Tuesday, 21 April 2015

Mkenya ashinda tuzo la Goldman


Phyllis Omido mshindi wa tuzo la Goldman

Phyllis Omido, kutoka Kenya, alikuwa miongoni mwa washindi sita waliokabidhiwa tuzo hilo huko San Francisco, Marekani, Jumatatu usiku. Omindo alipata tuzo hilo kwa kutetea wakaazi wa mtaa wa mabanda wa Owino Ohuru ulioko Mikindani kaunti ya Changamwe mjini Mombasa.
Wakaazi hao wameathirika na sumu aina ya ''lead'' kutokana na kiwanda cha kukarabati betri kuu kuu kilichojengwa karibu na mtaa huo wa mabanda. Ukarabati wa betri kuu ulisababisha umwagikaji wa madini ya sumu aina ya "lead" na kuwadhuru kiafya wakaazi hao kiasi kwamba baadhi ya wanaume sasa wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya nyumbani.
Kiwanda hicho kilianza kazi mwaka wa 2009 lakini Omido alitetea wakaazi hao wa Uwino Uhuru kwa kufanya maandamano ya mara kwa mara hadi kikafungwa miaka mitatu baadae.

Omido apongezwa kwa ushindi wake

Anastacia Nambu anatueleza jinsi mumeo ameumia:''Sasa sisi tunaishi tu kama dada na ndugu kwa sababu mzee sasa hawezi kazi na si kupenda kwake ni kwa sababu ya hicho kibanda. Sisi tuliakua tunaishi karibi sana na hicho kibanda ndio kwa maana huo moshi ukaumiza mzee wangu. Ni jambo ka kusikitisha sana maanake tulitaka tupate watoto wengine lakini sasa hatuwezi. Tuna watoto wanne.''
Mzee wa kijiji Alfred Ogolla anatueleza juhudi zao za kuhimiza serikali ya Kenya iwape matibabu zimegonga mwamba. Ogolla anatueleza zaidi:''Sote hapa wazee, kina mama na watoto tunaumia sana. Mimi ninakohoa kila mara, wasichana hawawezi kuzaa kwa sababu huo moshi uliharibu nyumba zao za uzazi na watoto nao wengine miguu imejipinda na wengine nao ni vibofu hawawezi kuona. Pesa ya matibabu ni nyingi sana hatuwezi kupata dawa kila siku.''
Tuzo hilo la Omido limeandamana na kitita cha dola 175,000.

Omido afurahia tuzo lake

Je, Omido atatumiaje fedha hizo ambazo ni kama shillingi milioni 17 za Kenya?:''Kiasi kikubwa cha pesa hizi nitatumia kwa wakili maanake kesi ya wakaazi wa Owino Uhuru ingali kotini. Tunataka serikali iwape fidia na kuwalipia matibabu. Fedha zingine nitazitumia kuendeleza shirika langu lisilo la kiserikali (Centre for Justice, Governance and Environmental Action) maanake kuna mengi nataka kufanya licha ya vitisho kwa maisha yangu kwa sababu ya kupigania wakaazi wa Owino Uhuru.
''Kwa kweli nimefurahia sana kupata tuzo hili ambalo linanipa morali zaidi kwa kuwa kazi yangu imetambuliwa kote duniani. Nataka kufuata nyayo za mwanaharakati mwingine wa mazingira, merehemu Wangari Maathai. Nitazidi kutetea wanyonge kwa sababu ni wengi sana wanaumia.''
Share:

0 comments:

Blog Owner

Blog Owner
FESTO MDEMU

Blog Archive

Flag


Total Pageviews

Translate

Powered by Blogger.