Menu - Pages
▼
Wednesday, 3 June 2015
Boko haram yatoa video nyingine..
Wanamgambo wa kiislamu nchini Nigeria wametoa picha mpya za video lakini Kiongozi wa Boko Haram ambaye huwa anaonekana kwenye video zao, Abubakar Shekau hakuonekana kwenye picha hizo za video.
kutoonekana kwa Shekau kwenye Video hiyo kumeleta hali ya wasiwasi kuhusu kuwepo kwa hali ya mgawanyiko ndani ya kundi hilo.
Takriban watu 13 wameuawa siku ya jumanne katika shambulio la bomu katika Soko la Ng'ombe mjini Maiduguri, mji ambao uliwahi kuwa ngome ya Boko Haram, Kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Katika picha ya video ya dakika 10, msemaji huyo amekanusha taarifa zilizotolewa na Jeshi la Serikali kuwa linadhibiti miji yote kutoka mikononi mwa wanamgambo.
Ameonyesha vitambulisho vya wanajeshi akisema kuwa wameuawa, na kuonyesha mabaki ambayo amedai ya ndege ya kijeshi waliyoidungua.
Msemaji aliyekuwa amebeba bunduki na huku uso wake ukiwa umefunikwa, amesema video hiyo ilirekodiwa sambisa, msitu unaozunguka hifadhi.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari,amesema kuwa vikosi vya kijeshi viko kwenye doria mjini Maiduguri na kuhakikisha kuwaondoa wanamgambo hao katika eneo hilo.
Baadae wiki hii, Buhari atakutana na Viongozi wenzie wa nchi jirani kwa ajili ya kuzungumzia mikakati ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kiislamu.
Takriban watu milioni moja na nusu wamekimbia makazi yao, na mamia zaidi wametekwa tangu kuanza kwa harakati za kundi hilo mwaka 2009.
Zaidi ya Watu 15,500 wameuawa katika mapigano.
Mti wa Ebola nchini Guinea..
Kuna mti unaodaiwa kusababisha mlipuko wa Ebola nchini Guinea.Kundi moja la wavulana lilimpeleka mwandishi wa BBC katika mti huu.
Walielezea kwamba siku moja waliwasha moto katika mti huo na popo wakaanguka kutoka kwa mti huo.
Waliwajaza popo hao katika mifuko na kuwala.Wakati huo hakuna mtu ambaye alikuwa amewahi kufariki na mlipuko wa Ebola.
Sokwe hawajambo kwa upishi wa vyakula..
Wanasayansi kutoka Marekani wana imani kuwa sokwe wana uwezo na akili ya kupika chakula. Wanasayansi hao wamefanya baadhi ya majaribio ambayo yameonyesha kuwa sokwe wanaweza kupika mboga za majani na wana uwezo wa kuhimili kusubiri chakula cha moto.
Hata kama wanyama wengi wana desturi ya kula chochote wanachokipata na kula moja kwa moja. Watafiti kutoka chuo kikuu cha Harvard wanasema matokeo ya utafiti walioufanya unasema kuwa Sokwe wana uwezo wa kupika na inawezekana suala hili liligundulika muda mrefu uliopita.
Hivyo wanachokihitaji sokwe ni ujuzi wa upishi kwani imedhihirika kuwa wana uwezo wa kuhimili moto.
China:Meli haikuweza kuzuia upepo mkali..
Maafisa wa Uchina wanasema meli ndogo iliopatwa na ajali na kuzama katika mto Yangtse ikiwa na abiria zaidi ya 450 haikuwa na uwezo wa kuhimili dhoruba ya upepo mkali.
Meli hiyo iitwayo The Eastern Star ilizama dakika chache tu ilipokumbwa na upepo uliovuma kwa kasi usiku wa Jumatatu.
Miaka miwili iliyopita meli hiyo ilichunguzwa kwa madai ya kukiuka vigezo vya ubora na usalama.
Hata hivyo maafisa wanasema kuwa hawajakata tamaa ya kuwapata watu walionusurika ajali ya meli na vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta walionaswa ndani ya meli hiyo kwa siku ya pili.
Watu saba wamethibitishwa kufariki huku watu kumi na tano wakiokolewa.
Kenya Airways yarudisha safari za S.Leone..
Shirika la ndege la Kenya limeanza tena kusafirisha wateja wake baina ya miji ya Nairobi na Freetown nchini Sierra Leone.
Ni shirika la kwanza kurejea nchini humo baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kuzuka mwaka uliopita.
Idadi ya maambukizi inapungua na kumekuwa na watu 12 tu waliopata maradhi hayo katika wiki moja iliyopita.
Shirika la ndege la Ufaransa pia linatarajiwa kurejea nchini humo baadaye mwezi huu.
FIFA:Interpol yataka maafisa 6 kukamatwa...
Shirika la maafisa wa polisi wa kimataifa Interpol limetoa ilani ya kukamatwa kwa watu sita wanaohusishwa na FIFA kufuatia madai ya kuhusika na ufisadi.
Agizo hilo linawalenga maafisa wanne wa mashirika makuu pamoja na maafisa wawili wakuu wa zamani wa shirikisho la soka duniani FIFA akiwemo aliyekuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo Jack Warner.
Sita hao tayari walikuwa wametajwa katika mashtaka yaliofunguliwa dhidi yao na mamlaka ya mahakama za Marekani wiki iliopita.
Ilani hiyo inawalenga watu wanaotafutwa kwa lengo la kuwakamata ili wasafirishwe hadi mataifa waliohusika na ufisadi huo ili washtakiwe ,lakini mataifa hayawezi kulazimishwa kumzuilia mtu yeyote aliyetajwa.