Menu - Pages
▼
Friday, 12 February 2016
Riek Machar makamu wa rais Sudan Kusini...BBC
Katika kutafuta amani ya Sudan Kusini, Rais Salva Kiir amemteua mpinzani wake Riek Machar kuwa makamu wa rais.Majeshi yanayowatii watu hawa wawili , walipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha watu zaidi ya milioni moja na nusu kukimbia makazi yao.
Machar ambaye alikuwa amehaidiwa wadhifa huo wa makamu wa raisi kama atakubali kuweka sahihi katika makubalino ya kuleta amani ulifanyika mwezi Agosti mwaka jana .lakini bado baadhi ya majeshi yamejigawa na kuendeleza mapigano katika baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini.
Mtangazaji akisoma kwa sauti ya juu amri ya raisi kumteua Machar kuwa msaidizi wake,amri hiyo ilisomwa kama ifuatavyo;katika zoezi la mgawanyiko wa utawala chini ya kifungu namba 524 cha sheria cha kwanza cha makubaliano ya kufikia hatima ya mgogoro unaoendelea jamuhuri ya sudan ya kusini.
Salva Kiir,raisi wa Jamuhuri ya Sudan ya kusini amemteu Dr,Riek Machar kuwa makamu wa kwanza wa raisi ya jamuhuri ya Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 11 Februari 2016
Wanasayansi wagundua mvutano wa mawimbi...BBC
Wanasayansi nchini Marekani wamefanikiwa kubaini Mvutano wa asili wa mawimbi na kusema uvumbuzi huo unawapa mwanya mpya wa kuuelewa ulimwengu zaidi.
Albert Einstein alitabiri kuwa uwepo wa mvutano huo wa mawimbi karne iliyopita,Nadharia yake ilikuwa kwa ujumla ikihusisha jimbo ambalo linasafiri kwa kasi na kumulika mwanga ikiwa inajaribu kujikunja na kutaka kutosha katika muda unaotumika.
Mpaka sasa wamedhibitisha kuwa ni ndoto,ingawa watafiti wa LIGO na mashuhuda wa suala hili nchini Marekani,wanasema kadri wanavyoyaona mawimbi yanayotoka katika mashimo mawili meusi wanaamini kuwa hiyo ni ishara iliyo wazi kabisa.
Msemaji wa wanasayansi hao Gabby Gonzalez anaeleza;"tunasikia mvutano wa asili wa mawimbi hayo,tunaona mzunguko wake ni jambo zuri kwa kweli kwa kuwa hatuoni tu maajabu ya ulimwengu bali tunasikia,lakini kiufupi hilo ni jambo ambalo halikubaliki,na sisi tulichokifanya ni kupata ishara ya sauti tu,''umesikia hiyo sauti nzuri?Ni sauti tu inayounguruma,oops hiyo ndiyo sauti tuliyokuwa tunaipima"
wakati katika mkutano wa habari mjini washington,mkurugenzi mtendaji wa Interferometer Gravitational wave Obsever Dave Rietze - akitoa tangazo hili:"mabibi na mabwana ,tumeweza kuchunguza mvutano huo wa asili wa mawimbi,na tumeweza,nina furaha kubwa kuwaambia kuwa mivutano wa asili wa mawimbi haya yaliandaliwa na katika mashimo mawili meusi ambayo yanakuja kwa pamoja na kutengeneza shimo moja,ni kama kitu cha miongo kadhaa iliyopita"
ICC kuamua juu ya William Ruto...BBC
Mahakama ya jinai ya kimataifa -ICC leo inatarajiwa kutoa uamuzi ambao huenda ukakuwa na athari kwa kesi inayomkabili naibu rais wa Kenya William Ruto. Bwana Ruto na mushtakiwa mwenzake, mwana habari Joshua arap sang wameshatkiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu kuhusiana na ghasia zilizotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Mashtaka kama hayo yaliyomkabili rais Uhuru Kenyatta yalifutiliwa mbali na mwendesha mkuu wa mashataka ya ICC, Fatou Bensouda kwa ukosefu wa ushahidi.
Bunge lachafuka A.Kusini, Malema nje...BBC
Kumetokea malumbano makali bungeni nchini Afrika Kusini ambapo wanasiasa wa upinzani wamechelewesha hotuba ya rais Jacob Zuma aliyekuwa akilihutubia taifa na kuzua maswali kuhusu utaratibu.
Baadhi ya wanasiasa wanasema rais huyo hakupaswa kuhutubia bunge kutokana na kashfa mbali mbali alizonazo
Ni mvutano huo baada ya spika wa bunge la Afrika Kusini mama Baleka Mbete na wafuasi wa upinzani wengi wao kutoka chama cha Ecoomic Freedom Fighters EFF wakiongozwa na Juliasi Malema ambao walikuwa wanadai kutaka utaratibu na kuvuruga hotuba ya Rais Jacob Zuma..
Hatimaye uvumilivu ukamshsinda spika wa bunge Baleka Mbete na kumuru kiongozi wa EFF Julias Malema kutolewa nje ya ukumbi wa bunge.
Baada ya fujo hizo Rais Jacob Zuma alijaribu kuendelea kuhutubia lakini wabunge wa upinzani walibaki wakarudia tena kumkatiza
Baada fujo hizo baadae angalau kidogo pakawa na utulivu ambapo Rais Zuma aliweza kumalizia hotuba yake na Katika hotuba hiyo Rais Zuma mbali na mambo mengine alisema serikali yake imekuwa akibana matumizi lakini anaona bado hatua zaidi zinahitajika.
