Kumbu kumbu ya mauaji ya Kimbari nchini Rwanda
Shahidi mmoja muhimu wa uchunguzi
unaofanyika kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda ambaye alikuwa
akitarajiwa kuhojiwa na majaji Nchini Ufaransa kuhusu kudunguliwa kwa
ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, anasemekana
kutekwa nyara na kutoweka jijini Nairobi.
Idara ya Polisi Nchini Kenya imekanusha kumtia mbaroni Emile Gafirita.
Majirani
wa Emile Gafirita wanasema kuwa walisikia milio ya breki za gari na
kamsa pale alipokuwa akirejea nyumbani muda mfupi kabla ya usiku wa
manane Jumatatu usiku na kuwaona watu wawili wakimtia pingu na kumrusha
kwenye gari.
Idara ya Polisi Nchini Kenya inasema kuwa hawajamtia mbaroni.
Jina
la bwana Gafirita liliibuka katika kesi ya hivi majuzi Nchini Rwada,
pale alipotajwa kama askari wa zamani katika kikosi cha ulinzi cha Rais
Paul Kagame.
Majaji wawili wa Ufaransa, Marc Trevidic na Nathalie
Poux, walikuwa wakipanga kumhoji ili atoe ushahidi mjini Paris kuhusiana
na mzinga ulioshambulia na hatimaye kuiangusha ndege iliyombeba Rais wa
zamani wa Rwanda hayati Juvenal Habyarimana mnamo mwezi Aprili ya mwaka
1994.
Mauaji ya Habyarimana yaliibua mapigano makali ya kikabila
yaliyosababisha mauwaji ya zaidi ya watu laki nane, wengi wao waTusti na
wahutu wenye siasa za kadri.