Thursday, 11 February 2016
Home »
» Magufuli akerwa na hali wodi ya wazazi Muhimbili...BBC
Magufuli akerwa na hali wodi ya wazazi Muhimbili...BBC
Rais wa Tanzania John Magufuli ameahidi kuchukua hatua baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alifika huko jana baada ya msafara wake kusimamishwa na wazazi waliomtaka kwenda akajionee jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.
Alifika mwenyewe na kujionea hali ya msongamano mkubwa wa wazazi uliosababishwa na uhaba wa vitanda na nafasi finyu katika wodi hiyo.
"Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso, na ndio maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua," alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisimamishwa na kina mama hao alipokuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumuona na kumjulia hali Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubery Bin Ally.
Mwezi Novemba, siku chache baada ya kuchukua hatamu, Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika sehemu kuu ya ya hospitali hiyo ya Muhimbili na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan baadhi waliolala chini.
Alifanyia mabadiliko usimamizi wa hospitali hiyo na kumteua Prof Lawrence Mseru kuwa mkurugenzi mkuu.
0 comments:
Post a Comment