"Tumekuwa tukichukua hatua za kubana matumizi ya fedha za umma kwa hekima ikiwa ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima. Lakini bila kuathiri wajibu muhimu wa serikali na kutoa huduma kwa raia. Mwaka 2013 waziri wa fedha alitangaza hatua za kubana matumizi. Matumizi ya ziada na yale yasiyo ya lazima yamepunguzwa lakini bado hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kubana upotevu wa fedha za umma."
Rais Zuma anakabiliwa na kashfa kadhaa lakini kubwa la hivi karibuni ni hatua ya kutumia fedha za umma kufanya ukarabati wa kasri lake la kifahari la Nkandla.
Clinton na Sanders wajibizana kuhusu Obama...BBC
Wagombea urais wa chama cha Democratic Marekani Hillary Clinton na Bernie Sanders wamejibizana kuhusu Rais Barack Obama kwenye madahalo wa kwanza tangu kumalizika kwa mchujo wa New Hampshire.
Bi Clinton alijionesha kama mlinzi wa sifa za utawala wa Barack Obama, na kumshambulia Bw Sanders kwa kumkosoa rais huyo.
“Ukosoaji ambao nimekuwa nikisikia kutoka kwa Seneta Sanders, ningetarajia hilo kutoka kwa wafuasi wa Republican pekee,” Bi Clinton alisema.
Bi Clinton tena na tena alirejelea uhusiano wake mwema na Bw Obama ambaye anapendwa sana na makundi ya wachache Marekani, hasa Wamarekani weusi.
Bw Sanders kwa upande wake alijaribu sana kuweka ujumbe wake kuonesha kwamba anataka kutetea usawa wa kiuchumi na kuwasaidia Waamerika weusi.
Bi Clinton alisisitiza kwamba ujumbe wake unaambatana na vitendo, na akatilia shaka ahadi ya Bw Sanders ya kutoa huduma ya afya kwa wote na kuondoa karo katika taasisi za elimu ya juu.
“Tunawajibika kueleza kwa uwazi yale ambayo tunayoahidi na ndiyo maana hatuwezi kutoa ahadi ambazo hatuwezi kutimiza,” Bi Clinton alisema.
Wagombea wanajiandaa kwa uchaguzi wa mchujo katika majimbo ya Nevada na South Carolina, ambayo yana raia wengi wa makundi ya wachache.
Bi Clinton anajaribu kujenga upya kampeni yake baada ya kushindwa pakubwa na Bw Sanders kwenye mchujo wa New Hampshire.
Alipokea uungwaji mkono muhimu kutoka kwa kundi la wabunge weusi katika chama cha Democratic mnamo Alhamisi.
Sanders, seneta wa Vermont, alishinda New Hampshire kwa zaidi ya asilimia 22 na alishindwa mchujo wa Iowa kwa kura chache mno.
Lakini majimbo hayo yote yana Wazungu wengi.
Sasa anakabiliwa na changamoto ya kutafuta kura miongoni mwa watu wa asili ya Amerika Kusini na Mexico pamoja na Wamarekani weusi katika majimbo ya Nevada na South Carolina.
Bi Clinton anaungwa mkono sana na makundi hayo na anatarajiwa kufanya vyema Nevada na South Carolina.
Kura ya maoni ya karibuni iliyofanywa na NBC News/Wall Street Journal/Marist jimbo la South Carolina ilisema Bi Clinton anaongoza akiwa na asilimia 74 ya kura dhidi ya Bw Sanders mwenye asilimia 17 miongoni mwa wapiga kura weusi.
Syria: Mataifa yaafikiana vita visitishwe...BBC
Mataifa yenye ushawishi duniani yameafikiana kuhusu mkataba wa kusitisha mapigano nchini Syria ambao utaanza kutekelezwa katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo nchini Ujerumani.
Mwafaka huo hata hivyo hautahusisha makundi ya kijiihadi ya Islamic State (IS) na al-Nusra Front.
Mawaziri wa mataifa wanachama wa Kundi la Kimataifa la Kusaidia Syria pia wamekubaliana kuharakisha na kuongeza juhudi za kutoa misaada.
Tangazo hilo limetokea huku jeshi la Syria, likisaidiwa na Urusi kwa mashambulio ya kutoka angani, likiendelea kupiga hatua eneo la Aleppo.
Hatua hiyo ya kijeshi inatishia kuzingira maelfu ya raia katika maeneo mengi ya mji wa Aleppo yanayodhibitiwa na waasi.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amekiri kwamba mpango wa kusitisha mapigano unaazimia kutimiza makuu lakini akasema changamoto kubwa itakuwa kuona iwapo pande zote zitaheshimu mkataba huo.
“Kile tulicho nacho kwa sasa ni ahadi kwenye karatasi, siku chache zijazo tunafaa kusubiri tuone iwapo hayo yatatekelezwa,” amesema.
Jopo kazi linaloongozwa na Marekani na Urusi litasaidia kutekeleza mkataba huo kupitia mashauriano na makundi yanayopigana nchini Syria.
Misaada inatarajiwa kuanza kufikishwa kwa raia waliozingirwa na majeshi katika baadhi ya maeneo Ijumaa.
Bw Kerry ametoa tangazo la kupatikana kwa mwafaka huo akiandamana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov na mjumbe maalim wa Umoja wa Mataifa Syria, Staffan de Mistura.
Bw Lavrov amesema kuna sababu za kuwa na matumaini kwamba “tumefanya kazi kubwa na nzuri leo”. Pendekezo la awali kutoka Urusi lilikusudia mapigano yasitishwe kuanzia tarehe 1 Machi.
