Wanamgambo wa kiislamu nchini Nigeria wametoa picha mpya za video lakini Kiongozi wa Boko Haram ambaye huwa anaonekana kwenye video zao, Abubakar Shekau hakuonekana kwenye picha hizo za video.
kutoonekana kwa Shekau kwenye Video hiyo kumeleta hali ya wasiwasi kuhusu kuwepo kwa hali ya mgawanyiko ndani ya kundi hilo.
Takriban watu 13 wameuawa siku ya jumanne katika shambulio la bomu katika Soko la Ng'ombe mjini Maiduguri, mji ambao uliwahi kuwa ngome ya Boko Haram, Kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Katika picha ya video ya dakika 10, msemaji huyo amekanusha taarifa zilizotolewa na Jeshi la Serikali kuwa linadhibiti miji yote kutoka mikononi mwa wanamgambo.
Ameonyesha vitambulisho vya wanajeshi akisema kuwa wameuawa, na kuonyesha mabaki ambayo amedai ya ndege ya kijeshi waliyoidungua.
Msemaji aliyekuwa amebeba bunduki na huku uso wake ukiwa umefunikwa, amesema video hiyo ilirekodiwa sambisa, msitu unaozunguka hifadhi.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari,amesema kuwa vikosi vya kijeshi viko kwenye doria mjini Maiduguri na kuhakikisha kuwaondoa wanamgambo hao katika eneo hilo.
Baadae wiki hii, Buhari atakutana na Viongozi wenzie wa nchi jirani kwa ajili ya kuzungumzia mikakati ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kiislamu.
Takriban watu milioni moja na nusu wamekimbia makazi yao, na mamia zaidi wametekwa tangu kuanza kwa harakati za kundi hilo mwaka 2009.
Zaidi ya Watu 15,500 wameuawa katika mapigano.