Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF linasema kuwa wavulana na wasichana wenye umri wa hadi miaka 7 wameuawa ,kutekwa na kubakwa katika ghasia za hivi majuzi nchini Sudan Kusini.
Waathiriwa wamesema kuwa makundi yaliojihami yalichoma vijiji katika jimbo la Unity.
Mapigano kati ya vikosi vya serikali na vile vya waasi yameongezeka katika majuma ya hivi karibuni na kuwaacha zaidi ya watu laki moja bila makao.
Shirika la msalaba mwekundu limeonya kuhusu ukosefu wa chakula huku watu zaidi wakitoroka vita hivyo karibu na mji wa Leer wakati wa msimu huu wa upanzi.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 baada ya rais Salva Kiir kumshtumu makamu wake Riek Machar kwa jaribio la mapinduzi.