Menu - Pages

Monday, 1 February 2016

Alshabab wavamia tena eneo la Mpeketoni Kenya...BBC


Watu wanne wameripotiwa kuuawa katika eneo la Bondeni Mpeketoni katika jimbo la Lamu.
Waliotekeleza shambulizi hilo wanadaiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al Shabab ambao walikuwa wamevalia magwanda ya kijeshi.
Walioshuhudia shambulizi hilo wanasema kuwa wapiganaji wao waliwaruhusu waislamu kuondoka huku wale waliokuwa wakristo wakishambuliwa kwa visu na wengine kwa risasi .
Wenyeji wanasema kuwa shambulizi hilo lilitokea mwendo wa saa kumi alfajiri.
Watu wengi waliachwa wakiuguza majeraha.
Nyumba kadha za wenyeji ambao sio waislamu zilichomwa moto.
Operesheni ya uokozi inayoendeshwa na maafisa wa usalama inaendelea katika eneo lililoko karibu na msitu wa Boni ambako inadaiwa wavamizi hao walitorokea.

Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni

Hii si mara ya kwanza kwa eneo hilo la Mpeketoni kushambuliwa na wanamgambo wa Al Shabab.
Mwaka 2014 wanamgambo wa Al shabab walishambulia mji wa Mpeketoni na kuua zaidi ta watu 60.
Washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la kwanza Mpeketoni walifikishwa mahakamani majuzi na kusomewa mashtaka dhidi yao.

Mwanamke aliyemuua mumewe asamehewa Ufaransa...BBC

Jacqueline
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amemsamehe mwanamke aliyekuwa amefungwa jela miaka 10 kwa makosa ya kumuua mumewe.
Mume wa Jacqueline Sauvage alikuwa mlevi aliyezoea kumpiga na alikuwa amembaka yeye na mabinti zake kwa miaka mingi.
Jacqueline alisema mumewe huyo pia alimnyanyasa mwana wao wa kiume, ambaye baadaye alijiua.
Watu zaidi ya 400,000 walikuwa wametia saini ombi la kumtaka Bw Hollande amwachilie huru.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 ataondoka gerezaji katikati mwa mwezi Aprili, mawakili wake wamesema.
Siku ya tarehe 10 Septemba 2010, siku ambayo mwanawe alijiua, Sauvage alimpiga risasi mumewe mara tatu akitumia bunduki.
Alipatikana na hatia na kufungwa jela miaka 10 gerezani Oktoba 2014, na kifungo chake kikadumishwa Desemba 2015 baada ya rufaa yake ya kujitetea akisema kwamba alikuwa anajikinga kukataliwa.
Kesi hiyo iliangaziwa sana Ufaransa, wengi wakitaka haki ya kutumia sababu ya kujikinga kujitetea ipanuliwe.
Walitaka watu walionyanyaswa na kudhulumiwa nyumbani waruhusiwe kutumia haki hiyo kujitetea.
Bw Hollande amefanya uamuzi wake siku mbili baada ya kukutana na mabinti watatu wa Sauvage.

Leo Kivumbi ni katika jimbo la lowa...BBC


Wagombea wa kiti cha urais wanafanya kampeni zao za mwisho katika jimbo la lowa ambapo upigaji kura wa kwanza katika uteuzi wa vyama utafanyika siku ya Jumatatu.
Kura ya maoni inaonyesha kuwa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump anaongoza kwa asilimia ndogo dhidi ya mwanzake Ted Cruz lakini wote hao wako mbele ya wengine.
Lakini kinyanganyiro katika chama cha Democratic kina ushindani mkali huku aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani Hillary Clinton akiwa mbele ya Seneta wa jimbo la Vermont Bernie Sanders.

