Menu - Pages
▼
Friday, 2 January 2015
BAADA YA KUKAA KIMYA HATIMAYE YULE ASKOFU ALIYEKULA PESA ZA ESCROW AELEZA ALIVYOPEWA MGAO HUO.
Askofu Nzigilwa.
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, amevunja ukimya kuhusu mgao wa Sh. milioni 40 alioupata kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering & Marketing Limited, James Rugemalira.
Ukimya wa Askofu Nzigilwa unatokana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya waliokuwa wanahisa wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ikiwamo VIP kuingia katika mgogoro na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Taarifa kwa vyombo vya habari jana ilisema fedha alizopewa Askofu Nzigilwa na Rugemalira, zilikuwa za matoleo kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.
Alisema kiutaratibu siyo vibaya kwa waumini kutoa michango na matoleo kwa Kanisa na watumishi wake.
Katika taarifa hiyo ambayo Askofu Nzingilwa alipotafutwa alithibitisha kwamba ni yake, alifafanua kuwa alifahamiana na familia ya Rugemalira tangu akiwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Makongo Juu, Dar es Salaam na hata baada ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wameendelea kushirikiana na kuwasiliana katika masuala mbalimbali ya kikanisa na kijamii.
“Samahani nipo kwenye kazi fulani hatuwezi kuongea kwa sasa.
Ni kweli kuna taarifa nimeitoa leo kwa Tumaini Media na nimewaambia waitume pia kwa vyombo vingine vya habari,” alisema Askofu Nzingilwa alipowasiliana na NIPASHE kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms).
Askofu Nzingilwa katika taarifa hiyo aliyoisaini juzi, alisema mwanzoni mwa Februari 2014, Rugemalira alimuomba namba ya akaunti yake ya benki ya Mkombozi ili aweke matoleo yake.
Alisema aliombwa akaunti yake na Rugemalira mapema Februari, mwaka jana na kwamba hakuwahi kufahamu kiasi cha fedha kilichowekwa kwenye akaunti yake hadi alipoangalia taarifa ya benki Februari 27, mwaka jana iliyoonyesha aliingiziwa Sh. milioni 40.4.
“Niliwasiliana na Rugemalira na kumwambia nimeona kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yangu, naye akaniambia hayo ni matoleo yake ambayo anaamini yatasaidia katika shughuli zetu za kitume na kichungaji. Nikamshukuru kwa ukarimu huo mkubwa,” alibainisha Askofu huyo.
Alisema matoleo hayo yalipokelewa kwa moyo mnyofu kutoka kwa mtu anayefahamika kwa ukarimu wake katika kusaidia Kanisa na watumishi wake.
“Kampuni anazomiliki na biashara anazofanya Rugemalira kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, haviwezi kumpa shaka mtu anayemfahamu kuhusu uwezo wake au kampuni yake kutoa mchango mkubwa kama huo,” alisema.
Alisema ni desturi ya kawaida katika Kanisa kwa waamini kutoa michango na matoleo mbalimbali kila mmoja kwa kadri ya uwezo na ukarimu wa moyo wake na kwamba matoleo ya waamini hutumika katika shughuli za uinjilishaji na uendeshaji wa Jimbo, Parokia na taaisi zake.
Askofu huyo aliongeza kuwa hutumika katika miradi maalum iliyokusudiwa na matoleo hayo na kwa kadri ya matakwa na lengo la mtoaji.
“Nilipokea matoleo hayo kwa roho safi na moyo mweupe na wa shukrani kama tunavyofanya siku zote tunapopokea ukarimu wa michango na matoleo ya waamini wetu. Na tangu matoleo hayo yalipotolewa Februari, mwaka jana, hakuna mamlaka yoyote iliyowahi kuniuliza ,” alifafanua na kuongeza:
“Nawaomba waamini tuendelee kujitoa kwa hali na mali katika kulijenga Kanisa la Mungu; kila aliyepewa talanta na Mungu aitumie kwa kuzalisha matunda mema ili kulijenga kanisa letu na hatimaye kuurithi ufalme wa mbinguni.”
Hata hivyo, alisema Kanisa hilo litaendelea kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki, ukweli na uadilifu, na halitarudi nyuma wala kukaa kimya katika kukemea maovu katika jamii.
