Ubishi umeibuka nchini Ufaransa, baada ya ufukwe maarufu wa bahari wa Riviera kufungwa ilikumruhusu mfalme wa Saudi Arabia na familia yake kujivinjari kwa amani faraghani.
Viongozi wa mji wa Vallauriswametangaza kuwa watafunga sehemu kubwa ya ufukwe huo ilikuhakikisha usalama wa mfalme huyo familia yake na takriban ujumbe wa watu 400.
Familia hiyo ya kifalme, inatarajiwa kuishi katika jumba la kifahari lililoko huko.
Jumba hilo lililowahi wakati mmoja kuwa jumba la mapumziko la Sir Winston Churchill linatarajiwa kuzingirwa na maafisa wa usalama.
Maafisa wa Vallauris iliyoko kwenye mwambao wa Cote d'Azur, kilomita 10 kutoka kwenye ufukwe huo wanasema wamethibitisha kuwa shughuli kwenye ufukwe wa Milandore zitafungwa kwa muda wote wa majira ya kiangazi.
Hatua hiyo imewagadhabisha wakazi wa maeneo hayo ya mwambao , ambao wametishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mpango wa kuziba barabara ya ardhini kuelekea kwenye ufukwe huo.
Familia hiyo ya kifalme ya Saudi Arabia , ikiongozwa na Mfalme Salman, inamiliki jumba la kifahari ambalo Rita Hayworth alitumia kama mahala pa mapokezi ya wageni wakati wa harusi yake .
Sir Winston Churchill na Elizabeth Taylor walikua miongoni mwa wale waliolitumia kama makazi ya mapumziko.
Wakazi wa eneo hilo wamekasirishwa na shughuli za ukarabati katika eneo hilo, hasa baada ya kuwekwa kwa sakafu kubwa ya saruji kwenye mchanga ulioko ufukweni, zimeleza ripoti za wakazi wa eneo hilo.
Blandine Ackermann, rais wa shirika la wanaharakati wanaolinda mazingira katika maeneo ya Golfe-Juan na Vallauris amesema anapanga kuchukua hatua za kisheria kama ufukwe huo hautaendelea kuwa wazi na kurejeshwa katika hali yake
Maafisa wa kulinda bahari wamesema tayari kuwa chombo chochote hakitaruhusiwa kukaribia eneo hilo kwa takriban mita 300 ndani ya bahari.