Menu - Pages
▼
Monday, 16 February 2015
Watoto wanashiriki mzozo wa Sudan Kusini..
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch limezituhumu serikali ya sudan kusini pamoja na vikosi vya waasi nchini humo kwa kuwasajili watoto walio na umri wa miaka 13 kupigana katika vita vya kiraia nchini humo.
Katika ripoti hiyo ambayo serikali imekana, Human Rights Watch limesema serikali imekuwa kiwasajili watoto hao, mara nyingi kwa nguvu, huku waasi waliwatumia watoto katika mzozo wa nchi hiyo ambao umeendelea kwa miezi 14 sasa.
Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za kibinadam la human rights watch daniel bekele, amesema kuwa licha ya kuwepo na ahadi kati ya serikali na upinzani ya kuacha kutumia watoto kama wanajeshi, pande zote mbili bado zinaendelea kuwasajili watoto jeshini.
Waziri wa habari wa Sudan Kusini Michael Makuei amepuuzilia mbali ripoti hiyo na kusisitiza kwamba kuna watu wengine wazima wenye uwezo wa kusajiliwa au kuajiriwa jeshini.
Lakini shirika hilo la Human Rights Watch limesema kuwa vikosi vya serikali vinachukua watoto , katika tukio moja shirika hilo limedai kuwa baadhi watoto huchukuliwa nje ya makao ya umoja wa mataifa iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo mjini Malakal.
Malakal, ni mji wenye utajiri wa mafuta, umebadilisha mamlaka mara sita tangu kuanza kwa vita Desemba mwaka wa 2013, vita ambavyo vimesababisha raia takriban 21000 kutafuta makaazi katika kambi za muda za umoja wa mataifa.
Mji huo wa malakal kwa sasa uko chini ya udhibiti wa serikali.
Shirika la umoja wa mataifa la unicef limesema mwaka uliopita watoto 12,000, wengi wao wavulana, walisajiliwa kujiunga na jeshi, la serikali au kulazimishwa kuwa wapiganaji wa waasi na wanamgambo washirika wa serikali.
Kuanzia mwanzoni mwa mwaka, huu shirika la Unicef, limefaulu kuandaa mazungumzo na kundi la waasi linaloongozwa na David Yau Yau na kuezesha kuachiliwa huru kwa watoto 3000, lakini watoto wengi wangali wanatumiwa na pande hizo mbili.
Kufuatia shinikizo la kimataifa, serikali ya sudan kusini imepitisha sheria mpya inayopiga marufuku watoto kuajiriwa au kusajiliwa jeshini kabla ya umri wa miaka kumi na nane.
Vita vilianza desemba 2013 nchini humo baada ya rais wa nchi hiyo salva kirr kumtimua makamu wake riek machar kwa madai ya kujaribu kupindua serikali..
No comments:
Post a Comment