Menu - Pages

Wednesday, 28 October 2015

Matokeo ya uchaguzi Zanzibar yafutwa....source BBC


Mwenyekiti wa ZEC amesema uchaguzi huo unafaa kurudiwa

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha ametangaza kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi visiwani humo akisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi.
Kulingana na mwanahabari wa BBC aliyeko hilo Sammy Awami, mwenyekiti huyo ametangaza hatua hiyo kupitia runinga ya serikali visiwani ZBC.
Bw Jecha amesema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukaji mkubwa wa sheria za uchaguzi, kwa mujibu wa taarifa ambayo baadaye imetumwa kwa vyombo vya habari.
Amesema baadhi ya makamishna wa tume hiyo, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba "wamekuwa ni wawakilishi wa vyama vyao".
"Kumegundulika kasoro nyingi katika uchaguzi huu miongoni mwa hizo ni kubainika kwa baadhi ya vituo hasa Pemba vimekuwa na kura nyingi kuliko daftari la wapiga kura wa kituo husika."
Amesema hilo ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba "baadhi ya wapiga kura hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao vya kupigia kura".
Kadhalika, amesema kura hazikupata ulinzi mzuri hususan kisiwani Pemba ambako amesema kuwa baadhi ya mawakala wa baadhi ya vya vyama vya siasa katika kisiwa hicho walifukuzwa.
Ameongezea kuwa vijana katika eneo hilo walivamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kutaka kuzua ghasia, na pia vyama vya siasa vilionekana "kuingilia majukumu ya tume ikiwemo kujitangazia ushindi na kupelekea mashindikizo kwa tume."

Hii ni sehemu ya taarifa ya Bw Jecha

"Nimeridhika kwamba uchaguzi huu haukiwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi," amesema Bw Jecha.
"Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu."
Tangazo la mwenyekiti huyo limetolewa huku hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda visiwani humo.
Siku moja baada ya uchaguzi kufanywa, mgombea wa chama cha upinzani cha Civic United From (CUF) Seif Sharif Hamad alijitangaza kuwa mshindi, hatua iliyokemewa na chama cha CCM ambacho mgombea wake Dkt Ali Mohamed Shein amekuwa rais wa visiwa hivyo muhula unaomalizika.
Tume ya uchaguzi visiwani humo pia ilishutumu hatua ya mgombea huyo. Kabla ya kufutiliwa mbali kwa matokeo ya uchaguzi, tume hiyo ya uchaguzi ilikuwa imetangaza matokeo ya majimbo 31 kati ya majimbo 54 visiwani humo.
Hayo yakijiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania inaendelea kutoa matokeo ya uchaguzi wa urais. Kufikia sasa imetoa matokeo ya majimbo 155 kati ya majimbo 264.

No comments:

Post a Comment