Maelfu ya watu wanatarajiwa kuandamana katika bara-bara za miji ya Washington na New York kupinga mauaji ya wanaume weusi wasiokuwa na silaha yaliyofanywa na polisi wa Marekani, ili kulitaka bunge lilinde wananchi.
Taarifa iliyotolewa na kiongozi wa kutetea haki za raia, Al Sharpton, ilieleza kuwa bunge linahitaji kuchukua hatua kubadilisha sheria na hali bara-barani.
Kati ya wataohudhuria maandamano hayo ni familia za Michael Brown, kijana aliyeuwawa katika jimbo la Missouri, na Eric Garner, ambaye alikufa wakati anakamatwa mjini New York.
Kesi za askari polisi waliohusika na vifo hivyo zilifutwa na kuzusha maandamano kote Marekani.