Kila mgombea ambaye atateuliwa kutoka kwa kila chama atagombea urais mwezi Novemba.
Mishoni mwa wiki wagombea walifika katika jimbo lisilo na watu wengi la lowa katika dakika za mwisho za kuwarai wapiga kura ambao bado hawakuwa wamefanya uamuzi.
Mshindi wa mwisho wa chama cha Republican katika jimbo la lowa ambaye alishinda uteuzi wa chama hicho ni George Bush miaka 16 iliyopita.
Suala moja ambalo huenda likaathiri shughuli za leo ni hali ya hewa. Watabiri wa hali ya hewa wanasema kuwa huenda theluji ikashuhudiwa leo usiku.

Waliokosea hukumu China waadhibiwa...BBC


Maafisa 27 nchini China wameadhibiwa kwa kumnyonga kimakosa kijana mmoja kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo Xinhua.
Huugjilt alikuwa ana umri wa miaka 18 wakati alihukumiwa kutokana na mashtaka ya kubaka na kumuua mwanamke mmoja ndani ya choo za kiwanda mwaka 1996.
Mbakaji mmoja alikiri kufanya makosa hayo mwaka 2005 na Huugjilt kuondolewa mashtaka mwaka 2014.

Zhao Zhihong aliyekiti kutenda ubakaji huo

Kuondolewa mashtaka si jambo la kawaida nchini China na sio rahisi hukumu kubatilishwa. Maafisa 26 waliadhibiwa kwa kushuswa madaraka.
Wachunguzi katika eneo la Mongolia walikiri kushinikizwa kupata hukumu ya kesi hiyo wakati matumizi ya nguvu kusababisha mtu kukiri kuripotiwa kuongezeka nchini humo.
Wazazi wake Huugjilt walipewa dola 4800 kama msamaha kutoka kwa mahakama wakati hukumu hiyo ilipobatilishwa.

Magufuli alaani kuuawa kwa rubani porini... BBC

Rubani
Rais wa Tanzania John Magufuli amesema amesikitishwa sana kitendo cha kuuawa kwa rubani Mwingereza aliyekuwa akisaidiana na maafisa wa Tanzania kupambana na ujangili.
Rubani wa helkopta Kapteni Roger Gower, alifariki baada ya majangili kuifyatulia risasi na kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na askari wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
Askari mmoja wa Tanzania alijeruhiwa wakati wa kisa hicho.
Tembo watatu pia walipatikana wakiwa wameuawa.
Dkt Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua rubani huyo wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa vyombo vya sheria, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kurugenzi ya mawasiliano ya ikulu.
Polisi tayari wamewakamata  washukiwa watatu kuhusiana na mauaji hayo.
Kiongozi huyo amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote.
Amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hilo na wasaidie kuwafichua watu wote wanaojihusisha na ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.
Hivi karibuni, utawala nchini Tanzania umekuwa ukikosolewa kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na uwindaji haramu wa pembe za ndovu.
Uwindaji haramu umeenea sana katika pori ya Maswa na sio tukio la kwanza ambapo wanaharakati wanaolinda wanyama wa porini wanashambuliwa na wawindaji haramu.

Meli kubwa iliyoinama yazua wasiwasi Ufaransa...BBC

Meli
Meli ya kubwa iliyoegemea upande mmoja inakaribia kufika katika pwani ya Ufaransa, maafisa wa bahari wanasema, ingawa kuna matumaini ya kuiokoa kabla ya kuzama.
Meli hiyo kwa jina Modern Express ambayo, imesajiliwa Panama, ilianza kulala upande mmoja Jumanne baada ya kutokea kwa hitilafu za kimitambo.
Mabaharia wote 22 wameondolewa kutoka kwenye meli hiyo.
Modern
Juhudi za kuisimamisha zimefeli, lakini maafisa wanasema jaribio jingine litafanywa leo Jumatatu.
Juhudi za leo zikishindikana, basi meli hiyo itagonga pwani ya Ufaransa kati ya Jumatatu usiku na Jumanne asubuhi.
Hali mbaya ya hewa ilitatiza juhudi za uokoaji Jumapili.
Meli hiyo imebeba tani 3,600 za mbao na mashine kadha za uchimbaji, na imeinama kwa pembe ya kati ya nyuzi 40 na 50.
Ina tani 33 za mafuta.
Mabaharia
Mwaka 2002, meli ya kusafirisha mafuta kwa jina Prestige ilizama karibu na pwani ya Uhispania na kumwaga mafuta tani 50,000 na kuchafua eneo kubwa la bahari.