Thursday, 11 February 2016
Roboti inayoiga Mende ..BBC
Wanasayansi nchini Marekani wametengeneza roboti inayofanana na mende ambayo inaweza kutumiwa kuwaokoa watu kunapotokea tetemeko la ardhi.
Watafiti wanasema roboti hiyo inatumia mbinu zinazotumiwa na mende kutembea kwenye nyufa kupenya vifusi na kuwaokoa walionaswa katika maporomoko.
Wanasayansi hao wanasema kuwa endapo roboti hiyo inawezavishwa kamera kisha ikatumwa kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka inaweza kurahisisha uchunguzi wa usalama wa vifusi kabla ya makundi waokoaji kuingia.
Ukubwa wa roboti hiyo ni sawa na kiganja cha mwanadamu.
Roboti hiyo inaweza kupenyeza katika mianya midogo maradufu ama nusu wa ukubwa wake.
Miguu yake inapanuka kama vile mende.
Utafiti huo umechapishwa katika jarida la kisayansi lijulikanalo kama ''Proceedings of the National Academy of Sciences''.
Ashtakiwa kwa kumrusha burukenge mgahawani....BBC
Mtu mmoja mjini Florida anakabiliwa na mashtaka ya unyanyasaji baada ya kumtupa burukenge katika mgahawa mmoja wa chakula.
Joshua James mwenye umri wa miaka 23,ametuhumiwa kwa kumtupa mnyama huyo aliye hai kupitia dirisha la mgahawa huo wa Wendy.
Mamaake amesema kuwa alikuwa akitaka kumtania rafikiye aliyekuwa akifanya kazi katika mgahawa huo.
Mnyama huyo alikamatwa na kurudishwa msituni.
Bwana James kutoka eneo la Jupiter mjini Florida alimpata burukenge huyo katika upande mmoja wa barabara na kumbeba katika lori lake,kulingana na ripoti ya tume ya kuwahifadhi wanyama mjini Florida.
Baadaye alienda katika mgahawa huo huko Royal Palm Beach,ambapo aliagiza kinywaji katika dirisha la mgahawa huo kabla ya kumrusha nyama huyo mwenye urefu wa futi tatu kupitia dirisha hilo.
Kisa hicho kilitokea mnamo mwezi Octoba lakini mshukiwa amekamatwa na anazuiliwa kwa sasa.
Pia anakabiliwa na mashtaka ya umiliki wa mnyama huyo pamoja na usafirishaji wake kinyume cha sheria.
Ndege yenye shimo: Maswali 5 bila majibu...BBC
Ndege moja ya abiria ililazimika kutua kwa dharura baada ya bomu kulipuka ilipokuwa angani muda mchache tu kutoka uwanja wa ndege wa Mogadishu.
Rubani wa ndege hiyo alilazimika kurejea ardhini baada shimo kubwa kutokea karibu na hifadhi ya mafuta katika sehemu ya kulia ya ubavu wa ndege hiyo ya Daallo Airlines.
Licha ya serikali ya Somalia kukiri kuwa bomu lililotegwa ndani ya ndege hiyo ndiyo iliyosababisha shimo hilo maswali mengi yamebakia bila majibu.
Nani aliweka bomu hiyo ndani ya ndege?
Ripoti moja ya uchunguzi ilidai kuwa mshukiwa mkuu aliyetega bomu hiyo ndiye aliyetupwa nje kutokana na kishindo cha mlipuko huo ndege ikiwa angani.
Afisa mmoja wa serikali ya Somali alisema kuwa mshukiwa huyo Abdulahi Abdisalam Borle, raia wa Somalia alikuwa na umri wa 55 .
Ndege hiyo ya shirika la ndege la Daallo, ilikuwa ikielekea Djibouti, na ilikuwa imebeba abiria 60.
Awalio duru zilisema kuwa abiria hao walikuwa wamenunua tiketi ya shirika la ndege la uturuki ila walilazimika kuabiri ndege hiyo ya daalo baada ya ile ya Uturuki kukosa kufika kwa wakati siku hiyo.
Kuna dukuduku kuwa abiria huyo alikuwa amebebwa kwenye kiti chenye magurudumu ila kauli hiyo imepingwa na mkurugenzi wa Daallo Airlines bwana Mohamed Yaseen.
Olad told BBC's Newsday that this was not recorded when he was checked in.
Wachunguzi walisema kuwa mwili wa mtu mmoja ulipatikana katika kitongoji cha Balad, takriban kilomita 30 kaskazini mwa Mogadishu.
Utafiti wa kina haujafanyika kufikia sasa kujua iwapo kweli ndiye anayeshukiwa ndiye.
Je bomu hilo lilitegwa vipi?
Utawala nchini Somalia ulitoa Video inayoonesha watu wawiliwakimkabidhi abiria mmoja anayeshukiwa kuwa mlipuaji wa kujitolea mhanga kitu kinachoonekana kama Laptop kabla ya mlipuaji huyo kuabiri ndege hiyo ya Daallo iliyokumbwa na mkosi huo.
Msemaji wa serikali anasema kuwa watu hao ndio washukiwa wakuu katika ulipuaji uliotokea juma lililopita kwa ndege ya abiria ilipolazimika kutua kwa dharura baada ya bomu kulipuka ikiwa angani.
Inasadikika kuwa mmoja kati ya watu walioleta kipakatilishi hicho alikuwa ni mfanyikazi wa shirika linalohudumu katika uwanja huo wa ndege wa Mogadishu.
Bwana Abdisalam Aato anasema kuwa kifaa hicho kinachofanana na kipakatilishi ndicho kinachoshukiwa kuwa ni kilipuzi kilichosababisha ndege ya Daallo kurejea ardhini mara moja muda mchache baada ya kupaa ikiwa na abiria.
