Makubaliano kuhusu muundo wa baadaye wa mpango wa nyuklia wa Iran, yamefikiwa baada ya mazungumzo na mataifa sita makubwa yaliyokuwa yakifanyika nchini Uswisi.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Iran itapunguza uwezo wake wa kurutubisha madini ya urani huku ikiahidiwa kuondolewa vikwazo kwa awamu.
Rais Barack Obama amesema ni "uelewano wa kihistoria" uliofikiwa na Iran.
Mataifa makubwa ya dunia na Iran sasa yanalenga kuandika mkataba kabambe ifikapo Juni 30.
Muundo wa mkataba ulitangazwa na Umoja wa Ulaya na Iran baada ya siku nane za majadiliano mjini Lausanne.
Mazungumzo kati ya mataifa makubwa matano jumlisha moja yaani-Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Urusi pamoja na Ujerumani- na Iran katika mkutano uliofanyika mjini Lausanne, uliendelea na kupitiliza muda uliopangwa wa kufikia tarehe 31 Machi.
Mwandishi wa BBC kutoka mjini Lausanne, Barbara Plett Usher, anasema baada ya kupitiliza muda uliopangwa na siku mbili za majadiliano ya kina kati ya Iran na mataifa sita makubwa duniani wameelezea muundo wao uliofikiwa katika mkutano huo kama mafanikio makubwa.
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya,Federica Mogherini, alisoma taarifa ya pamoja ikielezea vipengele vikuu, ambavyo ni kupunguza vinu vya uchakataji wa fito za nyuklia, kubadili zana za kutengenezea nyuklia na ahadi ya kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran.
Makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo si ya maandishi, sio rasmi, bali yanajenga msingi wa kufanyika mazungumzo ya kina.
Lakini waanzilishi wa mazungumzo haya wanasherehekea mafanikio makubwa yaliyofikiwa, ambayo wanasema ni ya kihistoria.
Iran imekuwa ikikana madai ya mataifa ya magharibi kuwa mpango wake wa nyuklia unalenga kutengeneza silaha za nyuklia. Iran imeingia katika mazungumzo haya ili kuona inaondolewa vikwazo.
Katika mahojiano na BBC, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ilifikia hatua alishawishika kujitoa katika mazungumzo hayo lakini anasema cha msingi wameweza kupenya vikwazo vilivyojitokeza katika awali.
Rasimu ya mazungumzo hayo pia imepongezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye amesema anaamini "yatachangia hali ya amani na utulivu katika eneo hilo".
Mkuu wa sera ya nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametangaza mkataba huo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif, akisema hiyo ni "hatua ya maamuzi" iliyofikiwa.
Urusi imepongeza mkataba huo kuwa ni hatua ya kutambua mpango wa nyuklia wa Iran usio na masharti na ambao ni salama.
Lakini kiongozi wa Israel, Benjamin Netanyahu amemwaambia Rais Obama kwa njia ya simu kwamba mkataba huo ambao umejikita katika muundo uliokubaliwa, unatishia uwepo wa Israel.
Kwa upande wake Rais Obama amemwambia Bwana Netanyahu kwamba mkataba huo kwa namna yoyote ile unaondoa wasiwasi kwao kuwa Iran ni kinara wa kufadhili ugaidi na vitisho dhidi ya Israel.
Mkataba huo pia umekosolewa na wajumbe wa baraza la Congress la Marekani ambao wanataka wabunge wa Marekani kuwa na haki ya kupitia kila makubalino ya mwisho yanayofikiwa katika mkataba huo.
Nao wananchi wa Iran wanaoishi nchini Uswisi wameelezea kufurahishwa na mpango huo.