Hatimaye Malaysia, Thailand na Indonesia zimekubaliana kuwapa makazi ya muda wahamiaji elfu saba waliokwama kwa siku kadhaa kwenye pwani ya mataifa hayo.
Hayo yameafikiwa na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa hayo katika mkutano uliokuwa ukiendelea mjini Kuala Lumpur.
Mawaziri hao wamesema kuwa hatua hiyo ya muda ya kuwapa usaidizi wakimbizi hao,wanaotoka kwa kabila dogo la waislamu wa Rohingya kutoka Mynmar na Bangladesh,
kutaipa muda jamii ya kimataifa kuwatafutia sehemu ya kudumu, katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Mataifa hayo matatu ya Malaysia, Indonesia na Thailand, yamekosolewa sana kwa kukataa kuwaruhusu wahamiaji hao kuingia katika mataifa yao.
Mynmar ilikataa kuhudhuria mkutano huo na badala yake ikaandika barua ikielezea namna ya itakavyokabiliana na swala hilo la uhamiaji.
Msemaji wa shirikisho linalosimamia maswala ya wahamiaji ILO Jeff Labovitz ameiambia BBC kuwa hatua hii ya dharura itasaidia sana kuokoa maisha ya maelfu ya wakimbizi ambao wamekuwa wakihangaika baharini bila chakula wala muundo msingi wa afya.
Wavuvi nchini Indonesia waliwaokoa zaidi ya wahamiaji 100 siku ya jumatano
Bado kuna hofu kuhusu usalama na afya ya wale waliokwama baharini ambao wanahitaji chakula na maji.
Maelfu ya raia kutoka Bangladesh na Waislamu jamii ya Rohingya wamekuwa katika bahari ya Andaman kwa majuma kadhaa sasa baada ya serikali ya Indonesia kubadili sheria ilikukabiliana na walanguzi wa watu kupitia bahari na ardhi yake.
Thailand,Malaysia na Indonesia zilikuwa zimekataa kuwaruhusu wamahiaji kuingia katika pwani za nchi zao
Huku hayo yakijiri, mashua moja iliyokuwa imewabeba wahamiaji mia nne, na ambayo ilikuwa imenyimwa ruhusa ya kutia nanga katika mataifa matatu ya bara Asia, sasa imewasili katika kisiwa cha Aceh, nchini Indonesia.
Mashua hiyo imekuwa baharini kwa miezi miwili unusu ikiwa imewabeba wahamiaji wa kiislamu wa kabila la Rohingya kutoka nchini Myanmar.
Mashua hiyo iliyopigwa picha na BBC juma lililopita ilipokuwa imekwama katika maji ya mipaka ya Thailand, ilikuwa na tatizo la Injini.