WHO yakutana kujadili virusi vya Zika...BBC

Zika
Shirika la Afya Duniani (WHO) leo linafanya mkutano wa dharura kujadili kuenea kwa virusi vya Zika.
Mkutano huo mjini Geneva utajadili iwapo mlipuko wa virusi hivyo unafaa kutangazwa kuwa “dharura ya kimataifa”.
Maafisa wa WHO wamesema mlipuko huo wa Zika unabadilika utoka “hatari ndogo hadi kuwa wa hatari kubwa”.
Katika visa vingi, watu walioambukizwa virusi hivyo vya Zika huwa hawaonyeshi dalili zozote, lakini virusi hivyo vinadaiwa kusababisha maelfu ya watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.

Kutangazwa kwa mlipuko wa sasa wa Zika kuwa “dharura ya kimataifa ya afya ya umma” kutavifanya virusi hivyo kutambuliwa kama hatari kubwa duniani na kupelekea pesa, rasilimali na wataalamu wa kisayansi kutengwa kuangazia tatizo hilo Amerika Kusini na katika maabara kote duniani.
WHO inaangazia sana hasa baada ya kukosolewa kutokana na ilivyoshughulikia mlipuko wa maradhi ya Ebola Afrika Magharibi.
◾ Kundi laomba wenye Zika waruhusiwe kutoa mimba
◾ “Msishike mimba sasa”, mataifa yashauri wanawake
Wengi walisema ilichelewa sana katika kuchukua hatua, na huenda hilo lilichangia vifo vingi.
Virusi
Katika mkutano huo wa leo, wataalamu wa kudhibiti magonjwa, wataalamu kuhusu virusi na wale wanaoangazia kutengenezwa kwa chanjo, watamfahamisha mkugugenzi mkuu wa WHO Dkt Margaret Chan habari muhimu kuhusu mlipuko wa Zika.
Wiki iliyopita, alisema: “ Kiwango cha wasiwasi ni cha hali ya juu, na pia hali ya suitafahamu.
“Kuna maswali mengi, na tunahitaji majibu upesi.”

Nigeria yaomba mkopo wa dharura... source BBC

Mafuta
Nigeria inaomba mkopo wa dharura wa jumla ya dola bilioni tatu unusu kutoka kwa Benki ya Dunia kujaribu kuziba pengo kwenye bajeti yake.
Uchumi wa Nigeria umeathiriwa sana na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Waziri wa fedha nchini humo Kemi Adeosun amesema amekuwa akifanya mazungumzo na maafisa wa Benki ya Dunia.
Hatua ya Nigeria kuomba mkopo wa dharura inashangaza ikizingatiwa kwamba siku chache zilizopita  Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilisema haihitaji usaidizi wa kifedha.
◾ Nakala za bajeti zatoweka Nigeria
◾ Nigeria kurudisha fedha zilizoibiwa
Serikali mpya ya Rais Muhammadu Buhari ilikuwa imeacha pengo katika ufadhili wa bajeti yake katika juhudi za kujaribu kusisimua uchumi wa taifa.
Lakini tofauti kati ya mapato na matumizi imeendelea kuongezeka na kuilazimu Nigeria kuomba usaidizi kutoka nje.
Nigeria silo taifa la pekee kuathiriwa na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Mafuta
Azerbaijan, nchi nyingine inayozalisha mafuta kwa wingi, pia imeanza mazungumzo na Benki ya Dunia.
Uchumi wa Venezuela nao umekuwa katika hali ya tahadhari.
Kushuka kwa bei ya mafuta kulichangia sana katika kushuka kwa jumla ya mapato ya taifa Urusi mwaka jana.