Takriban watu 20 wamekamatwa wakiwemo wale wawili walionaswa kwenye video hiyo .
Mtaalamu wa maswala ya usalama wa ndege bwana David Learmont, anashuku iwapo hilo linaweza kubainika kupitia kwa video hiyo moja iliyotolewa na serikali ya Somalia.
Hata hivyo anakiri kuwa wafanyikazi katika viwanja vya ndege kote duniani ndio watepetevu na ndio wanaoruhusu mashambulizi kuendelea kutokea katika ndege za abiria.
''Njia rahisi kabisa ya kuingiza na kutega bomu katika ndege za abiria ni kuwasajili wahudumu wenye vibali vya kuingia katika maeneo ya kuegesha ndege'' alisema Learmont
Rubani a ndege hiyo hata hivyo hakuficha lolote ''hakuna usalama wa aina yeyote katika uwanja wa ndege wa Mogadishu'' alisema Vlatko Vodopivec
Kwanini bomu hilo halikusababisha madhara makubwa?
Rubani wa ndege hiyo alikiri kuwa walikuwa na bahati sana kwa sababu ndege hiyo ndio ilikuwa imepaa tu na haikuwa mbali ndio sababi=u ilitua kwa haraka na ghafla.
''kama ndege hii ingekuwa katika anga ya mbali ,,,bila shaka ndege ingeanguka'' aliiambia shirika la habari la AFP.
Mtaalamu wa usalama wa ndege David Denman anasema laiti shimo hilo lingetokea ndege hiyo ikiwa imepanda hadi zaidi ya futi elfu 20,000 juu ya usawa wa bahari hata shimo dogo kabisa lingesababisha hewa kusaki watu nje ya ndege hiyo na hivyo ndege ingepasuka mara mbili au zaidi.
''Msidharau mlipuko huo mdogo eti haukusababisha madhara makubwa ,ilikuwa bahati hawakuwa wamefyonza hewa kutoka ndani ya ndege ilikuiruhusu kupaa kwa urahisi zaidi''
Wangelikuwa wamefanya hivyo bila shaka ndege ingepasuka msamba na hakuna aliyekuwemo angepatikana akiwa hai'' alisema bwana Denman
''Bahati ilikuwa yakwamba bomu hilo lililipuka dakika 15 tu baada ya ndege hiyo kupaa na wakati huo ndege ikiwa takriban futi elfu 11,000'' alielezea mtaalamu huyo wa mabomu.
Je kwanini bomu hilo lililipuka wakati huo ?
Ni vigumu kubaini bila ya kuwahoji waliopanga njama hiyo.
Kwanini hakuna kundi lililodai kutekeleza shambulizi hilo ?
Mwandishi wa idhaa ya kisomali ya BBC Abdirahman Koronto kuna kundi la wapiganaji waliodai kutekeleza shambulizi hilo.
Kwa kawaida kundi la wapiganaji wa al-Shabab, hutuma taarifa wakidai kutekeleza mashambulizi muda mchache tu baada ya tukio lenyewe.
Kundi hilo lilmewahi kutumia bomu iliyofichwa ndani ya Laptop yapata miaka mitatu iliyopita.
Hata hivyo katika tukio hilo la mwaka wa 2013 walichanganya bomu iliyotegwa ndani ya kipakatilishi na ile iliyotegwa ndani ya gari.
Wakati huo walifanikiwa kuua watu 6 katika shambulizi hilo.
Sio mara ya kwanza shambulizi limetekelezwa na likaenda bila kundi lolote kudai kupanga.
Kwa mfano kunashambulizi lililotekelezwa dhidi ya kundi la madaktari kutoka Syria lililosababisha 3 kati yao na mwenyeji wa kuuawa hakuna aliyedai kutekeleza shambulizi hilo.
Hata kundi la wanamgambo wa al-Shabab walipinga kutekeleza mauaji hayo.
Ndovu aingia mjini na kuhangaisha watu India...BBC
Ndovu mwitu aliingia katika mji mmoja katika jimbo la Bengal Magharibi nchini India na kuhangaisha wakazi kwa saa kadha.
Maafisa walitumia vishale vyenye dawa ya kutuliza wanyama kumtuliza.
Lakini tayari alikuwa ameharibu nyumba, magari na pikipiki kabla ya kudhibitiwa.
Hata hivyo, maafisa wa mji huo wa Siliguri wanasema hakuna mtu aliyeumizwa wakati wa kisa hicho.
Ndovu huyo baadaye alipelekwa kwenye hifadhi moja ya wanyama ambayo hutumiwa kuwafuga ndovu na wanasema wanapanga kumrejesha porini baadaye.
Watu walioshuhudia wanasema ndovu huyo aliingia mjini kutoka msitu ulio karibu na alionekana kuwa na wasiwasi na kukanganyikiwa.
Kisa hicho kimetokea siku chache tu baada ya chui kuingia shuleni na kujeruhi watu sita katika eneo la Bengaluru.
Maafisa walitumia vishale vyenye dawa ya kutuliza wanyama kumtuliza.
Lakini tayari alikuwa ameharibu nyumba, magari na pikipiki kabla ya kudhibitiwa.
Hata hivyo, maafisa wa mji huo wa Siliguri wanasema hakuna mtu aliyeumizwa wakati wa kisa hicho.
Ndovu huyo baadaye alipelekwa kwenye hifadhi moja ya wanyama ambayo hutumiwa kuwafuga ndovu na wanasema wanapanga kumrejesha porini baadaye.