UHUSIANO NA FAMILIA YA RUGEMALIRA
Alisema familia ya Rugemalira ni waumini wakatoliki wanaosali katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu, Makongo juu katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kwamba ni washiriki wazuri katika shughuli za ibada na wamekuwa na moyo mkubwa wa ukarimu katika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kanisa ndani na nje ya jimbo.
“Binafsi, nimeifahamu familia hii muda mrefu kutokana na majitoleo yao katika shughuli za Kanisa na uhusiano baina yangu na familia hiyo ulizidi kuimarika pale alipopangwa kufanya huduma za kichungaji katika Parokia ya Makongo Juu nikiwa Paroko Msaidizi, mwaka 2008,” alibainisha na kuongeza:
“Kipindi hicho ilikuwa katika harakati za ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba ya mapadre na mikakati ya ujenzi wa Kanisa jipya la Parokia na walikuwa wachangiaji wazuri katika kufanikisha.”
Hata hivyo, aliwaomba waumini wa kanisa hilo kuendelea kujitoa kwa hali na mali katika kulijenga Kanisa la Mungu.
Aidha, Askofu huyo alisema utume wa kanisa siku zote umekuwa ukiwezeshwa na kutegemezwa kwa nguvu ya Mungu Roho Mtakatifu anayeliongoza kanisa katika ukweli wote, na kwa sadaka, matoleo na michango mbalimbali ya hali na mali kutoka kwa waamini na watu wengine wenye mapenzi mema waliopo ndani na nje ya nchi.
“Kwa waumini kutoa michango na matoleo kwa kanisa na watumishi wake ni jambo la kawaida katika desturi za imani yetu tangu nyakati za mitume,” alisema Askofu Nzigilwa.
KASHFA YA ESCROW
Mei, mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliibua kashfa ya kuchotwa kwa zaidi ya Sh bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo ilipingwa vikali na baadhi ya wabunge na viongozi wa serikali na Mbunge huyo kutakiwa kufuta kauli kwa kulidanganya Bunge.
Mbunge huyo aliendelea na msimamo wake na kutaka Bunge kuunda kamati ya kuchunguza sakata hilo.Juni mwaka jana, Bunge liliagiza Ofisi ya CAG kufanya ukaguzi wa fedha hizo na ripoti yake kuwasilishwa Bungeni.
Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukamilisha kazi yake, ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uenyekiti wa Zitto Kabwe.
Kamati hiyo ilifanya uchunguzi na kuweka wazi ripoti na mapendekezo yake ya awali ambayo yalizua mjadala mkali bungeni kiasi cha kutishia Bunge kushindwa kufikia maamuzi ya pamoja na baadaye Spika Anne Makinda, aliunda kamati ya maridhiano ambayo ilikubaliana katika maazimio yaliyowasilishwa Bungeni na Zitto.
Novemba 26, mwaka jana, Zitto, aliwasilisha ripoti iliyowataja viongozi wa dini, serikali na watu wengine waliopokea fedha za Tegeta Escow.
Viongozi wa dini waliotajwa na Zitto kiasi cha fedha walichopokea kwenye mabano ni Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh. milioni 80) Askofu Eusebius Nzigirwa na Padri Alphonce Twimanye Simon (Sh. milioni 40.4), ambao walipewa fedha hizo kupitia Benki ya Mkombozi.
VIONGOZI WA SERIKALI WALIOWAJIBIKA
Desemba 16, mwaka jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alijiuzulu nafasi kutokana na ushauri alioutoa.
Desemba 22, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete, alimfukuza kazi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye katika kashfa hiyo alipokea kiasi cha Sh. bilioni 1.6, huku akimuweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Desemba 23, mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alimsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
VIONGOZI WENGINE WALIOPATA MGAWO
Viongozi waliopata mgawo wa Rugemalira Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (bilion 1.6); Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (milioni 40.4); Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona (milioni 40.4); Mbunge mstaafu Paul Kimiti (milioni 40.4); Msajili wa zamani wa Hazina na Mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (milioni 161.7).
Wamo pia Jaji Profesa Eudes John Ruhangisa (milioni 404.25) na Jaji Aloysius Mujulizi (milioni 40.4).
Watumishi wa umma ni aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa wa Rita, Philip Saliboko (milioni 40.4); aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Emmanuel Ole Naiko (milioni 40.4) na Mtumishi wa TRA, Lucy Appolo (milioni 80.8).
No comments:
Post a Comment