Menu - Pages
▼
Tuesday, 9 December 2014
Al Jazeera yaihusisha Kenya na mauaji.....source BBC
Shirika la habari la Al Jazeera limepeperusha ripoti ambayo imehusisha maafisa wa usalama wa Kenya na mauaji ya viongozi wa dini ya kiisilamu pamoja na washukiwa wa ugaidi.
Taarifa hiyo ya ufichuzi iliyopeperushwa Jumatatu, ilionyesha baadhi ya maafisa wa polisi wanaofanya kazi yao kwa usiri mkubwa wakikiri kuwaua baadhi ya viongozi wa kiisilamu wanaosemekana kufunza mafunzo yenye itikadi kali ya kiisilamu pwani ya Kenya.
Ripoti hio http://goo.gl/wYV91g ambayo ilikuwa ni kanda ya video yenye polisi hao wakikiri kuwaua waisilamu mjini Mombasa, iliwekwa kwenye mtandao wa YouTube na shirika hilo.
Inaonyesha sura za polisi hao zikiwa zimefichwa huku wakisimulia ambavyo wamekuwa wakiwaua watu wanaonekana kua wenye kutoa mafunzo ya itikadi kali na wanaotatiza usalama wa nchi.
Wengi ambao wameuawa na maafisa hao ni washukiwa wa ugaidi waliodaiwa kutoa mafunzo ya itikadi kali za kidini.
Walisema kuwa wampokea mafunzo yao kutoka kwa mashirika ya kijasusi ya kimataifa ikiwemo MI5 la Uingereza na Mossad la Israel.
Mmoja wa maafisa anasema wamewaua washukiwa wengi sana wa ugaidi akiwemo Sheikh Abubakar Shariff Makaburi mnamo mwezi April.
Taarifa hizo zilichapishwa kwenye vyombo vingine vya habari vikizungumzia mauaji ya kisiri ya washukiwa wa Ugaidi yanayofanywa na maafisa wa polisi waliopata mafunzo ya hali ya juu nchini Kenya.
Baadhi ya maafisa hawa wanatoka kitengo cha polisi wa kupambana na ghasia au GSU na shirika la kitaifa la ujasusi.
Mmoja wao alinukuliwa akisema katika kanda hio ....''sisi hupewa taarifa tu na kisha kutekeleza matakwa ya wakuu wetu. Huwa tunamuua yule mshukiwa tuliyetumwa kumuu na kazi hii huwa tunaifanya kwa usiri mkubwa sana,''
wote waliohojiwa wanasema wao hupokea mafunzo ya hali ya juu mno kabla ya kufanya kazi yao kwa umakini mkubwa.
Ripoti hiyo ya Al Jazeera inasema kuwa washukiwa wa ugaidi huuawa badala ya kupelekwa mahakamani.
Sio mara ya kwanza kwa mashirika ya usalama nchini Kenya kutuhumiwa kwa mauaji ya washukiwa wa ugaidi kwa siri.
Hata hivyo, Serikali ya Kenya imetoa taarifa kupinga ripoti hio inayodai kuwa polisi nchini humo walihusika na mauaji ya washukiwa wa ugaidi.
Ripoti hiyo iliyoonyeshwa na runinga ya al jazeera ilidai kuwa maafisa kadhaa wa polisi walikiri kuwa kikosi maalum cha usakama kilihusika na kutoweka na hatimaye mauaji wa washukiwa wa ugaidi, hasa viongozi wa dini ya kiislamu waliokiswa kuwa na siasa za misimamo mikali.
Lakini katibu wa wizara ya habari nchini Kenya amesema ripoti hiyo haina msingi wowote na kutaka shirika hilo la habari kuiomba msamaha.
No comments:
Post a Comment