Watu walioshuhudia wanasema ndovu huyo aliingia mjini kutoka msitu ulio karibu na alionekana kuwa na wasiwasi na kukanganyikiwa.
Kisa hicho kimetokea siku chache tu baada ya chui kuingia shuleni na kujeruhi watu sita katika eneo la Bengaluru.
Magufuli akerwa na hali wodi ya wazazi Muhimbili...BBC
Rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi kuchukua hatua baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alifika huko jana baada ya msafara wake kusimamishwa na wazazi waliomtaka kwenda akajionee jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.
Alifika mwenyewe na kujionea hali ya msongamano mkubwa wa wazazi uliosababishwa na uhaba wa vitanda na nafasi finyu katika wodi hiyo.
"Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso, na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua," alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisimamishwa na kina mama hao alipokuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumuona na kumjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Bin Ally.
Mwezi Novemba, siku chache baada ya kuchukua hatamu, Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika sehemu kuu ya ya hospitali hiyo ya Muhimbili na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan baadhi waliolala chini.
Alifanyia mabadiliko usimamizi wa hospitali hiyo na kumteua Prof Lawrence Mseru kuwa mkurugenzi mkuu.
Nestle yavunja mkataba na IAAF...BBC
Kampuni kubwa ya chakula pamoja na vinywaji Nestle imevunja ufadhili wake katika shirika la riadha duniani IAAF ,ikihofia kwamba kashfa ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli inyokumba shirika hilo huenda ikaharibu sifa zake.
Kampuni hiyo kutoka Uswizi imesema kuwa imechukua uamuzi huo mara moja.
Hatahivyo ,rais wa shirikisho hilo Lord Coe amesema kuwa amekasirishwa na uamuzi huo na hataukubali.
Mwezi uliopita,kampuni ya nguo za michezo Adidas ilivunja mkataba wake na shirikisho hilo.
Tumeamua kuvunja uhusiano wetu na mpango wa riadha miongoni mwa jina katika IAAF mara moja.
Uamuzi huu unatokana sifa mbaya kutoka kwa umma kutokana na madai ya ufisadi na utumizi wa dawa za kutumia nguvu dhidi ya IAAF.
Tunaamini kwamba hili huenda likaathiri vibaya sifa na sura yetu na hivyobasi tumevunja mkataba wetu na IAAF,ulioanzishwa 2012.
Tumeelezea IAAF kuhusu uamuzi wetu na sasa tunasubiri jibu lao kwamba ushirikiano wetu umekwisha.
Utafiti:Farasi hubaini hisia za mwanadamu...BBC
Farasi huweza kubaini kati ya mtu aliye na furaha na aliye kasirika kwa kuangalia uso wa mwanadumu,utafiti umesema.
Katika jaribio, kwa kutumia picha za mwanamume wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Sussex walionyesha kwamba farasi wanaofugwa nyumbani huchukizwa na sura zilizokasirika.
Wanasayansi hao wanasema kuwa ufugaji huo huenda umewawezesha farasi kuelewa tabia za binaadamu.
Matokeo hayo yamechapishwa katika jarida la Biology Letters.
Kundi hilo lilifanya vipimo vyake kwa kuwasilisha picha nyingi mbele ya farasi 28.
''Mtu mmoja anashikilia farasi huku mwengine akishikilia picha,''alielezea mtafiti Amy Smith.
Matokeo yake ,alielezea ni kwamba waliangalia picha za watu waliokasirika na jicho lao la kushoto.
Akili za wanyama zimeumbwa kana kwamba hisia zinazotolewa na jicho la kushoto huangaziwa na eneo la kulia la ubongo ambalo hutumiwa kuangazia hisia mbaya.
Watafiti hao pia waliweka vipimo vya moyo katika moyo wa farasi hao ,ambavyo vilibaini kwamba nyuso zilizokasirika hufanya myoyo ya wanyama hao kudunda kwa haraka.
Matokeo kama hayo yameripotiwa miongoni mwa mbwa na kuzua maswali kuhusu ni vipi kuishi na binaadamu kuna badili tabia za wanyama hao.
Al-Shabab ''lashambulia uwanja wa ndege Somalia''..BBC
Wanamgambo wa kiislamu wamefanya mashambulio ya makombora katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Walioshuhudia wanasema wanamgambo hao walirusha makombora hayo usiku kucha na kuwa milipuko kadhaa ilisikika karibu na uwanja mkuu wa ndege.
Hata hivyo hakuna ripoti yoyote kuhusu majeruhi, lakini ripoti zinasema kuwa safari kadhaa za ndege kuelekea Mogadishu zimefutiliwa mbali.
Uwanja wa ndege wa Mogadishu unalindwa vikali na unakaribiana na kambi ya wanajeshi wa kulinda amani wa muungano wa Afrika nchini Somalia.
Kikosi hicho cha wanajeshi elfu ishirini na mbili wa muungano huo wanaunga mkono serikali ya nchi hiyo katika harakati zake za kupambana na wanamgambo wa kiislamu.
Ofisi za umoja wa mataifa pia ziko katika kambi hiyo sawa na ubalozi wa mataifa ya kigeni.
Kufikia sasa hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini wapiganaji wa Al shabaab walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, wamefanya mashambulio kadhaa ya mabomu mjini humo.
Wakati huo huo uchunguzi unaendelea kufuatia mlipuko wa bomu katika ndege moja ya abiria iliyotokea tarehe mbili mwezi huu.
Mlipuko huo ulitokea katika ndege inayomilikiwa na shirika la Daalo muda mfupi tu baada ya kuruka kutoka uwanja huo wa ndege wa Mogadishu na kusababisha kifo cha mlipuaji huyo wa kujitolea, hali iliyoilazimisha ndege hiyo kutua kwa dharura.
