Menu - Pages
▼
Tuesday, 19 May 2015
UNICEF:Watoto zaidi wauawa Sudan Kusini.
Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF linasema kuwa wavulana na wasichana wenye umri wa hadi miaka 7 wameuawa ,kutekwa na kubakwa katika ghasia za hivi majuzi nchini Sudan Kusini.
Waathiriwa wamesema kuwa makundi yaliojihami yalichoma vijiji katika jimbo la Unity.
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na vile vya waasi yameongezeka katika majuma ya hivi karibuni na kuwaacha zaidi ya watu laki moja bila makao.
Shirika la msalaba mwekundu limeonya kuhusu ukosefu wa chakula huku watu zaidi wakitoroka vita hivyo karibu na mji wa Leer wakati wa msimu huu wa upanzi.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 baada ya rais Salva Kiir kumshtumu makamu wake Riek Machar kwa jaribio la mapinduzi.
Nkurunziza awafuta kazi mawaziri 3.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewafuta kazi mawaziri watatu, huku maandamano yakiendelea katika mji mkuu kufuatia jaribio la mapinduzi, juma lililopita.
Mawaziri walioachishwa kazi ni wa Ulinzi, mashauri ya nchi za kigeni na biashara.
Mapema hii leo, polisi walifyatua risasi hewani katika mji mkuu Bujumbura, kujaribu kuutawanya umati wa vijana uliokuwa ukifanya ghasia.
EU kupambana na wahamiaji haramu.
Umoja wa ulaya umekubali kuanzisha kikosi cha Jeshi la wanamaji kwa ajili ya kupambana na wafanya biashara wanaosafirisha watu kutoka Libya.
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa EU,Federica Mogherini, amesema nia ni kuvunja mtandao unaowasafirisha wahamiaji kupitia bahari ya Mediterania.
Mogherini amesema umoja wa ulaya utaendelea kutafuta kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuhusu kikosi hicho kipya.
Lakini Serikali ya Libya inayotambulika na jumuia ya kimataifa imesisitiza kuwa itahitaji kushirikishwa katika kuratibu operesheni za kijeshi dhidi ya wahalifu hao.
Balozi wa Libya ndani ya Umoja wa Mataifa, Ibrahim Dabbashi, amesema Mamlaka za libya hazijaelezwa chochote kuhusu Operesheni hiyo kwenye milki yake.
Dabbash amesema mipango ya EU pekee haiwezi kumaliza tatizo la wahamiaji haramu isipokuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuisaidia Serikali halali ya Libya kuweza kudhibiti mipaka yake hali itakayorahisisha kukomesha wimbi la wahamiaji haramu.
Prince Charles kukutana na Gerry Adams.
Mwana wa Mfalme wa Uingereza Prince Charles anatarajiwa kukutana na rais wa Sinn Féin, Gerry Adams mwanzoni mwa ziara yake nchini Ireland Jumanne.
Bwana Adams atakuwa miongoni mwa wanasiasa watakaomlaki Prince Charles atakapoanza ziara yake ya siku nne.
Kukutana kwao huko Galway itakuwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya Ireland kati ya uongozi wa Sinn Féin na mwana familia wa Familia ya Kifalme ya Uingereza.
Mwenyekiti wa chama Declan Kearney amesema ni kukuza uelewano na kuponya makovu ya mambo yaliyopita.
Bwana Kearney amesema Gerry Adams na Martin McGuinness watakutana na mwana mfalme.
"Hii ilikubaliwa kukuza mchakato wa kutatua uonevu uliopita na kukuza uelewano na kusameheana," amesema.
Gerry Adams kiongozi wa Sinn Fein
Mwaka 2012, Bwana McGuinness alikutana na Malkia huko Belfast kutokana na wadhifa wake kamanaibu waziri wa kwanza wa Ireland Kaskazini.
Kushikana mkono kati ya Malkia Elizabeth na kamanda wa zamani wa IRA, katika ukumbi wa Lyric Theatre huko Belfast, ilichukuliwa kuwa tendo la kihistoria.
Wakati wa ziara yake Charles, akiandamana na Duchess wa Cornwall, atatembelea kijiji cha Mullaghmore katika kaunti ya Sligo - ambako baba yake mkubwa, Earl Mountbatten, aliuawa kwa bomu la IRA mwaka1979.