Mwalimu mkuu wa shule moja ya kiislamu mjini Melbourne, Australia amedaiwa kuwazuia wasichana katika shule hiyo kutoshiriki katika maswala ya michezo kwa hofu kwamba huenda wakapoteza ubikira.
Wanafunzi wa kike katika chuo cha Al-Taqwa mjini Truganina pia walizuiwa kucheza soka kwa kuwa majeruhi huenda yakawafanya kuwa tasa kulingana na fairfax.
Wasimamizi wa shule hiyo kwa sasa wanachunguza madai hayo yaliowasilishwa dhidi ya Mwalimu mkuu Omar Hallak ambaye awali alizua hisia kali baada ya kusema kuwa wapiganaji wa Islamic state walikuwa wakiungwa mkono na mataifa ya magharibi.
Katika barua iliondikwa na wizara na kuchapishwa na The Age,mwalimu mmoja wa zamani alisema kuwa:''Anaamini kwamba iwapo wasichana wataruhusiwa kukimbia huenda wakapoteza ubikra wao.Mwalimu huyo pia ana ushahidi wa kisayansi unaosema kuwa iwapo wasichana watajijeruhi,kupitia kuvunjika mguu wakati wanapocheza soka huenda ikawafanya kuwa tasa''..
Mwalimu huyo amedai kwamba Bwana Hallak aliwazuia wanafunzi wa kike kutoshiriki katika mashindano ya wilaya ya mbio za marathon mwaka wa 2013 na 2014.