Watu kum na watano wamekamatwa kuhusiana na shambulizi hilo la Ndege.
Shule zafungwa Bangalore kwa sababu ya chui... BBC
Shule zaidi ya 100 zimefungwa nchini India baada ya chui mwingine kuripotiwa kuonekana viungani mwa mji wa Bangalore.
Wakazi wametakiwa kutotoka nje kwa sababu ya usalama wao. Polisi na maafisa wa misitu wanamsaka mnyama huyo.
Chui dume aliingia katika shule moja Jumapili na kuwajeruhi watu sita waliojaribu kumkamata.
Mwanasayansi na mfanyakazi wa idara ya misitu ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwenye operesheni ya kumdhibiti mnyama huyo iliyodumu saa 10.
Chui wa sasa anadaiwa kuonekana na mfanyakazi wa ujenzi Jumatano eneo la Nallurhalli, karibu na Whitefield, mwandishi wa idhaa ya Kihindi ya BBC Imran Qureshi aliyeko Bangalore anasema.
"Tumeunga makundi ya maafisa wa misitu na polisi ambao wanazunguka eneo hilo wakimtafuta. Lakini kufikia sasa hatujaona dalili za kuwepo kwake,” afisa mkuu wa huduma za wanyamapori jimbo la Karnataka Ravi Ralph amesema.
Chui huyo alijeruhi watu sita shule ya Vibgyor Jumapili
Mnamo Alhamisi, serikali ya jimbo hilo iliagiza kufungwa kwa shule 129, zikiwemo 53 za serikali.
“Tutaamua baadaye jioni iwapo shule zitaendelea kufungwa Ijumaa au la. Tunasubiri uamuzi wa maafisa wa misitu na polisi,” afisa wa serikali KS Satyamurthy amesema.
Sensa ya karibuni zaidi ilionesha kuna karibu chui 14,000 nchini India.
Rwanda lawamani juu ya Burundi.
Maafisa wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani wamesema wameona ushahidi kuwa serikali ya Rwanda imekua ikichangia matukio ya machafuko katika nchi jirani ya Burundi.
Inaelezwa kuwa Rwanda imekuwa ikiwapa silaha na mafunzo wakimbizi waliokimbia machafuko nchini Burundi.
Burundi imetumbukia mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe tangu Rais Pierre Nkurunziza alipoamua kugombea uraisi kwa muhula wa tatu.
Maafisa hao wa Marekani wanasema taarifa walizo nazo kutoka kwa maafisa wenzano waliopo kwenye kambi za wakimbizi nchini Rwanda, zinasema Rwanda imekuwa ikihusika na vurugu katika nchi jirani ya Burundi.
Akihojiwa na Bunge la Congress mmoja wa wanadiplomasia amesema kuna taarifa za kuaminika kwamba wakimbizi wa Burundi ikiwa ni pamoja na watoto wamekuwa wakipewa mafunzo katika makambi nchini Rwanda, na kufunzwa kupambana kwa silaha na serikali.
Ghasia zilizuka nchini Burundi mwaka jana baada ya rais wa nchi hiyo kusema atagombea kwa muhula wa tatu.
Serikali za nchi hizi mbili zina makabila ambayo ni mahasimu, na kuna ongezeko la wasiwasi wa kimataifa kuwa mgogoro mwingine wa kikabila inaweza kuota mizizi katika eneo hilo.
Tayari Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda amekanusha tuhuma hizo ambapo amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kutafuta mikakati ya kutatua mgogoro ya kisiasa badala ya kutafuta nani wa kumtupia lawama.
Aliyeishi muda mrefu na moyo wa kupandikizwa afariki... BBC
Mwanamume aliyeishi muda mrefu duniani na moyo wa kupandikizwa amefariki, baada ya kuishi miaka 33 na moyo huo.
John McCafferty aliambiwa alikuwa amesalia na miaka mitano pekee ya kuishi alipofanyiwa upasuaji katika hospitali ya Harefield, Middlesex Uingereza mnamo tarehe 20 Oktoba 1982.
Mjane wake Ann amesema: "Miaka 30 iliyopita ilikuwa ya furaha sana. Tulitembea na kujionea ulimwengu.”
Bw McCafferty, kutoka Newport Pagnell eneo la Buckinghamshire, alifariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 73 akitibiwa hospitali ya Milton Keynes.
Alitambuliwa na Guiness World Records mwaka 2013 kuwa mtu aliyeishi muda mrefu zaidi na moyo wa kupandikizwa.
Wakati huo alisema: “Ninataka rekodi hii ya dunia iwapo moyo wote wanaosubiri kufanyia upasuaji wa kupandikiza moyo na kwa wale, ambao kama mimi, wamebahatika kupandikizwa moyo mwingine kama mimi.”
Bw McCafferty alipatikana na maradhi ya moyo akiwa na umri wa miaka 39.
Alifanyiwa upasuaji na Sir Magdi Yacoub.
Upasuaji wa kwanza wa kupandikiza moyo uliofanikiwa ulifanyiwa nchini Afrika Kusini mwaka 1967 na Prof Christiaan Neethling Barnard na kundi la matabibu 30 katika hospitali ya Groote Schuur, Cape Town.
Mgonjwa wao, Louis Washkansky, alifariki siku 18 baada ya kupokea moyo mpya.
Monday, 1 February 2016
Alshabab wavamia tena eneo la Mpeketoni Kenya...BBC
Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika eneo la Bondeni Mpeketoni katika jimbo la Lamu.
