya wameonya kwamba kura ya 'La' huenda ikasababisha Ugiriki kuondoka kanda inayotumia sarafu ya Euro.
Tayari uchumi wa Ugiriki unakumbwa na msukosuko mkubwa baada ya nchi hiyo kushindwa kupata mkopo wa dharura.
Benki za nchi zimefungwa huku kukiwekwa kiwango rasmi ambacho wateja wanafaa kutoa.
Hakujafanyika mihadhara, mikubwa mjini Athens lakini mabango ya mirengo ya 'La' na 'Ndio' yametawala kote mjini Athens kila upande ukijaribu kuwashawishi wapiga kura.