Menu - Pages

Thursday, 27 November 2014

Misikiti iliofungwa yafunguliwa Mombasa.........



Misikiti minne iliofungwa na maafisa wa polisi wiki iliopita baada ya kuchukuliwa na vijana wenye itikadi kali za kiislamu hatimaye imefunguliwa.
Hatua ya kuifungua misikiti hiyo ya Minaa,Sakina,Musa na Swafaa inajiri baada ya siku mbili za mazungumzo kati ya viongozi wakuu wa kiislamu,wataalam na uongozi wa kaunti ya Mombasa.
Maelezo ya mazungumzo hayo yalioandaliwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho na kaunti kamishna Nelson Marwa yamefanywa kuwa siri.
Kabla ya misikiti hiyo kufunguliwa ,viongozi wa kiislamu pamoja na wataalam walilazimika kuajiri kiongozi wa dini wa kila msikiti na kubuni kamati maalum ya kusimamia misikiti hiyo ya kisauni na majengo mjini Mombasa.





''Hatutaki wajisikie kana kwamba serikali ina wakandamiza.Tumewapa mda wa kuzungumza na kuamua kuhusu kamati za misikii hiyo na viongozi w dini ambao watakuwa wakisimamia ibada.Watatupatia majina na kufikia kesho{leo} misikiti hiyo itafunguliwa'',alisema bwana Marwa ambaye ndio mwenyekiti wa kamati ya usalama kaunti ya Mombasa.
Duru zinaarifu kuwa miongoni mwa wale walioalikwa katika mazungumzo hayo ni viongozi wakuu wa kiislamu wakiwemo wawakilishi kutoka baraza kuu la waislamu nchini Kenya SUPKEM,barasa kuu la ushauri wa maswala ya kiislamu na baraza la maimamu na wahubiri nchini Kenya CIPK.
Misikiti hiyo ilifungwa wiki iliopita na maafisa wa usalama baada ya uvamizi katika Msikiti wa Musa pamoja na msako wa kuwanasa zaidi ya watu 250 ambao baadaye walishtakiwa kwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi.
Maafisa wa polisi pia walionyesha baadhi ya silaha na nakala ambazo wanasema zilipatikana katika msikiti huo.
Muda mchache baada ya kukamatwa kwao,magenge ya vijana walizua ghasia na kuanza kuwashambulia raia wasio kuwa na hatia katika vituo vitatu vya mabasi pamoja na makaazi katika eneo la kisauni.
Wakati wa ghasia hizo watu watatu walidungwa visu na kufariki huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya.
Viongozi wa kiislamu mjini Mombasa na maeneo mengine ya nchi wamekuwa wakitaka kufunguliwa kwa misikiti hiyo ambayo imekuwa katikati ya utata kuhusu madai kwamba ilikuwa inatumiwa kuwafunza vijana itikadi kali mbali na kuhifadhi silaha kinyume na sheria.

No comments:

Post a Comment