Wednesday, 5 August 2015

Wasifu wa Edward Lowassa


Umoja usio rasmi wa vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania unajulikana kwa jina la Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kusubiri kwa muda hatimaye umemtangaza Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Lowassa anagombea kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku vyama vingine vitatu vikimuunga mkono. Hii inatokana na sheria za Tanzania ambayo haitambui umoja wa vyama.
Kabla ya kujiengua chama Tawala chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa amekuwa mwanachama wa CCM kwa muda wa miaka 38, ambapo alijiunga na chama hicho mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu mwaka 1977.
Hatua ya mwanasiasa huyo mashuhuri nchini Tanzania kuamua kujiunga na chama cha upinzani Chadema, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuelekea uchaguzi mkuu, kumebadilisha kabisa upepo wa kisiasa nchini Tanzania, na hasa uchaguzi mkuu ujao.

Lowassa alikuwa Maziri Mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008 kabla ya kujiuzuLu wadhifa huo kufuatia sakata la kashfa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya kuzalisha umeme ya ki-Marekani Richmond Development Company LLC ya Houston Texas.
Hata hivyo wakati anatangaza kuhamia kwake Chadema, Lowassa alikanusha katu katu kuhusika kwa namna yoyote na kashfa hiyo na kudai kuwa yeye alifuata tu amri kutoka kwa ‘wakubwa’ walio juu yake.
“Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa

Kuhama kwake kunamfanya Lowassa kuwa ndie kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa wa CCM kukihama chama hicho tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo mwaka 1992.
Mwanajeshi wa zamani na aliyewahi kupigana wa vita kati ya Uganda na Tanzania mwaka 1978/79, Lowassa aliiambia hadhara kwamba akiwa kama mtu mwenye uchungu na nchi yake isingekuwa rahisi kubaki ndani ya CCM huku akiona chama hicho kimepoteza mwelekeo na sifa ya kuongoza nchi.
Lowassa amekimbilia upinzani baada jina lake kukatwa wakati alipoomba kuwa mgombea urais kupitia chama tawala CCM katika uchaguzi mkuu ujao utakafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Wakati mchakato wa CCM wa kumtafuta mgombea wao wa urais ulipoanza, Lowassa ndiye aliyekuwa kinara wa wagombea wote 42. Kila kona aliyozunguka, mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono.
Wakati chama cha CCM kilimtaka kila mgombea apate sahihi za wadhamini 450 lakini Lowassa alipata sahihi za wadhamini zaidi ya 700,000.

Hata hivyo mchujo wa chama ulipofanyika jina lake lilikatwa mapema kabla hata ya kupelekwa kwenye vikao vya vya juu vya chama hicho. Ambapo baadae Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa mgombea kupitia chama tawala CCM.
Lowassa ameushutumu mchakato CCM wa kutafuta mgombea urais akiuita kuwa ulijaa chuki na mizengwe dhidi yake, hali ambayo aliifananisha na ‘ubakaji wa demokrasia’
“Nitakuwa mnafki nikisema bado nina imani na CCM. CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia”, alisema, na kuongeza “kama Watanzania hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM”
Wakati sakala la Richmond lilipoibuka miaka michache tu iliyopita, Chadema ilimfanya limsakama Lowassa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa nchini. Lakini wakati chama hicho kinamkaribisha kuwa mwanachama wao, kiligeuka na kusema hakuna mtu msafi nchini na kwamba hawawezi kuacha kumpokea mwanasiasa mwenye mtaji mkubwa wa wafuasi kama Lowassa.
Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa shughuli za serikali. Bado anaendelea kufahamika kwa jina la utani la ‘mzee wa maamuzi magumu’.

Moja ya mafanikio makubwa ya uwaziri mkuu wake ni jitihada kubwa na mafanikio ya upatikanaji wa fedha za kujenga chuo kikuu cha Dodoma. Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007.
Lowassa ni mashuhuri pia kwa kusimamia mpango wa serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za kata ambazo uliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto wengi kupata nafasi shuleni.
Mtoto wa Mzee Ngoyai Lowassa, ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa serikali ya kikoloni, Lowassa ameanza harakati zake za kuwania urais tangu mwaka 1995 lakini inaarifiwa kwamba rais wa kwanza wa Tanzania Mwl Julius Nyerere alimkatalia kushika nafasi hiyo. Wafuasi wa Lowassa wamekuwa wakiyatupilia mbali madai hayo
Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2005, Lowassa hakutaka kuwania urais, lakini badala yake alimnadi rafiki yake wa siku nyingi Rais wa sasa Jakaya Kikwete ambaye alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80.
Share:

China ni haramu kuhifadhi mayai ukiwa hujaolewa


Mjadala mkali umeibuka nchini China baada ya serikali kupiga marufuku kwa uhifadhi wa mayai kwa wanawake ambao hawajaolewa.
Aidha mayai ya wanawake walioolewa wanaweza kuhifadhi mayai iwapo tu wanapata matibabu ya saratani ama matibabu ambayo yatadhuru kizazi chao.
Marufuku ya aina hii si jambo geni kwa raia wa China ambao tayari wanastahimili sheria kali ya kupanga uzazi.
Hata hivyo,ripoti zilipoibuka kuwa muigizaji Xu Jinglei alikwenda Marekani kuhifadhi mayai yake ya uzazi ndipo wachina wakang'amua kuwa huenda sheria hiyo inawalemga maskini.