Waliotekeleza shambulizi hilo wanadaiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al Shabab ambao walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi.
Walioshuhudia shambulizi hilo wanasema kuwa wapiganaji wao waliwaruhusu waislamu kuondoka huku wale waliokuwa wakristo wakishambuliwa kwa visu na wengine kwa risasi .
Wenyeji wanasema kuwa shambulizi hilo lilitokea mwendo wa saa kumi alfajiri.
Watu wengi waliachwa wakiuguza majeraha.
Nyumba kadha za wenyeji ambao sio waislamu zilichomwa moto.
Operesheni ya uokozi inayoendeshwa na maafisa wa usalama inaendelea katika eneo lililoko karibu na msitu wa Boni ambako inadaiwa wavamizi hao walitorokea.
Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni
Hii si mara ya kwanza kwa eneo hilo la Mpeketoni kushambuliwa na wanamgambo wa Al Shabab.
Mwaka 2014 wanamgambo wa Al shabab walishambulia mji wa Mpeketoni na kuua zaidi ta watu 60.
Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni walifikishwa mahakamani majuzi na kusomewa mashtaka dhidi yao.
Mwanamke aliyemuua mumewe asamehewa Ufaransa...BBC
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amemsamehe mwanamke aliyekuwa amefungwa jela miaka 10 kwa makosa ya kumuua mumewe.
Mume wa Jacqueline Sauvage alikuwa mlevi aliyezoea kumpiga na alikuwa amembaka yeye na mabinti zake kwa miaka mingi.
Jacqueline alisema mumewe huyo pia alimnyanyasa mwana wao wa kiume, ambaye baadaye alijiua.
Watu zaidi ya 400,000 walikuwa wametia saini ombi la kumtaka Bw Hollande amwachilie huru.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 ataondoka gerezaji katikati mwa mwezi Aprili, mawakili wake wamesema.
Siku ya tarehe 10 Septemba 2010, siku ambayo mwanawe alijiua, Sauvage alimpiga risasi mumewe mara tatu akitumia bunduki.
Alipatikana na hatia na kufungwa jela miaka 10 gerezani Oktoba 2014, na kifungo chake kikadumishwa Desemba 2015 baada ya rufaa yake ya kujitetea akisema kwamba alikuwa anajikinga kukataliwa.
Kesi hiyo iliangaziwa sana Ufaransa, wengi wakitaka haki ya kutumia sababu ya kujikinga kujitetea ipanuliwe.
Walitaka watu walionyanyaswa na kudhulumiwa nyumbani waruhusiwe kutumia haki hiyo kujitetea.
Bw Hollande amefanya uamuzi wake siku mbili baada ya kukutana na mabinti watatu wa Sauvage.
Leo Kivumbi ni katika jimbo la lowa...BBC
Wagombea wa kiti cha urais wanafanya kampeni zao za mwisho katika jimbo la lowa ambapo upigaji kura wa kwanza katika uteuzi wa vyama utafanyika siku ya Jumatatu.
Kura ya maoni inaonyesha kuwa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump anaongoza kwa asilimia ndogo dhidi ya mwanzake Ted Cruz lakini wote hao wako mbele ya wengine.
Lakini kinyanganyiro katika chama cha Democratic kina ushindani mkali huku aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani Hillary Clinton akiwa mbele ya Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders.
Kila mgombea ambaye atateuliwa kutoka kwa kila chama atagombea urais mwezi Novemba.
Mishoni mwa wiki wagombea walifika katika jimbo lisilo na watu wengi la lowa katika dakika za mwisho za kuwarai wapiga kura ambao bado hawakuwa wamefanya uamuzi.
Mshindi wa mwisho wa chama cha Republican katika jimbo la lowa ambaye alishinda uteuzi wa chama hicho ni George Bush miaka 16 iliyopita.
Suala moja ambalo huenda likaathiri shughuli za leo ni hali ya hewa. Watabiri wa hali ya hewa wanasema kuwa huenda theluji ikashuhudiwa leo usiku.
Waliokosea hukumu China waadhibiwa...BBC
Maafisa 27 nchini China wameadhibiwa kwa kumnyonga kimakosa kijana mmoja kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo Xinhua.
Huugjilt alikuwa ana umri wa miaka 18 wakati alihukumiwa kutokana na mashtaka ya kubaka na kumuua mwanamke mmoja ndani ya choo za kiwanda mwaka 1996.
Mbakaji mmoja alikiri kufanya makosa hayo mwaka 2005 na Huugjilt kuondolewa mashtaka mwaka 2014.
Zhao Zhihong aliyekiti kutenda ubakaji huo
Kuondolewa mashtaka si jambo la kawaida nchini China na sio rahisi hukumu kubatilishwa. Maafisa 26 waliadhibiwa kwa kushuswa madaraka.
Wachunguzi katika eneo la Mongolia walikiri kushinikizwa kupata hukumu ya kesi hiyo wakati matumizi ya nguvu kusababisha mtu kukiri kuripotiwa kuongezeka nchini humo.
Wazazi wake Huugjilt walipewa dola 4800 kama msamaha kutoka kwa mahakama wakati hukumu hiyo ilipobatilishwa.
Magufuli alaani kuuawa kwa rubani porini... BBC
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema amesikitishwa sana kitendo cha kuuawa kwa rubani Mwingereza aliyekuwa akisaidiana na maafisa wa Tanzania kupambana na ujangili.
Rubani wa helkopta Kapteni Roger Gower, alifariki baada ya majangili kuifyatulia risasi na kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na askari wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
Askari mmoja wa Tanzania alijeruhiwa wakati wa kisa hicho.
