Friday, 17 April 2015

Somalia yalenga kushiriki mechi za CAF


Rais wa shirikisho la soka nchini Somalia Adbi Qani anatumai kwamba taifa lake litashiriki katika michuano ya kombe la Afrika mwaka 2019 na kumaliza kiu ya taifa hilo tangu mwaka 1974.
Walishiriki katika kombe la mataifa ya Afrika mara moja kutokana na ghasia za kisiasa,ukosefu wa fedha na miundo msingi mibovu.
Pamoja na Eritrea nchi hizo mbili hazitashiriki katika mechi za kufuzu za mwaka 2017.
Ni mataifa hayo mawili katika shirikisho la soka barani afrika CAF yatakayokosa kushiriki.
Lakini Qani anaamini kwamba huu uwanja mpya ukitarajiwa kumalizwa kujengwa baadaye mwaka huu ,taifa hilo hilo linajiandaa kurudi katika michuano hiyo kabla ya kukamilika kwa muongo huu.
Share:

Waasi Ukrain: makubaliano yatashindwa


Kiongozi wa cheo cha juu zaidi anayeiunga mkono Urusi katika eneo linalothibitiwa na waasi mashariki mwa Ukrain amesema kuwa usitishwaji wa mapigano ulioafikiwa mapema mwaka huu na serikali hautadumu.
Alexander Zakharchenko aliiambia BBC kuwa maafikiano ya Minsk yangefanikiwa tu ikiwa serikali ya Ukrain ingetambua jamhuri iliyojitenga anayoiongoza eneo la Donetsk.
Bwana Zakharchenko aliongeza kuwa kile angependa kuona ni kupanuka zaidi kwa eneo hilo.
Chini ya makubaliano ya Minsk ambayo yaliungwa mkono na Urusi , Ujerumani na Ufaransa , serikali ya Ukrain ungerejesha mipaka chini ya udhibiti wake.
Mapigano yameendelea licha ya kuwepo kwa makubaliano hayo.
Share:

Washukiwa wa ugaidi wakamatwa Australia


Polisi katika jimbo la Victoria nchini Australia wanasema kuwa wamewakamata wanaume watano kufuatia oparesheni kubwa ya kupambana na ugaidi kwenye mji wa Melbourne.
Wawili kati ya wanaume hao walio na umri wa miaka 18 walikamatwa baada ya kushukiwa kupanga mashambulizi ya kigaidi yaikiwemo ya kuwalenga polisi.
Mshukiwa mwingine naye alikamatwa kufuatia sababu zinazohusiana na silaha. Shughuli za kuwatafuta washukiwa wengine zinaendelea sehemu zingine za mji wa Melbourne.
Share:

Hussein Machozi asema bado yupo hai


Mwimbaji wa wimbo ''Kafia Ghetto'' na 'Jela' Hussein machozi ameshtumu uvumi unaondelea kwamba amefariki baada ya ajali mbaya ya barabarani iliotokea katika mji wa Dodoma nchini Tanzania siku ya jumatano.
Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya habari za kifo chake zilianza kuenea katika mitandao ya kijamii baada ya ajali hiyo ambapo mtu mmoja aliyeonekana kufanana na msanii huyo alifariki kutokana na majeraha.
Hussein amesema kuwa yuko hai na buheri wa afya kupitia mtandao wake wa facebook ambapo alisema kuwa habari hizo zilimwacha mamaake na dadaake wagonjwa baada ya kuzirai waliposikia habari hizo.
Huu ndio ujumbe alioandika katika mtandao wake wa facebook.
{Nilijiandaa hapa nimekwenda mazoezini kucheza mpira, niliacha simu yangu kwenye charge na niliporudi baada ya mazoezi nakuta missed calls nyingi sana, msg na simu za mama yangu pamoja na dada, wakati najiandaa kuanza kupiga simu ghafla naanza kupata simu za watu mbalimbali kwamba nimepata ajali na kufariki, mimi nikawaambia sio kweli mimi ni mzima na nipo}
Share:

Ashtakiwa kwa kumtia mimba mwanawe


Mahakama moja mjini Bungoma nchini Kenya imemshtaki afisa mmoja wa wadi ya Bukembe kwa kulala na mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 14 kwa zaidi ya miaka miwili baada ya mkewe kufariki mwaka 2013.
Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya,mwathiriwa ambaye ni mjamzito wa miezi minne amesema kuwa mshukiwa huyo ambaye ni babaake amekuwa akimlazimisha kufanya mapenzi naye kila usiku na kumuonya kwamba angemdhuru iwapo angemwambia mtu yeyote.
''Babaangu pia ameninyima fursa ya kwenda katika shule ya upili licha ya mimi kufanya vyema katika mtihani wa KCPE. Mwaka 2013,nilifanya vyema lakini akanilazimisha kurudia darasa. Mwaka jana nilifanya vizuri zaidi lakini anadhani kwamba iwapo nitajiunga na shule ya upili ya bweni,nitamkosesha fursa ya kufanya tendo la ngono nami'',.Mwathiriwa aliiambia mahakama.
Hakimu mwandamizi Peter Ireri alimwachilia mtuhumiwa kwa dhamana ya shilingi laki moja ama pesa taslimu shilingi elfu ishirini.
Share:

Kanye West azindua biblia yake


Kanye West Hujulikana sana kwa maringo yake,lakini kwa kweli Kanye West asingekufuru na kujitambulisha kama mungu katika biblia hiyo.
Kitabu hicho kitukufu kimebadilishwa na kuwa Biblia ya sasa kwa jina ''Yeezus'' na amini usiamini kila neno la Mungu katika kitabu hicho limeondolewa na badala yake msanii huyo wa muziki wa kufoka foka ameweka jina lake.
Kulingana na gazeti la The Independence nchini Uingereza,kitabu hicho kinasema kuwa katika kizazi hiki ,Kanye West ndio mkubwa na vilevile kiongozi wa kidini
Kitabu hicho kinaongezea kwamba ''katika utangulizi wetu tunamsherehekea Kanye West na vile alivyotufanyia katika maisha yetu''

Ijapokuwa Kanye hajatoa tamko lolote kuhusu wadhfa huo aliojipatia,amekuwa akijifananisha na Mungu hapo mbeleni.
''Mungu alinichagua mie,alinitengezea njia.Mimi ni chombo cha mungu'',alisema mwaka 2009.
''Lakini kinachoniudhi maishani mwangu ni kwamba sitawahi kujiona nikicheza muziki moja kwa moja''.,aliongezea.

Wasanii wengine waliofananishwa na Yeezy ni Marilyn Monroe na Michael Jackson.
Share:

18 waaga katika ajali Tanzania


Watu wasiopungua 18 wameuawa katika ajali ya gari mkoa wa Mbeya Kusini Magharibi mwa Tanzania baada ya basi dogo la abiria kuanguka na kutumbukia kwenye bonde lenye maji.
Mwandishi mmoja wa habari aliyefika eneo la ajali ameeleza kuwa basi hilo dogo limetumbukia bondeni katika eneo lenye mteremko mkali na kona.
Polisi wanachunguza chanzo cha ajali, lakini walioshuhudia wanadai dereva wa gari hilo alikuwa akiwakimbia madereva wengine
waliotaka kumlazimisha aunge mkono mgomo wa utoaji huduma unaoendelea kwa safari za kati ya Mbeya na Kyela.
Imeelezwa kuwa madereva wa mabasi ambayo kwa kawaida hutoa huduma kati ya eneo la Kyela na Mbeya mjini walikuwa katika mgomo,
na kwamba hawakufurahishwa na basi hilo dogo kuendelea kutoa huduma ndipo wakawa wanamfukuza hatimaye akashindwa kulidhibiti
Ajali hiyo ni mwendelezo wa ajali mbaya za barabarani kuhusisha magari ya abiria ambazo zimetokea Tanzania kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Share:

Wageni waendelea kushambuliwa A Kusini


Kumekuwa na mashambulizi zaidi usiku dhidi ya biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.
Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira kutawanya umati kusini mwa mji wa Johannesburg ambapo gari na nyumba vilichomwa moto.
Msemaji wa polisi aliiambia BBC kuwa karibu raia mia mbili wa kigeni walikimbilia usalama kwenye kituo cha polisi lakini wakaondoka muda baadaye.

Usalama umedumishwa kufuatia mashambulizi yaliyowalenga raia wa kigeni ambapo watu watano wameuawa.
Rais Jacob Zua amelaani ghasia hizo na maandamano ya amani mjini Durban siku ya Alhamisi yalihudhuriwa na zaidi ya watu elfu kumi.
Share:

Mwanzilishi wa IS auawa nchini Iraq


Runinga nchini Iraq imeripoti kuwa Izzat Ibrahim al-Douri, ambaye wakati mmoja alikuwa makamu wa Rais Saddam Hussein na mmoja wawaanzilishi wa kundi la Islamic State nchini Iraq, ameuawa.
BBC bado haijapata taarifa rasmi ya kuthibitisha kifo chake, lakini picha na maelezo kuhusu kifo cha Bwana Al Douri imeripotiwa pakubwa.
Iwapo taarifa hiyo ni kweli, kifo chake kitakuwa hatua kubwa kwa serikali ya Iraq dhidi ya makundi ya Jihadi.
Al Douri ambaye daima ana masharubu mekundu, alikuwa mfalme katika kilabu kwenye kadi zilizotolewa ili kusaidia majeshi ya Marekani kutawambua wanachama katika utawala wa Saddam Hussein, mnamo mwaka 2003.
Share:

Raia wa Burundi waandamana dhidi ya rais


Polisi nchini Burundi wamerusha mabomu ya kutoa machozi na maji, ili kuwatawanya mamia ya waandamanaji katika mji mkuu Bujumbura.
Maandamano hayo ni ya kumpinga Rais Pierre Nkurunziza, kutowania tena kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu ujao, unaopangiwa kufanyika mwezi Juni.
Mwaandishi wa BBC mjini Bujumbura, anasema kuwa malori makubwa yanayobeba vitoa machozi yamewekwa tayari kukabiliana na waandamanaji hao kote katika mji huo.
Anasema kuwa wazazi wamekimbia shuleni ili kuwaondosha watoto wao na kuwapeleka nyumbani.
Bwana Nkurunziza hajasema hadharani iwapo atawania kiti cha urais kwa muhula mwingine, lakini kuna tetesi kuwa ana mpango wa kufanya hivyo.
Share:

Blog Owner

Blog Owner
FESTO MDEMU

Blog Archive

Flag


Total Pageviews

Translate

Powered by Blogger.