Maelfu ya wachina wameikashifu sheria hiyo wakisema kuwa ni ya kibaguzi kwa misingi ya jinsia.
Aidha wengine wanahoji kwanini serikali inaingilia kati maswala ya kibinafsi na mambo ya kijamii.
Mjadala huu ulitibuka mwezi Julai baada ya Xu Jinglei alipokiri kuwa ni kweli amehifadhi mayai yake huko Marekani tangu mwaka wa 2013.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alisema alichukua uamuzi huo kwani hajui ni lini hamu ya kupata mtoto itamwandama.
Siku ya jumapili televisheni ya kitaifa ya CCTV ilitoa ripoti kuhusiana na swala hilo na kuonyesha athari zake na kusema marufuku hiyo haina uhusiano na upangaji uzazi.
Ripoti hii ilisisimua watu katika mitandao ya kijamii ambao wengi wamekuwa wakiitupia dongo serikali.
Share:

Boti la abiria lazama ziwa Victoria Kenya


Boti moja iliyokuwa imebeba abiria 23 imegongana na mtumbwi wa wavuvi na kuzama katika ziwa Victoria Magharibi mwa Kenya.
Taarifa za awali zilikuwa zimetoa idadi hiyo kuwa 200 lakini maafisa wa usalama nchini Kenya wamethibitisha kuwa idadi ya abiria kwenye boti hiyo ilikuwa 23.
Watu 21 wameokolewa.
Miili ya watoto wawili imepatikana ikielea kwenye ziwa hilo.
Afisa huyo ameiambia BBC kuwa waliwaokoa watu 14 walipowasili katika eneo la tukio kabla ya kuwanusuru wengine saba waliporejea mara ya pili.
Wavuvi wanne waliokuwa kwenye mtumbwi wa pili pia waliokolewa.
Kwa mujibu wa walionusurika, boti hilo lililokuwa limewabeba abiria liligonga mtumbwi wa wavuvi kisha zote mbili zikazama majini.
Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi hii leo.

Ajali hiyo imetokea karibu na visiwa viwili vidogo ndani ya ziwa Victoria viitwavyo Kiwa na Remba Magharibi mwa Kenya.
Boti hiyo iliyokuwa na abiria ilikuwa inaelekea Sori kutoka kisiwa cha Remba.
Shughuli za uokoaji zinaendelea huku maafisa wa idara za serikali ya Kenya na wavuvi wakishirikiana kuwanusuru abiria hao.
Share:

Japan yakumbuka shambulio la Heroshima


Raia wa Japan leo wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 70 tangu shambulio la kwanza la bomu la Atomiki kutekelezwa mjini Heroshima.
Takriban watu laki moja na arobaini walikadiriwa kupoteza maisha baada ya Ndege ya Marekani kudondosha bomu ambalo liliuharibu mji huo tarehe 6 mwezi Agosti mwaka 1945.
Watu elfu sabini walipoteza maisha papo hapo, huku wengine wa idadi kama hiyo walipoteza maisha kutokana na athari za mionzi ya sumu.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema kumbukumbu ya Heroshima inasisitiza uhitaji wa kufanya jitihada ya kupiga vita matumizi ya Nuklia.
Shambulio la Heroshima lilifuatiwa na shambulio jingine la bomu la Atomiki katika mji wa Nagasaki.
Japan ilijisalimisha siku kadhaa baadae, hatua iliyomaliza vita ya pili ya dunia.
Share:

Hofu baada ya boti iliyojaa wahamiaji kuzama Libya


Waokoaji wanaendelea na shughuli ya kuwasaka mamia ya wahamiaji waliotumbukia baharini baada ya boti walimokuwa wakisafiria kwenda Ulaya kuzama majini katika bahari ya Mediterrania karibu na ufuo wa Libya.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa takriban watu 700 walikuwa kwenye mtumbwi huo uliozama baada ya kukumbana na mawimbi makali.
Wanajeshi wa majini kutoka Ireland wanakisia kuwa idadi kubwa ya watu wamekufa maji.
Aidha shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka Medecins Sans Frontieres (MSF) limeonya kuwa huenda kukazuka maafa makubwa kufuatia idadi kubwa ya abiria waliokuwa kwenye mtumbwi huo uliozama.
Inakisiwa kuwa takriban wahamiaji 2,000 walikufa maji kwanza mwanza wa mwaka huu wakijaribu kufika ulaya kupitia bahari hiyo ya Mediterranea
Meli nne za uokozi na ndege tatu zimetumwa huko kujaribu kunusuru maisha ya wahamiaji hao.

Walinzi wa Ufuo wa bahari ya Uitaliano wamesema boti hiyo ya uvuvi iliyokuwa imebeba mamia ya wahamiaji.
Inavyoelekea boti hiyo ilikumbwa na dharuba lakini pia ilipenduka pale watu walipokurupuka upande mmoja walipoona chombo kingine kilichokuwa kikienda kuwasaidia.
Zaidi ya watu 150 wameokolewa lakini wengine wengi wanahofiwa wamekufa maji.
Msemaji wa shirika linalohusika na maswala ya wahamiaji IOM, Leonard Doyle ameiambia BBC kuwa
''Lazima tukumbuke kuwa hawa ni watu ambao hawajazoea usafiri wa baharini kwahivyo waliogopa.''
''Na wakati walipoona chombo kingine kinakuja kuwaokoa wakataharuki na kukurupuka upande mmoja''.

Hilo ndilo tunalokariri kuwa hao walanguzi wa kusafirisha watu hawajali kabisa kuhusu maisha ya wahamiaji hao licha ya kuwa wamewalipa pesa nyingi kwa safari hizo hatari''.
Kwamba mkasa wa aina hii unaweza kutokea wakati ambao hata watu wamepelekewa chombo cha kuwaokoa karibu yao ni jambo la kusikitisha sana.
Share:

Blog Owner

Blog Owner
FESTO MDEMU

Blog Archive

Flag


Total Pageviews

Translate

Powered by Blogger.