Tembo watatu pia walipatikana wakiwa wameuawa.
Dkt Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua rubani huyo wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kurugenzi ya mawasiliano ya ikulu.
Polisi tayari wamewakamata washukiwa watatu kuhusiana na mauaji hayo.
Kiongozi huyo amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote.
Amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hilo na wasaidie kuwafichua watu wote wanaojihusisha na ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.
Hivi karibuni, utawala nchini Tanzania umekuwa ukikosolewa kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na uwindaji haramu wa pembe za ndovu.
Uwindaji haramu umeenea sana katika pori ya Maswa na sio tukio la kwanza ambapo wanaharakati wanaolinda wanyama wa porini wanashambuliwa na wawindaji haramu.
Meli kubwa iliyoinama yazua wasiwasi Ufaransa...BBC
Meli ya kubwa iliyoegemea upande mmoja inakaribia kufika katika pwani ya Ufaransa, maafisa wa bahari wanasema, ingawa kuna matumaini ya kuiokoa kabla ya kuzama.
Meli hiyo kwa jina Modern Express ambayo, imesajiliwa Panama, ilianza kulala upande mmoja Jumanne baada ya kutokea kwa hitilafu za kimitambo.
Mabaharia wote 22 wameondolewa kutoka kwenye meli hiyo.
Juhudi za kuisimamisha zimefeli, lakini maafisa wanasema jaribio jingine litafanywa leo Jumatatu.
Juhudi za leo zikishindikana, basi meli hiyo itagonga pwani ya Ufaransa kati ya Jumatatu usiku na Jumanne asubuhi.
Hali mbaya ya hewa ilitatiza juhudi za uokoaji Jumapili.
Meli hiyo imebeba tani 3,600 za mbao na mashine kadha za uchimbaji, na imeinama kwa pembe ya kati ya nyuzi 40 na 50.
Ina tani 33 za mafuta.
Mwaka 2002, meli ya kusafirisha mafuta kwa jina Prestige ilizama karibu na pwani ya Uhispania na kumwaga mafuta tani 50,000 na kuchafua eneo kubwa la bahari.
WHO yakutana kujadili virusi vya Zika...BBC
Shirika la Afya Duniani (WHO) leo linafanya mkutano wa dharura kujadili kuenea kwa virusi vya Zika.
Mkutano huo mjini Geneva utajadili iwapo mlipuko wa virusi hivyo unafaa kutangazwa kuwa “dharura ya kimataifa”.
Maafisa wa WHO wamesema mlipuko huo wa Zika unabadilika utoka “hatari ndogo hadi kuwa wa hatari kubwa”.
Katika visa vingi, watu walioambukizwa virusi hivyo vya Zika huwa hawaonyeshi dalili zozote, lakini virusi hivyo vinadaiwa kusababisha maelfu ya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.
Kutangazwa kwa mlipuko wa sasa wa Zika kuwa “dharura ya kimataifa ya afya ya umma” kutavifanya virusi hivyo kutambuliwa kama hatari kubwa duniani na kupelekea pesa, rasilimali na wataalamu wa kisayansi kutengwa kuangazia tatizo hilo Amerika Kusini na katika maabara kote duniani.
WHO inaangazia sana hasa baada ya kukosolewa kutokana na ilivyoshughulikia mlipuko wa maradhi ya Ebola Afrika Magharibi.
◾ Kundi laomba wenye Zika waruhusiwe kutoa mimba
◾ “Msishike mimba sasa”, mataifa yashauri wanawake
Wengi walisema ilichelewa sana katika kuchukua hatua, na huenda hilo lilichangia vifo vingi.
Katika mkutano huo wa leo, wataalamu wa kudhibiti magonjwa, wataalamu kuhusu virusi na wale wanaoangazia kutengenezwa kwa chanjo, watamfahamisha mkugugenzi mkuu wa WHO Dkt Margaret Chan habari muhimu kuhusu mlipuko wa Zika.
Wiki iliyopita, alisema: “ Kiwango cha wasiwasi ni cha hali ya juu, na pia hali ya suitafahamu.
“Kuna maswali mengi, na tunahitaji majibu upesi.”
Nigeria yaomba mkopo wa dharura... source BBC
Nigeria inaomba mkopo wa dharura wa jumla ya dola bilioni tatu unusu kutoka kwa Benki ya Dunia kujaribu kuziba pengo kwenye bajeti yake.
Uchumi wa Nigeria umeathiriwa sana na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Waziri wa fedha nchini humo Kemi Adeosun amesema amekuwa akifanya mazungumzo na maafisa wa Benki ya Dunia.
Hatua ya Nigeria kuomba mkopo wa dharura inashangaza ikizingatiwa kwamba siku chache zilizopita Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilisema haihitaji usaidizi wa kifedha.
◾ Nakala za bajeti zatoweka Nigeria
◾ Nigeria kurudisha fedha zilizoibiwa
Serikali mpya ya Rais Muhammadu Buhari ilikuwa imeacha pengo katika ufadhili wa bajeti yake katika juhudi za kujaribu kusisimua uchumi wa taifa.
Lakini tofauti kati ya mapato na matumizi imeendelea kuongezeka na kuilazimu Nigeria kuomba usaidizi kutoka nje.
Nigeria silo taifa la pekee kuathiriwa na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Azerbaijan, nchi nyingine inayozalisha mafuta kwa wingi, pia imeanza mazungumzo na Benki ya Dunia.
Uchumi wa Venezuela nao umekuwa katika hali ya tahadhari.
Kushuka kwa bei ya mafuta kulichangia sana katika kushuka kwa jumla ya mapato ya taifa Urusi mwaka jana.