Friday, 12 February 2016
Home »
» Clinton na Sanders wajibizana kuhusu Obama...BBC
Clinton na Sanders wajibizana kuhusu Obama...BBC
Wagombea urais wa chama cha Democratic Marekani Hillary Clinton na Bernie Sanders wamejibizana kuhusu Rais Barack Obama kwenye madahalo wa kwanza tangu kumalizika kwa mchujo wa New Hampshire.
Bi Clinton alijionesha kama mlinzi wa sifa za utawala wa Barack Obama, na kumshambulia Bw Sanders kwa kumkosoa rais huyo.
“Ukosoaji ambao nimekuwa nikisikia kutoka kwa Seneta Sanders, ningetarajia hilo kutoka kwa wafuasi wa Republican pekee,” Bi Clinton alisema.
Bi Clinton tena na tena alirejelea uhusiano wake mwema na Bw Obama ambaye anapendwa sana na makundi ya wachache Marekani, hasa Wamarekani weusi.
Bw Sanders kwa upande wake alijaribu sana kuweka ujumbe wake kuonesha kwamba anataka kutetea usawa wa kiuchumi na kuwasaidia Waamerika weusi.
Bi Clinton alisisitiza kwamba ujumbe wake unaambatana na vitendo, na akatilia shaka ahadi ya Bw Sanders ya kutoa huduma ya afya kwa wote na kuondoa karo katika taasisi za elimu ya juu.
“Tunawajibika kueleza kwa uwazi yale ambayo tunayoahidi na ndiyo maana hatuwezi kutoa ahadi ambazo hatuwezi kutimiza,” Bi Clinton alisema.
Wagombea wanajiandaa kwa uchaguzi wa mchujo katika majimbo ya Nevada na South Carolina, ambayo yana raia wengi wa makundi ya wachache.
Bi Clinton anajaribu kujenga upya kampeni yake baada ya kushindwa pakubwa na Bw Sanders kwenye mchujo wa New Hampshire.
Alipokea uungwaji mkono muhimu kutoka kwa kundi la wabunge weusi katika chama cha Democratic mnamo Alhamisi.
Sanders, seneta wa Vermont, alishinda New Hampshire kwa zaidi ya asilimia 22 na alishindwa mchujo wa Iowa kwa kura chache mno.
Lakini majimbo hayo yote yana Wazungu wengi.
Sasa anakabiliwa na changamoto ya kutafuta kura miongoni mwa watu wa asili ya Amerika Kusini na Mexico pamoja na Wamarekani weusi katika majimbo ya Nevada na South Carolina.
Bi Clinton anaungwa mkono sana na makundi hayo na anatarajiwa kufanya vyema Nevada na South Carolina.
Kura ya maoni ya karibuni iliyofanywa na NBC News/Wall Street Journal/Marist jimbo la South Carolina ilisema Bi Clinton anaongoza akiwa na asilimia 74 ya kura dhidi ya Bw Sanders mwenye asilimia 17 miongoni mwa wapiga kura weusi.
0 comments:
Post a Comment